25/10/2018 Uepuke Mtego Huu Uliowaangusha Wengi.

By | October 25, 2018

Unapokuwa huna chochote cha thamani huwezi kuona mtu yeyote akionesha kuvutiwa na wewe. Wakati mwingine unaweza kuwa unafanya mambo ya maana sana lakini ukashangaa hakuna mtu anahangaika na wewe. Hakuna mtu atahangaika na wewe kama ulichokibeba hakina thamani. Hakuna mtu atapoteza muda wake kwako kama wewe huna cha maana ulichobeba.

Unapoanza kuona unapata marafiki wapya, watu ambao hukuwahi kutarajia wakija kwenye Maisha yako na kukupongeza ni vyema pia ukawa makini sana. Katika wote kuna maadui pia, kuna watu watakuja kama marafiki lakini lengo lao ni kukupoteza.

Kuna watu watakuja kama waliopendezwa na kazi zako lakini lengo lao kubwa ni kukunyonya kile unachopata. Ni sawa na chemchem ambayo inatoa maji kila mmoja anatamani aje aweke bomba la kupeleka maji kwake. Usipokuwa makini utajikuta wewe unawafanyia kazi wengine na huoni matunda yeyote katika juhudi unazoweka.

Mtego ambao nataka kukwambia utazame kwa makini unakuja pamoja na hawa watu ambao wanajifanya ni marafiki zako. Watu ambao wanajifanya wanapendezwa na kazi zako.

Kaa mbali na watu wenye dalili hizi.

Wanaotaka Maadui zao Wawe Maadui Zako.

Wanaotaka Kupata Zaidi Kuliko Kutoa,

Wamejijenga Katika Misingi ya ‘’Napata Mimi, Unakosa Wewe”

Waliojenga Misingi Yao Katika Kulipa Visasi.

Wasioamini katika falsafa ya Kuwagusa Maisha ya Wengine.

Wanaomini Katika Kuwaangusha Wengine Ili Wao Waweze Kusimama Vizuri.

Wanaoweka Fedha Mbele Kuliko Uadilifu.

Sasa Rafiki yangu haya mambo yako mengi sana. Ukiwaona watu wamefanikiwa na wana sifa Nyingi nzuri nzuri kwenye jamii sio wote sifa hizo ni za kweli. Hivyo basi ni muhimu ukajipa muda wa kuchunguza mtu ambaye anataka kuingia katika Maisha yako ya mafanikio. Wengine wamefanya mambo maovu sana kwa siri hivyo ukijiunga nao unajikuta unafanana nao.

Usikubali kuingia makubaliano yeyote ambayo hujayaelewa kwa undani. Usikubali kufanya jambo kwa kulazimishwa hakikisha wewe binafsi umejiridhisha kwamba kuna uadilifu ndani yake. Epuka mtu yule anaetaka kukupa msaada wa kitu ili aje akudai kitu kingine Baadae kwasababu tu alikusaidia.

Kuwa na msimamo tengeneza kanuni ambazo huwezi kuzivunja hata aje mtu gani kwenye Maisha yako. Hata uletewe pesa Nyingi kiasi gani.

Tupo kwenye dunia ambayo sio rahisi sana kuwajua watu wema na wabaya. Sio Kila anaejitokeza kukusaidia ana nia njema na wewe. Wengine wanatoa msaada baada ya kuona kuna mahali ataweza kuja kukufaidi baadae.

Ni vyema ukawa makini kabla ya kupokea pokea vitu vya watu. Sio kila msaada ni wa nia njema wengine wameshaona ile nyota ndani yako wanaanza kuwekeza ili baadae waweze kukinga faida vizuri.

Msaada ambao unapokea hakikisha unaweza kuja kuuridisha endapo itatakiwa au kutatokea tatizo au kutokuelewana.
Usikubali kupokea kitu chenye thamani ambayo huwezi kulipia hata kwa baadae.

Usikubali kujiingiza katika gereza mwenyewe. Sio kila anaekupa msaada ana nia njema na wewe.
Pokea msaada lakini hakikisha umefikiria kabisa madhara yake na faida zake.

Hakikisha unaweza kulipa gharama ya Msaada wowote unaopokea lakini gharama hiyo isiwe utu wako, heshima yako, au mwili wako.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Leave a Reply