Pamoja na kwamba inawezekana unaona kama mwaka huu mambo hayajaenda sawa kabisa na malengo mengi hayajatimia bado una nafasi ya kumaliza mwaka vizuri sana. Kuna mambo machache tu ukiamua kuyafanya kwa siku hizi zilizobaki baki unaweza kupata furaha kubwa sana ndani ya moyo na ukajisikia utoshelevu.

Watazame wale ambao unawapenda inawezekana ni mwenzi wako, Watoto, ndugu zako wa karibu au hata mtu yeyote ambaye unampenda. Watu hawa ndio wa muhimu sana kwako sasa ili wewe ujisikie utoshelevu ni vizuri ukahakikisha wanatabasamu. Siku hizi chache zilizobaki badala ya kutumia pesa vibaya fanya kitu kwa ajili yao ambacho wakikitazama siku zote wataendelea kukumbuka na utabaki ndani ya mioyo yao.

Watazame watu wengine kwenye jamii yako ambao unafikiri ukiwagusa kwa chochote kile ambacho umepata basi moyo wako utafurahia na pia wao wataona wamemaliza mwaka vizuri.

Huu ni muda ambao pia unapaswa kukaa karibu na Mungu wako, ni muda wa kushukuru kwa ulinzi, afya njema na nafasi hii ya pekee ya kuendelea kuishi.

Usikubali kabisa kufanya mambo ambayo yatakufanya ujute na uanze mwaka ukiwa na mawazo mengi, huu ni muda wa kutenda yaliyo mema na yakuacha alama bora nyuma yako.

Tumia muda huu kuangalia Maisha yako miaka 20 ijayo yatakuaje, angalia kile unachokifanya sasa hivi kama kweli kinakupeleka kule unakotaka kufika. Zitafakari ndoto zako na uone ni kwa namna gani tena siku 365 utakwenda kuzitumia kusogea karibu na maono yako.

Tumia muda huu kufanya vile vitu ambavyo unavipenda na watu unaowapenda, tengeneza kumbukumbu nzuri ambayo ukiangalia nyuma utakuwa unafurahia.

Muda huu sio wa kufanya starehe na kutumia fedha vibaya badala yake unapaswa kutumika vizuri ili kuacha alama kwenye Maisha ya wengine.

Muda huu sio wa kulewa, kufanya uzinzi, kutumia vibaya pesa ulizotafuta mwaka mzima halafu Januari uanze tena safari ya kukusanya nyingine.

Kwa kifupi fanya Vitu Hivi.

Zitafakari kwa Undani Ndoto zako.

Fanya Jambo kwa ajili ya Uwapendao ambalo litaacha alama ya kudumu.

Fanya Jambo Kwa ajili ya wasiojiweza.

Kuwa Karibu na Mungu Wako Zaidi.

Fanya Kile Ambacho Unakipenda (Hobby)

Yaani hakikisha unafurahi lakini katika kutenda yaliyo mema. Lolote utakalolifanya ukilikumbuka likufanye utabasamu na sio kujuta.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading