Habari Rafiki yangu, leo tena nimeandika barua hii maalumu kwa watu wote wasio na wazazi na pia wenye mzazi mmoja. Ni kwa ajili ya kukutia moyo ili uweze kusonga mbele na kutimiza Ndoto yako. Unaweza kutuma Makala hii kwa Rafiki yako ambaye unafikiri akiisoma itamtia moyo na ataweza kusonga mbele.

Kwa waliopoteza wazazi kwasababu mbalimbali, waliotelekezwa na waliozaliwa nje ya ndoa lakini muda wanautumia wakiwa na mzazi mmoja. Kwanza nikupe pole sana kwa kuwepo kwenye hali ya aina hiyo, pia naomba utambue kwamba haupo peke yako na wala wewe sio wa kwanza.

Inawezekana wewe unaishi bila ya baba au mama kwasababu mbalimbali mojawapo ya sababu kubwa ambayo imekuwa ipo kwa wengi ni kutelekezwa na mzazi mmojawapo. Aina ya wazazi ambao mara nyingi huonekana ndio wanatelekeza watoto wao ni wanaume. Hivyo ina maana idadi kubwa ya watoto wanaolelewa au waliolelewa bila ya baba ni wengi Zaidi.

Nina amini kama umeweza kuisoma barua hii basi wewe tayari upo kwenye rika la utu uzima nikiwa na maana una uwezo wa kujitegemea kwa kiasi kikubwa hata kama bado upo kwa mzazi wako. Kujitegemea sio kuishi kwako peke yake nina maana ule uwezo wa kutafuta kipato na kuweza kuilisha familia yako au mzazi ambaye unaishi nae.

Yapo mambo machache nataka ujifunze ili uweze kuishi Maisha yenye furaha na wala hali hiyo isiwe inakuumiza.

Wewe Sio Mlemavu

Kuishi na mzazi mmoja sio ulemavu, usijione umepungukiwa kitu sana kuliko wale ambao wanaishi na wazazi wao wote. Ndio kuna umuhimu sana wa kulelewa na wazazi wote lakini ukishajikuta upo kwenye hali hiyo hupaswi kuendelea kubaki hapo na kuwaza sana.

Elewa kwamba huo ndio ukweli, na bahati mbaya sana huwezi kuubadilisha. Endelea mbele na Maisha yako. Jione kama mtu aliekamilika. Ishi kwa furaha kama wengine.

Furahia kile ulichonacho maana ndio hicho ulichobarikiwa. Kama una mzazi mmoja ishi nae kwa furaha kabisa kama mwenye wazazi wawili. Kumbuka kuna ambaye hana wazazi wala ndugu yeyote kabisa.

Kama huna wazazi wote pia kuhuzunika na kukata tamaa hakubadilishi huo ukweli. Elewa kwamba huo ndio ukweli kwamba huna wazazi wote halafu endelea na Maisha yako kwa furaha kama watu wengine. Furahia hata uzima ambao umebakia nao maana wapo wenye wazazi wote lakini ni walemavu na wengine wamelazwa kitandani, furahia marafiki ambao unao.

Ondoa Chuki na Visasi Moyoni Mwako.

Kuna watu nimekutana nao wanasema wanawachukia wazazi wao kwasababu ya historia za aina mbalimbali. Inawezekana baba alikukataa tangu ukiwa tumboni, inawezekana mama alikutupa baada ya kujifungua. Kumchukia yeyote hakuna kinachobadilika.

Kumchukia mzazi kwa ubaya alioufanya ni kujihamishia ile chuki aliyokuwa nayo yeye na kuiweka moyoni mwako. Tulipokuwa wadogo tuliwahi kuambiwa kwamba ukimuua mtu unazibeba na dhambi zake zote, hivyo mtu kuogopa kubeba dhambi za mtu mwingine anakuwa anaogopa kuua. Sasa nataka na wewe ujue kwamba ukimchukia mtu kwa mabaya aliyokufanyia unakuwa huna tofauti na yeye.

Wasamehe wazazi wako kwa yote ambayo yametokea. Iache iwe historia tu, wewe songa mbele Timiza Ndoto zako na maono yako makubwa ipo siku utawaelezea watu na ushuhuda wako utawainua wengi sana.

Acha Kulaumu

Ishi Maisha yako kama mtu ambaye aliekamilika kabisa. Kama huna mtu yeyote unaemtegemea basi hiyo sio sababu ya kukurudisha nyuma unatakiwa upate nguvu kwamba haya Maisha natakiwa niyabebe mwenyewe.

Acha kuwalaumu wazazi wako,

Acha kuwalaumu ndugu zako wenye fedha lakini hawakusadii chochote.

Acha kuilaumu dunia kwa lolote baya ambalo limekupata.

Lawama za aina yeyote hazisaidii wala kubadili chochote kwenye Maisha yako. Unatakiwa uanze kuchukua Hatua. Anza kutengeneza upya Maisha yako. Maisha yako yapo mikononi mwako mwenyewe.

Usiseme kwanini mimi angalia ni sababu ipi nzuri ambayo imesababisha wewe uwe kwenye hali hiyo. Ninaamini unaweza kuwa mfano mzuri kwenye dunia hii kwamba ulizaliwa bila ya wazazi lakini umeweza kufanya mambo makubwa.

Soma: BARUA MAALUMU KWA VIJANA AMBAO HAWAJAOA AU KUOLEWA

Usirudie Makosa Yaliyotokea Kwako.

Unachopaswa kujifunza ni kwamba usirudie makossa yaliyofanywa na baba yako au mama yako. Kama ulizaliwa nje ya ndoa usikubali kuwa na mtoto ambaye utamzaa bila ya mama yake au baba yake. Kama wazazi wako walifariki kwa sababu yeyote ile na wakajikuta wamekuacha kwenye hali ngumu basi na wewe jitahidi sana usikubali kuwaacha watoto wako bila ya msingi mzuri.

Ishi Maisha ya uadilifu, wapo waliotumbukia kwenye tabia mbovu kwasababu tu ya hali hii ya kuzaliwa bila ya wazazi. Wengine wamekuwa makahaba, wengine walevi waliopindukia. Kufanya yote hayo sio suluhisho la matatizo yako. Ni vyema ukajua kwamba yapo mambo mengi mema unaweza kuyafanya na yakakusaidia ukafanikiwa kimaisha. Una nafasi ya KUANDIKA HISTORIA MPYA kama nilivyosema kwenye kitabu cha SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO.

Jiandae sasa hivi kama umeshapata watoto basi waandae waweze kuishi katika namna ambayo hata kama ikatokea umeondoka ghafla wataweza kujisimamia wenyewe. Kama una mke basi hakikisha na yeye unamuandaa ili aweze kusimama hata kama hutakuwepo wewe aweze kuibeba familia bila ya kuona uzito.

Kuna msemo unasema “Ukimpa mtu samaki utakuwa umemsaidia kwa siku moja, lakini ukimfundisha kuvua samaki basi umemsaidia Maisha yake yote” hivyo basi kama utaweza kuwatengeneza katika namna ya wao kuweza kuvua samaki wao binafsi utakuwa una uhakika kabisa siku unaondoka duniani umeacha watu wanaoweza kusimama wenyewe.

Una Nafasi ya Kufanya Makubwa Sana.

Mmiliki wa mtandao wa amazon bwana Jeff Bezos ni mmoja wapo wa watu ambao wameishi Maisha kama yako japo ni tofauti kidogo. Mama yake mzazi alipewa mimba akiwa shuleni na baadae akaolewa na aliempa mimba (baba yake Jeff) lakini kutokana na ugumu wa Maisha na ulevi wa baba yake Jeff ikabidi waachane na mama yake Jeff akaolewa na mwanaume mwingine. Pamoja na changamoto zote hizo leo Jeff Bezos ni Tajiri namba moja duniani (2018).

Inawezekana na wewe umepitia hali kama hii na ukajikuta unajiona wewe huwezi chochote. Umekosa mtu wa kukulipia ada, umekosa mtu wa kukupa mtaji au wa kukusaidia kwa namna yeyote ile. Naomba ukumbuke kwanza uwezo uliopo ndani yako ni mkubwa sana. Usikubali hali ya Maisha ikufanye ushindwe kusonga mbele.

Wako wengi wenye historia kama yako na wameweza kufanya mambo makubwa sana kwenye dunia hii. Unachotakiwa ni wewe kuacha kuifanya hali hiyo ya kukosa wazazi kuwa sababu ya umaskini ulionao au kushindwa kwako kuchukua Hatua.

Kwanza jua kusudi lako hapa duniani, unaweza kukuta kusudi lako linahusiana kabisa na jinsi ulivyozaliwa. Tengeneza maono makubwa, kuwa na malengo. Ishi kusudi lako kila siku. Usikubali mtu yeyote akuambie huwezi na wala wewe mwenyewe usije kujiambia kwamba huwezi.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog

Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp… https://jacobmushi.com/whatsapp/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading