Ukikutana na watu wawili wanagombana na mmoja anasema ntakupiga,ntakuumiza halafu hafanyi chochote bali anaendelea kusema t umara nyingi mtu huyo huwa ni mwoga. Mwoga hutishia kwa maneno mengi kwamba anaweza hiki anaweza kile lakini jasiri huacha kusema naweza hiki bali huonesha pale panapotakiwa kuoneshwa.

Sasa kama wewe upo kwenye uwanja wa mapambano hutakiwi kusema tena nitakupiga hapana wewe piga maana hapo sio pakusema nitakupiga uwanjani ni sehemu ya kupigana. Mfano mwingine ni kama michezo hii ya mpira au ya ngumi kabla ya mchezo wahusika hutwa kwenye vyombo vya habari na kuhojiwa. Hapo ndio sehemu ambayo unatakiwa uongee kama unasema nitashinda basi hapo ndio pa kusemea ukifika muda wa uwanjani ni wa vitendo tu.

Kama unataka kujua kama wewe ni jasiri na unaweza kuzikabili changamoto subiri wakati wa changamoto uje. Hauwi jasiri kwa kusema mimi ni jasiri bali kwa kukabiliana na vile vitu vinavyohitaji uwe jasiri.

Unapopitia magumu na bado ukaendelea kusimama basi tunasema wewe ni jasiri, wewe huitwi mshindi kabla hujaingia kwenye ushindani na ukashinda. Unaweza kujiita mshindi kabla ili kujitia nguvu na kujikumbusha lakini wakati sahihi wa kuonesha kuwa wewe ni jasiri ni ukiwa kwenye pambano.

Uwezo wako, nguvu zako, hazitajulikana kama huna chochote kigumu unachopitia maishani mwako. Acha kuogopa magumu yanapokuja kwani huo ndio wakati ambao unapimwa uwezo ulioko ndani yako. Halafu kitu kizuri ni kwamba hakuna jambo gumu litakalokuja lizidi uwezo wako hiyo ndio kanuni, kinachofanya wewe uone unapitia mambo mazito sana ni kwasababu hayo ni mapya. Yakikujia mara ya pili utaweza kuyabeba.

Usiogope wala kulalamika unapopitia magumu kwasababu hapo ndipo unakomazwa Imani yako. Imani yako unaongeza na kuwa imara Zaidi pale unapopitia magumu. Tunaweza kujua uwezo wa rubani pale anapoweza kushinda hali ya hewa mbaya aliyokutana nayo angani.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading