Habari Rafiki, leo kwenye mbinu za mafanikio tunakwenda kuwaona watu aina nne tulionao katika safari ya mafanikio. Ni kweli watu wengi wamekuwa wanatamani sana kufikia mafanikio. Ni kweli watu wengi wamekuwa wanahamasika sana wakiona wengine wamepiga Hatua Fulani kwenye Maisha. Lakini tunatofautiana sana katika hao wengi kwenye mchakato wa kufikia mafanikio.

Katika watu wengi waliofikia mafanikio makubwa, ukiangalia historia zao unakutana na jambo moja ambalo wamelifanya kwa muda mrefu hadi likawatoa, japokuwa mwanzoni utaona wamejaribu mambo tofauti tofauti kisha wakayaacha lakini lile ambalo waliamua kabisa kudumu nalo/nayo ndio yamewafanikisha. Ili uweze kufikia Hatua ya juu kabisa ya mafanikio katika kile unachokifanya kuna muda mrefu utapita. Muda huo unaweza kuwa ni wa ukimya sana hadi pale utakapoweza kufika sehemu ile ya juu ya mafanikio.

Huwezi ukaanza leo na ukapokea heshima leo. Yeyote unaemuona anapewa heshima kuna muda mwingi amekuwa chini akidharaulika na kuonekana ni mtu wa kawaida. Wengine watakuita wewe ni mganga njaa tu, hueleweki, hujui unachokifanya, lakini endelea mbele. Wapo watakaokudharau sana lakini unapaswa kusonga mbele hadi ufike kwenye Hatua ya juu kabisa.
Sasa katika safari yetu kuna aina nne za watu ambao wapo. Ni vyema ukajifunza nami ili utazame upo kundi gani.

1. Wanaotaka Kuonekana Wamefanikiwa.

Hawa ni aina ya watu ambao siku zote wanapenda kujionyesha. Wakipata mafanikio kidogo wanataka kila mtu ajue. Wakipiga Hatua Fulani wanapiga kelele kuliko lile walilofanya lenyewe. Aina hii ya watu ni wale ambao wanapenda Maisha ya kuigiza na kuwaridhisha watu.
Wengi wao hupenda sana kuongea kuliko kutenda, mara nyingi hupima mafanikio ya watu kwa kutazama nje kuliko ndani.
Usikubali kuwa kama mtu huyu maana huwa hawapigi Hatua hata siku moja, wanaishia kuwa na Maisha ya kawaida kama watu wengine.

2. Wanaoyataka Mafanikio.

Kuna mfano mmoja huwa unatolewa sana kwenye semina au makongamano, pale mzungumzaji anatoa pesa na kuuliza nani anaitaka pesa hii. Mara nyina utaona wote wanasema wanataka lakini hakuna hata mmoja anaechukua Hatua kwenda kuichukua. Na kwenye mafanikio ni hivyo kila mmoja anasema anataka mafanikio, anataka kufanikiwa lakini sio wote wanaotoka kwenye kutaka na kwenda kwenye Hatua ya mchakato wa mafanikio.
Ukiwa kundi hili wewe utakuwa ni mtu wa kuhamasika na kuguswa na mafundisho peke yake lakini hubadiliki. Lazima ukubali kutoka kwenye kutaka uanze Hatua ya kufuata yalipo mafanikio.

3. Wanaojaribu Kufikia Mafanikio.

Wapo watu wamekuwa wao ni wa kujaribu tu. Yaani yeye kila anachokutana nacho anafanya akifikiria labda ndio kinaweza kumtoa yaani kumfanikisha. Unajua kama hujajua wewe ni nani utakuwa yeyote tu. Kama hujajua ni wapi unakwenda njia yeyote itakuchukua.
Mara nyingi watu hawa hupenda kusema, kufanikiwa ni bidii yako mwenyewe tu. Wanadharau vitabu, wanadharau wahamasishaji, wanasahau kwamba huwezi kuoga siku moja ukawa msafi siku zote. Hata gari haliwekwi mafuta ile siku ya kununua basi.
Usikubali kuwa mtu anaejaribu, mtu huyu hafiki popote, mtu huyu hana Imani sawasawa.

4. Waliojitoa 100% Liwalo na Liwe.

Hawa ndio watu ambao mar azote hupiga Hatua kwenye mambo wanayoyafanya. Hawa wana maono makubwa. Wana malengo ya Maisha yao. Wapo tayari kujitoa kwenye kile walichoamua kufanya hadi kilete mafanikio.
Watu hawa ndio huwa hawaogopi changamoto, wapo tayari kujifunza. Wakikataliwa huku wanajaribu kule. Wakikwama hapa wanatafuta suluhisho sehemu nyingine. Huwezi kuwakuta wanalalamika. Wanajua Maisha yao yote ni majukumu yao, wamebeba misalaba yao wenyewe na wako tayari kufika kule wanapopaona.
Wewe Rafiki yangu napenda uwe mtu huyu. Kwasababu huyu pekee ndio anaweza kufika kwenye mafanikio. Yale makundi mengine yote yataishia njiani. Kama wewe mpaka sasa hujajua ni kitu gani hasa utakifanya hadi kikuletee mafanikio kaa chini ujitafakari.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

6 Responses

      1. Asante sana mr Jacob…iko kitabu kinacho kunacho elezea kilimo kinauzwaje…na vip unafundisha ujasilia mali pia?

Leave a Reply to Jacob MushiCancel reply

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading