Habari ya siku rafiki, pole kwa changamoto ya Ugonjwa huu wa COVID-19. Nakutia Moyo usiogope tunakwenda kuvuka pamoja.

Kila kitu hutengenezwa kuanzia kwenye akili zetu. Furaha, huzuni, matatizo, na kila aina ya vitu ambavyo hutusumbua na kutufurahisha huanzia ndani yetu.

Vile unavyofikiri mara nyingi ndio huwa tatizo kuliko hata tatizo lenyewe, moyo wako ukijaa wasiwasi, hofu na mashaka juu ya jambo fulani asilimia kubwa ya vile unavyoona huwa imejaa zaidi kwenye hofu.

Hii husababishwa na uwezo wa akili yetu kuumba vitu (imagination) mfano umeingia kwenye simu ya mpenzi wako ukakutana na sms ambayo haiweleweki. Moja kwa moja utaanza kujenga mawazo kwamba huyu mtu ananisaliti, akili yako itaanza kukupa matukio mbalimbali ya nyuma ili kuthibitisha kile ulichokiona kwenye sms.

Mwisho wa siku kumbe ni mawazo yako tu hakuna ukweli wowote. Nataka nikwambie kitu kimoja jifunze kuyaongoza mawazo yako, jifunze kuzitawala hisia zako. Hisia zako ukishindwa kuzitawala zitakupeleka kwenye fikra potofu.

Hisia zako ukishindwa kuzitawala utajikuta unawaza mambo ya ajabu ajabu ambayo yatakupelekea kushindwa kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yako.

Hisia za hofu huleta fikra za kushindwa ndani yako, usiruhusu ziutawale moyo wako.

Huwezi kuishi bila kuwa na hofu kabisa kwasababu vipo vitu vingi vinakuwa nje ya uwezo wako, kitu pekee unachoweza kufanya ni kuziongoza hisia zako na fikra zako.

Unapokuwa na hofu jitahidi uwe unajinenesha maneno ya kukutia nguvu na ujasiri. Jisemeshe nakwenda kushinda, nakwenda kuvuka hili jaribu, Mimi ni mzima, tayari nimepona, Nimelivuka hili jaribu, ninavuka hizi changamoto.

Maneno kama haya yatakufanya uweze kuzishusha chini hisia za hofu na utaweza kufikia ushindi mkubwa.

Kumbuka tunaambiwa tusiogope kwasababu kuna vitu vinaogopesha, tunatakiwa tuwe majasiri kwasababu kuna mambo mazito tunakwenda kupitia.

Yoshua 1:9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.

Unaweza kununua vitabu Vyangu kwenye link hii https://www.getvalue.co/home/seller_collection/200

Nakutakia Kila La Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading