Mojawapo ya vitu ambavyo huanza juu havipendezi sana na sio vizuri mfano wa haraka ni shimo. Shimo linachimbwa kwa kuanzia juu kwenda chini na shimo linaweza kuwa hatari lakini vitu vingi vizuri huanzia chini na kuelekea juu. Unapojenga ghorofa lazima uanze chini kuweka msingi ndio upande juu Zaidi.

Sasa Rafiki ukitaka usiteseke, kwasababu wengi wanateseka kwa kuanzia juu wewe anza tu chini kawaida. Hakuna haja ya kuanza kujionesha una Maisha mazuri kwa pesa ambazo umezipata kwa mara ya kwanza. Hakuna haja ya kuonesha mnafurahia mahusiano yenu na wakati mmeanza juzi tu hamna hata mwezi.

Subiri kwanza jenga msingi imara ndipo uwe huru kucheza hata juu ya bati bila woga. Wewe ukitaka kuanguka kimbila juu, kimbilia kuonekana na kila mtu halafu huku chini hakuna msingi wowote uliojenga wa kukuweka imara.

Anza chini kwasababu hata ukianguka hakuna anaekuona, ukikosea hakuna anaejua sana sana wataona wale ambao wanaweza kukushauri vizuri. Ukianzia juu halafu ukakosea utakuta kila mtu akakukosoa na mwisho wa siku utakata tamaa kabisa kurudi pale juu.

Ukianzia juu lazima urudi chini kwanza ili uje utengeneze huku ambako hakuna uimara. Wengi waliopata pesa za haraka halafu wakakimbilia kufanya vitu vya anasa na vyenye kuonesha wao wana pes asana wamekuja kuishia hawana chochote. Wengi wamekuja kuanza tena sifuri na aibu kubwa ikiwa ndani yao kwasababu kila mtu anawasema hawa watu walikuwaga na hela sana kipindi kile.

Haijalishi unajionaje sasa hivi, wewe kubali kushuka na kunyenyekea. Acha bidii na juhudi zikuinue na sio wewe mwenyewe ujinyanyue.

Hatari nyingine ya kuanzia juu ni kwamba sio rahisi sana kurudi tena juu unapoanguka. Yaani unaweza kukosa kabisa hamasa kwasababu ya lile anguko lako kutoka juu kuja chini. Ila unapoanza chini halafu ikatokea umefika mahali ukayumba ni rahisi sana kurudi tena kwasababu kwanza unaielewa njia vizuri.

Naomba ukumbuke kwamba hakuna mashetani kwenye pesa za mashamba ya urithi wala kwenye fedha za madini. Inawezekana ulishawa fikiri labda wale waliopata pesa nyingi za ghafla kwa kupitia vitu hivi labda walilogwa au pesa hizi zina mashetani. Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho wengi wao wamekimbilia kuanzia juu ndio maana wakaanguka.

Kuwa na ndoto kubwa lakini kubali kuanza kidogo, hakuna haja ya kutaka kila mtu ajue kuwa una pesa wakati pesa zenyewe huwezi kuzigawa kwao. Haina maana kabisa, wewe endelea kupambana tu taratibu kuna vyombo maalumu hutaja matajiri wa dunia ukifkia huko vitakutaja tu usiogope.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading