Ukiamua kuwaza juu ya mawazo ya biashara na ukaweka ufahamu wako vizuri kila sehemu utakayokwenda utakuwa unaona fursa na mawazo mbalimbali ya biashara.

Kitu kimoja kinaweza kukupoteza ni pale utakapotaka kutamani kufanya kila kitu. Kila wazo linakojua kichwani kwako unaona ni zuri na litakupa pesa unataka ulifanye. Mwisho wa siku unajikuta hata lile ambalo ulianza kulifanyia kazi hujalifikisha popote.

Sio vibaya kuwaza au kuona fursa mpya ila kama utakuwa unaona halafu unataka uchukue hatua ya kufanya kwa kila wazo zuri linalokuja kichwani mwako utajikuta unakosa mwelekeo mzuri. Unapaswa kuwa na kalamu na daftari kila wazo jipya unalopata wewe liandike chini kisha endelea kufanyia kazi ile biashara uliyonayo sasa hivi.

Kitu kingine kinaweza kuwa sababu ya wewe kutamani kila wazo jipya na zuri unaloliona ni kuweka pesa mbele. Inawezekana kabisa hamasa kubwa inayokuvuta wewe kuchukua maamuzi ya kufanya biashara Fulani ni ile faida unayokwenda kutengeneza. Ukiwa mtu ambaye kivutio kikubwa kwenye kuingia kwenye biashara ni pesa utakuta unafanya kila kitu bila kujali unakwenda wapi.

Lazima uwe na uchaguzi na uwe na mipaka hapo ndipo utaweza kufanya jambo moja na likakuletea mafanikio. Kwasababu karibu kila kitu ukisema uangalie jinsi unavyoweza kupata pesa nyingi utaona pesa.

Kitu kingine ni pesa zilizoko kwenye maandishi zinaweza zisiwe na uhalisia. Unajua unaweza kuweka mipango mizuri sana ya biashara inaonyesha jinsi utakavyotengeneza pesa nyingi utakapooanza. Lakini sasa utakapochukua hatua na kuanza utakuja kugundua kwamba bado kuna changamoto nyingi utakutana nazo kabla hujaanza kutengeneza zile pesa ulizoziandika kwenye mpango wako.
USHAURI WANGU KWAKO.

Chagua wazo moja au mawili ambayo unaweza kuanza nayo kwa sasa yafanyie kazi hadi yawe biashara iliyosimama na kuweza kujiendesha yenyewe ndipo uanze kuangalia namna ya kuingia kwenye mawazo mengine.

Kwa kupitia biashara moja utapata uzoefu ambao utakuwezesha kuanzisha mawazo mengine uliyonayo. Kuwa na mwelekeo mmoja na weka nguvu zako zote hapo hadi uone matokeo. Usikubali kuyumbishwa na kuonyeshwa kwamba unachokifanya hakifai au hakina hela uende kwenye vingine.

Kuna watu watakuja watataka kukutoa kwenye unachokifanya sasa hivi wakupeleke kwenye biashara nyingine ambazo wanakwambia zinaingiza pesa nyingi kuliko hiyo unayoifanya usikubali kwasababu utajikuta hakuna unachokifanya. Hakikisha umeweka muda, nguvu, juhudi, maarifa ya kutosha kwenye hicho unachokifanya sasa hivi kabla hujaacha au kukata tamaa.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

2 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading