Category Archives: HATUA ZA MAFANIKIO

535: Yanapokuja Usiyoyatarajia…

Weka Email Yako Hapa Upokee Makala Kama Hizi

Kwenye maisha yetu ya kila siku kuna mambo mengi hutokea na kwa namna moja au nyingine mambo haya yanatuathiri moja kwa moja au kwa sehemu. Kila siku kuna mtu atakuwa amezidiwa na akakimbizwa hospitali, kuna ambaye atafiwa, kuna ambaye atapata ajali, kuna ambaye ataibiwa, kuna ambaye atapoteza pesa, kuna ambaye atafanya uzembe Fulani, na mengine mengi sana.

Haya ni mambo yanayotokea katika maisha yetu ya kila siku. Kwa bahati mbaya sana haya mambo mengi hatuna uwezo wa kuyathibiti. Huwezi kuzuia mtu mwingine asiwe mgonjwa asiibiwe, asipate ajali, na hivyo basi yanapotokea yanakuwa ni mambo ambayo tusiyoyatarajia.

Leo natamani kuona wewe unakuwa mtu mwenye furaha na maisha yako yanakuwa bora lakini bado haya mambo yatakuwa yanaingilia furaha yako ya kila siku, mipango yako binafsi,  na hata yale mambo ya muhimu.

Inawezekana wewe ni dereva mzuri sana, hujawahi kupata ajali, hujawahi kuandikiwa kosa lolote hata la bahati mbaya na askari wa usalama barabarani. Siku moja asubuhi unaamka ukiwa na mipango yako mizuri sana, unaingia barabarani halafu unajikuta upo kwenye foleni ambayo itakuchelewesha labda kwa masaa kadhaa. Foleni ile imesababishwa na dereva moja mzembe ambaye amepata ajali. Akaathiri ratiba zako zote za siku nzima. Ubora wako kwenye udereva hapo hautakusaidia chochote.

Unachotakiwa kwenye maisha yako ya kila siku, ni kujiandaa kwa yale ambayo hayatarajiki. Hakuna anaemka asubuhi na kutarajia kwenda kupata ajali, au kuibiwa, au hata kuumwa. Kila mmoja anatarajiwa mambo mazuri. Lakini mambo mabaya hayaachikuja. Yanakuja kwasababu ndio asili ya dunia. Kila saa kuna mambo mengi yanaendelea na yanaweza kukuathiri wewe moja kwa moja au kwa sehemu.

Unachopaswa kuelewa ni kutarajia yasiyotarajiwa. Unapanga mambo yako lakini unaweka akili kwamba lolote pia linaweza kutokea likasababisha hii mipango yako ikakwama. Wakati mwingine sio lazima ujiandae na mabaya, lakini unapaswa tu kuelewa yanaweza kutokea popote na yakakukuta bila kujalisha wewe ni mwadilifu kiasi gani. Ukiwa na hili kichwani mwako hata itokee nini huwezi kuumizwa sawasawa na Yule ambaye akili yake aliiweka kwenye upande mmoja pekee. Kama vile anaishi peke yake hapa duniani.

UNAPOTARAJIA MAMBO MAZURI MAKUBWA KWENYE MAISHA YAKO USIACHE PIA KUTARAJIA NA YASIYOTARAJIWA.

Ni mimi rafiki Yako wa Siku Zote Jacob Mushi.

511; Unakimbilia Wapi? Tazama Pembeni Yako.

 Haya Ndio Maisha yetu kwenye vitu vingi tunavyopitia kila siku, Soma kisa hiki ujifunze: “Habari kaka Jacob, ninaomba ushauri wako kuhusu hili. Ni mwaka wa tatu sasa tangu nikutane na binti mmoja na nikampenda sana. Nina tabia moja huwa sikati tamaa haswa pale ninapokuwa nimekipenda kitu Fulani maishani mwangu. Nimekuwa naamini kwamba ipo siku tu kitakuwa cha kwangu.

Binti huyu kila nilipokuwa namfuatilia ili niweze kuwa nae amekuwa akinisumbua sana, kila wakati ananipiga chenga za namna mbalimbali. Nimejitahidi kumpatia kila anachokitaka, lakini alikuwa anasema anatamani tuwe marafiki tu kwani tukiingia kwenye mahusiano tutakuwa tunagombana na mwisho wake tutaachana.

Kwasababu nilimpenda kwa dhati ikanibidi nimsikilize tu. Sasa huu ni mwaka wa tatu tumekuwa karibu kama marafiki na nilijiapiza sitaingia kwenye mahusiano mengine kwakuwa niliona kama ananipima uaminifu wangu.

Wiki mbili zilizopita kanijia huku akilia machozi na kuniomba msamaha anasema ananipenda sana na yupo tayari kuwa na mimi kuanzia sasa. Anadai amegundua alikuwa anapoteza muda na watu ambao hwakuwa wanampenda bali kumtumia tu.

Hilo halikuwa shida, kubwa Zaidi ananiambia kwamba mwanaume aliekuwa nae kwenye mahusiano kwa Zaidi ya miaka 3 akijua anampenda, amempa ujauzito na kumkimbia. Huku akidai hawezi kuwa nae kwenye Maisha yake.

Naomba ushauri wako, nifanyeje, ukweli huyu binti nampenda sana, changamoto ni huu ujauzito alioniletea, sielewei kama ananipenda kweli au ni kwasababu ya matatizo aliyopitia tu. “

Kijana huyu amekumbwa na mkasa huu mzito sana kwenye Maisha yake. Ni kweli inaumiza sana, nataka na wewe ujifunze kitu kwenye huu mkasa, je ni vitu gani umekuwa ukivikimbilia ukijua ni vyako mpaka pale ulipopoteza?

Huyu binti amekua akishikamana na watu ambao hawakumpenda na akasahau kabisa kuona mtu aliekuwa karibu yake wakati wote. Inawezekana hata wewe kuna vitu umekuwa unavishikilia ukidhani ni vyako na ukasahau vile ambavyo ni vyako siku zote vipo karibu na wewe siku zote.

Embu jaribu kutazama ni nani huwa yupo karibu yako kila mara? Ukiwa na shida, ukiwa na raha yupo. Wakati wowote ukimhitaji anakuwa yupo tayari kwa ajili yako. Naomba nikwambie watu hawa ni wa thamani sana kwenye Maisha yetu. Usikubali kuwa mtu ambaye unaiona thamani yao wakati wa matatizo tu.

Kuna watu wanaweza kukwambia wanakupenda kwa maneno matamu lakini kuna watu wanakupenda kwa kufanya vitendo kwenye Maisha yako. Kuna watu ambao hujawahi kusikia wakisema NAKUPENDA lakini wamekuwa wakifanya mambo makubwa kwenye Maisha yako kuliko neno hilo na NAKUPENDA.

Jifunze kutofautisha watu wanaouhitaji mwili wako na wanaouhitaji moyo wako, jifunze kutofautisha watu wanaozihitaji pesa zako na wanaokuhitaji wewe kwenye Maisha yao. Wapo wengi wanaonekana kama wanatuhitaji sisi kumbe wanahitaji vile vitu tulivyonavyo. Ukishindwa kujua haya utaishia kutumbukia kwenye shimo kila mara.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

417; Ukianzia Juu Utashuka Chini.

Mojawapo ya vitu ambavyo huanza juu havipendezi sana na sio vizuri mfano wa haraka ni shimo. Shimo linachimbwa kwa kuanzia juu kwenda chini na shimo linaweza kuwa hatari lakini vitu vingi vizuri huanzia chini na kuelekea juu. Unapojenga ghorofa lazima uanze chini kuweka msingi ndio upande juu Zaidi.

Sasa Rafiki ukitaka usiteseke, kwasababu wengi wanateseka kwa kuanzia juu wewe anza tu chini kawaida. Hakuna haja ya kuanza kujionesha una Maisha mazuri kwa pesa ambazo umezipata kwa mara ya kwanza. Hakuna haja ya kuonesha mnafurahia mahusiano yenu na wakati mmeanza juzi tu hamna hata mwezi.

Subiri kwanza jenga msingi imara ndipo uwe huru kucheza hata juu ya bati bila woga. Wewe ukitaka kuanguka kimbila juu, kimbilia kuonekana na kila mtu halafu huku chini hakuna msingi wowote uliojenga wa kukuweka imara.

Anza chini kwasababu hata ukianguka hakuna anaekuona, ukikosea hakuna anaejua sana sana wataona wale ambao wanaweza kukushauri vizuri. Ukianzia juu halafu ukakosea utakuta kila mtu akakukosoa na mwisho wa siku utakata tamaa kabisa kurudi pale juu.

Ukianzia juu lazima urudi chini kwanza ili uje utengeneze huku ambako hakuna uimara. Wengi waliopata pesa za haraka halafu wakakimbilia kufanya vitu vya anasa na vyenye kuonesha wao wana pes asana wamekuja kuishia hawana chochote. Wengi wamekuja kuanza tena sifuri na aibu kubwa ikiwa ndani yao kwasababu kila mtu anawasema hawa watu walikuwaga na hela sana kipindi kile.

Haijalishi unajionaje sasa hivi, wewe kubali kushuka na kunyenyekea. Acha bidii na juhudi zikuinue na sio wewe mwenyewe ujinyanyue.

Hatari nyingine ya kuanzia juu ni kwamba sio rahisi sana kurudi tena juu unapoanguka. Yaani unaweza kukosa kabisa hamasa kwasababu ya lile anguko lako kutoka juu kuja chini. Ila unapoanza chini halafu ikatokea umefika mahali ukayumba ni rahisi sana kurudi tena kwasababu kwanza unaielewa njia vizuri.

Naomba ukumbuke kwamba hakuna mashetani kwenye pesa za mashamba ya urithi wala kwenye fedha za madini. Inawezekana ulishawa fikiri labda wale waliopata pesa nyingi za ghafla kwa kupitia vitu hivi labda walilogwa au pesa hizi zina mashetani. Ukweli ni kwamba hakuna kitu kama hicho wengi wao wamekimbilia kuanzia juu ndio maana wakaanguka.

Kuwa na ndoto kubwa lakini kubali kuanza kidogo, hakuna haja ya kutaka kila mtu ajue kuwa una pesa wakati pesa zenyewe huwezi kuzigawa kwao. Haina maana kabisa, wewe endelea kupambana tu taratibu kuna vyombo maalumu hutaja matajiri wa dunia ukifkia huko vitakutaja tu usiogope.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/kocha

HATUA YA 396: Usifanye kwa Kwa Ajili Yako.

Penda kuwaweka wengine mbele kwanza ndio utaweza kufurahia kile unachokifanya. Unataka kununua gari, Sema napambana ninunue gari ili niwahamasishe wengine kuwa inawezekana ” Chochote kile unachokifanya hata kama ni wewe unafaidi jaribu kuweka katika namna ambayo wengine wanaguswa pia.

Furaha ya kweli haipo katika vitu tunavyomiliki ila katika watu tunaowasaidia.

Furaha ya kweli ipo katika kuwasadia wengine, na ni kwamba umezaliwa una kila kitu ndani yako kwa ajili ya kuwasaidia wengine. Biashara unayoifanya sio kwa ajili yako ni kwa wengine, inawezekana ni Watoto wako, Wateja, na hata watu ambao huwajui.

Ukitaka kusahaulika haraka hapa duniani ni kuwa mbinafsi, kuangalia Zaidi kile unachokipata kuliko thamani unayotoa kwa ajili ya wengine. Waweke wengine mbele kwanza na chochote unachokifanya kama hakimgusi mtu basi usikifanye.

Niko Njiani natembea nikawa nawaza kwamba kuna mtu kafungua Bookshop anauza vitabu ambavyo viliandikwa karibia miaka 100 iliyopita. Hawa waandishi hawana undugu na huyu muuzaji, lakini kwa kupitia kazi iliyofanyika miaka 100 iliyopita kuna mtu anapata pesa ya kula, ada ya watoto na kadhalika.

Nikawaza na kusema hivi hawa waandishi wangesema “naandika Kitabu cha nini wakati nitakufa na kuviacha,” naandika Kitabu cha nini wakati sina shida yoyote, naweza kula, nina nyumba nzuri sasa vitabu vya kazi gani”. Ila kwasababu walijua hawaandiki ili wapate hela ya kula kwa wakati huo, na hata kama wangepata kulikuwa hakuna shida. Wamefanya kazi yao wameondoka duniani wameacha watu wengi wakiendelea Kufaidika na kazi waliyoifanya.

Embu fikiria unachokifanya sasa hivi ni kwa ajili yako au kwa ajili ya wengine? Endapo ikatokea ukaondoka sasa hivi unachokifanya kitaendelea kuwa baraka kwa wengine?

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

HATUA YA 395: Upo Tayari Kufanya Hata Kama Hujisiikii Kufanya?

Watu waliofanikiwa wanaendelea kufanikiwa kwasababu wapo tayari kufanya hata yale ambayo hawajisikii kufanya. Unajua kuna vitu unatakiwa kuvifanya halafu mwili unakuwa umechoka hivi unasema nitafanya kesho au siku nyingine.

Kuna wakati unakuwa umechoka sana hadi yale mambo ya muhimu unataka kuahirisha, unatakiwa ujue kwamba kitu pekee ambacho hutakaa ukipate tena ni muda. Lazima ukubali kujitoa vya kutosha ili ufanikiwe.

Sisemi kwamba unapaswa kujiumiza hapana ila unatakiwa ulipe zile gharama ambazo zinastahili kile unachokitaka. Wewe umeenda Dukani una elfu kumi halafu unataka kununua kitu cha elfu ishirini kamwe huwezi kupata hata ukilia. Njia pekee ya kupata ni wewe kuongeza pesa, hivyo hivyo na mafanikio sio kama bahati kwamba utafika tu hata usipo weka juhudi.

Lazima ujue ni yapi unapaswa kufanya ili kupata kile unachokitaka. Kuna nyakati itabidi hata usielewane na wale unaowapenda kwasababu na wao wanaweza kuwa sababu ya wewe kukosa kile unachokitaka. Kuna wakati itabidi was ahau kidogo zile simu ambazo umekuwa unawapigia mara kwa mara kwasababu umeweka lengo na unataka litimie.

Usipokuwa tayari kulipa gharama, sahau kuhusu mafanikio. Mafanikio sio lelema, sio bahati ambayo kama ipo utakutana nayo Njiani. Mafanikio ni kujitoa, kufanya vitu vya tofauti na wengine. Kufanya vitu ambavyo wengi wanaogopa kufanya.

Ukiamua na ukawa tayari kufanya hata yale ambayo unajisikia uvivu na kuchoka basi utaweza kufika sehemu ambazo wewe hujawahi kufika. Ukiamua kuzungumza na watu ambao ulikuwa unaogopa na ukawasumbua utajikuta unapata kile ambacho unakitaka. Hakuna kitu chenye thamani kinachopatikana kwa urahisi.

Kama dhahabu ingelikuwa inaweza kuchimbwa na kila mtu wala isingeuzwa ghali, embu tazama wale ambao unazama chini kabisa kuifata dhahabu, wengine hupoteza Maisha humo kwasababu dhahabu ina thamani kubwa sana. Kile unachokitaka kama haupo tayari kujitoa vya kutosha huwezi kupata matokeo unayotaka.

 

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

HATUA YA 394: Kama Hutengenezi Maadui….

Ni kweli hutakiwi kufanya kutafuta maadui kwasababu haina maana yeyote, ila katika safari ya mafanikio huwezi kuepuka kuwa na maadui. Kuna watu watakuchukia tu bila sababu yeyote. Wengine watakuchukia kwasababu kile unachokifanya wao hawajaweza kufanya, wengine watakuchukia kwasababu wameona umeanza kuwapita kwasababu mnafanya kitu kinachofanana.

Sasa wakati mwingine ili kujua kama kweli unasonga mbele na unafanya mambo ya tofauti ni pale unapokutana na watu ambao wanakuchukia. Inakupasa uelewe kwamba maadui hawaji kwako sio kwasababu unafanya kitu kibaya bali ni kwasababu unafanya kitu kizuri sana hadi unawakera.

Kuna wakati naanza kuandika walitokea watu wakaanza kuniambia wewe unaandika sana hadi unakera, unapost sana Makala zako. Nikagundua Kumbe nimefanya hadi wameanza kuona.

Unachotakiwa kujua maadui wanapokusema wanakutangaza, watu wanaposema mambo yako wanawaambia watu ambao walikuwa hawakujui kwamba kuna jamaa anafanya jambo Fulani la tofauti. Sasa mojawapo ya kipimo cha ukubwa wako sio watu wengi wanakusifia tu bali hata wale ambao wanakuchukia bila ya sababu.

Unachotakiwa kujua kwamba:

Huwezi kumfurahisha kila mtu.

Unapokuwa tofauti na wengi ndio maadui watakuja wengi.

Maadui wanapokusema wanakutangaza kwa wale ambao hawajasikia Habari zako tena bure.

Endelea mbele, fanya kazi zako kwa ubora na maadui watakuja wenyewe. Hutakiwi kutengeneza maadui hata mara moja wewe unatakiwa kuwa bora tu na wa tofauti katika kile unachokifanya. Usipoteze muda wako kujibizana nao wewe endelea na kazi matokeo ya kile unachokifanya ndio yatatoa majibu.

Nikusihi Rafiki kama huna adui maana yake wewe bado hujawa tishio kwa mtu yeyote hapa duniani. Hivyo basi nenda kafanye jambo la tofauti na la kipekee ambalo litawashtua wale waliokuwa wamelala waanze kuzungumza Habari zako.

Nenda kafanye jambo la tofauti sana na la kipekee uwapatie kazi wengine, hivi unajua kuna watu hawana cha kufanya sasa kama ukianza kufanya kwa ubora unakuwa unawapa cha kufanya. Unawapa kazi ya kukusema, unawapa kazi ya kukufuatilia, unawapa kazi ya kuandika mabaya yako.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

HATUA YA 393: Yeyote Anaejaribu Kukuzuia…

Ukiona kuna mtu ana muda mwingi sana wa kufuatilia unachokifanya na siku zote anakuja na mawazo hasi tu na wala hujamwajiri afanye hivyo basi ujue tu huyu Ameshapoteza Muelekeo wa Maisha Yake Mwenyewe.

Huo ndio ukweli kama yeye Maisha yake hana muda nayo ndio anapata muda wa kufuatilia Maisha yako maana yake yeye ameshayapoteza Maisha yake. Usitegemee ushauri wake utafaa kwa chochote kwasababu angekuwa mtu anaejielewa huo muda wa kukufuatilia kila unachokifanya angeuwekeza kwenye Maisha yake binafsi.

Hivi unajua kwamba mtu aliekutangulia mbele yako sio rahisi sana awe anakuona unavyokuja nyuma yake? Na kama ni hivyo ukiona anatumia muda mwingi kukufuatilia wewe ulieko nyuma yake na kukuzuia basi ujue ameshakuogopa anahisi utakuja kumpita na kumuacha. Sasa cha ajabu ni kwamba kila mtu ana Maisha yake na malengo yake. Mtu akikupita haikupunguzii wewe chochote.

Kamwe usikubali Maneno ya watu wa aina hii yakupotezee kasi na mwelekeo wako katika kuyatimiza malengo yako na maono yako makubwa. Hawa ni watu waliokata tamaa au wanaoogopa yale mambo makubwa ambayo unataka kuyafanya.

Usikatishwe tamaa na mtu aliekata tamaa. Usirudishwe nyuma na mtu alieko nyuma yako. Songambele watazame wale ambao wameshakutangulia usiwatazame wale ambao walishindwa. Muda wako ni thamani sana usije kuutumia kujali walioshindwa wamesema nini juu yako.

Rafiki yangu nataka ukumbuke kwamba yeyote anaepoteza muda wake kukuzuia basi hana mwelekeo wa Maisha yake, ni muoga, anahisi utakuja kumpita Kumbe wewe hata hushindani na mtu mwingine, anajaribu kukuvuta ufanane nae.

Kama yote hayo ni hivyo kwanini ujali? Kwanini uumie eti kisa kuna mtu mmoja anataka kukukwamisha wakati umeshajua huyu ameshayasahau Maisha yake anatumia muda mwingi kuangalia Maisha ya wengine? Bila kujali ni nani kwako usipoteze muda wako kuumia maana utakosa mwelekeo katika mambo yako ya muhimu.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

HATUA YA 392: Una Uwezo wa Kudhibiti.

Imekuwa ni kawaida kusikia watu wanalalamika wameumizwa kihisia, na wanasema hawatakaa wapende tena. Imekuwa ni kawaida pia kuona watu wakilalamikia mambo mbalimbali ambayo walijitoa  sana na kisha yakaja kuwaumiza kuliko walivyotarajia.

Unachotakiwa kujifunza hapa ni wewe binafsi kujitahidi uweze kudhibiti hisia zako. Usipende kuziachia zikatoka au zikaonekana san ahata kwa mtu ambaye bado hujajua kama ana mpango gani na wewe. Ni sawa na kutoa maji kwenye ndoo na kutaka yaingie yote kwenye kikombe lazima utayamwaga. Unapozitoa hisia zako kwa mtu ambaye bado hajafungua moyo wake kwako lazima utaumizwa kwasababu hisia zako zinakuwa zinapotea hewani.

Jifunze kudhibiti hisia zako, hasa kama umeshajijua kuwa wewe ni mwepesi wa kupenda mtu. Usipende kuonesha waziwazi ule udhaifu wako kwa watu ambao hujawajua vizuri kwasababu wengine watautumia kukuumiza.

Hivi umeshawahi kujiuliza kwamba kama kuna mtu ambaye hapendi kupendwa? Mbona sasa unakutana na mtu anasema nilimpenda sana lakini akaniumiza? Ukweli ulimpenda ila yeye hakuona upendo aliona udhaifu wako.

Usitumie muda mwingi sana kuwaza Zaidi kwenye ule udhaifu wako au kuufanyia kazi kwasababu huo ni udhaifu na mara Nyingi huwezi kubadili ila unaweza tu kudhibiti. Tumia muda mwingi Zaidi kwenye vile vitu ambavyo uko vizuri na utajikuta unaweza kushinda kile ambacho kinakufanya uanguke kirahisi.

 

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

HATUA YA 391: Kwanini Uamke Asubuhi na Mapema?

Wakati wa Asubuhi Ndio wakati ambapo watu wengi wenye mafanikio huanza siku zao. Wengi wanaamka mapema ila sio kwasababu ndoto zao zinawasukuma, wengine wanawahi kuamka kwasababu bosi wake ni mkali akichelewa.

Asubuhi akili inakuwa haijachoka hivyo chochote utakachokifanya asubuhi kinakuwa na matokeo bora sana.

Asubuhi hakuna usumbufu, watu wengi wanakuwa wamelala, mifugo, redio zimezimwa, Watoto hawasumbui hivyo unakuwa na utulivu wa kufanya mambo yako vizuri.

Asubuhi ndio muda ambao mwili wako pia unakuwa umechangamka.

Ukiamka mapema unaanza kujiengenezea ushindi mdogo mdogo hivyo siku yako yote inakwenda kuwa ya kishindi na yenye matokeo chanya.

Ukiamka asubuhi na mapema ukaipangilia siku yako unajitengenezea matokeo chanya.

Kama utaamka asubuhi na mapema na ukaanza kujikumbusha yale malengo yako makubwa utakuwa na hamasa kubwa sana ya kufanya kazi siku hiyo na utapata matokeo mazuri Zaidi.

Ukiamka asubuhi ukasoma kitabu unaweza kukielewa vizuri Zaidi kuliko wakati wa mchana kwasababu unakuwa na focus Zaidi.

Nawashauri wote wale mliokuwa hamuwezi kuamka asubuhi na mapema muanze kuamka mapema. Wale mliokuwa mnaamka mapema lakini mnafanya mambo ya kawaida kabisa basi muanze kuyafanya haya niliyoelekeza kwenye Kanuni yetu.

Mafanikio yako yaanza asubuhi, ushindi unaanza asubuhi, kila kitu ni asubuhi na mapema. Usiamke ukaanza kutembelea kwenye mitandao ya kijamii badala yake amka uanze kufanya yale ya muhimu kwako.

Mwanzo utakuwa mgumu lakini endelea kuwa mvumilivu na kurudia rudia hadi ikae kwenye utaratibu wako wa kila siku.

 

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

HATUA YA 390: Kumbuka Kitu Hiki Pale Wengine Wanapokukatia Tamaa.

Siku moja nilikutana na kijana mmoja anaitwa Baraka ambaye alikuwa na changamoto ya kukatiwa tamaa yaani kuchokwa na watu wa karibu yake kama wazazi, mpenzi wake na kadhalika. Baraka alinieleza kuwa ilifika mahali akasema sasa afanye nini tena maana kila anachokifanya wale waliomkatia tamaa wanakuwa wanaendelea kumkatisha tamaa.

Ilifika mahali akiwaeleza wazo lolote jipya ambalo ameona litafaa kufanya mfano kama wazo la biashara Rafiki zake na ndugu zake walimcheka na kumwambia; “wewe tumeshakuzoea kila siku unakuja na hadithi zako za kufanikiwa tu lakini hatuoni matokeo yeyote. Embu badilika kwanza ndio utueleze kitu tukuelewe.”

Hali hii ilimkatisha tamaa sana hasa pale alipokuwa anataka kujaribu kitu kwasababu akikumbuka Maneno hayo mabaya anaishiwa nguvu. Akili yake inamwambia atakataliwa tena.

Ilifikia kipindi mahusiano yake na mpenzi wake yakawa mabovu sana. Hii ni kwasababu walikuwa wanagombana kila siku na mpenzi wake. Msichana yule ambaye alikuwa anapenda starehe alikuwa hamuelewi kabisa alipoelezwa kuwa hakuna pesa kwa sasa.

Baraka ananiambia ikafika mahali ilibidi asitishe mahusiano yake na binti yule. Japokuwa alikuwa anampenda sana lakini hakuwa na namna ya kuendelea nae kwasababu alikuwa kama kidonda. Rafiki zake waliokuwa wanamsema vibaya na kupinga kila alichokuwa anawaambia aliamua kuacha kabisa kuwaeleza chochote.

Walibakia ndugu zake wa karibu haswa baba yake ambaye mar azote ndio huenda kumuomba fedha kwa ajili ya mtaji wa biashara aliyokuwa anaifanya. Halafu sijakwambia kwamba Baraka alifeli shule kidato cha nne hivyo yeye pekee ndie aliebakia nyumbani akifanya shughuli za biashara. Baba yake alimwambia nimechoka kukupa pesa kila siku za mtaji halafu sioni maendeleo yeyote. Kila siku unakuja na wazo jipya la biashara lakini hakuna unalofanikisha hata moja.

Baba alifikia kumwambia kuwa amemchoka. Akamwambia atafute njia nyingine au kitu kingine cha kufanya kinachoeleweka. Baraka alisema alifikia mahali akaona kabisa amekata tamaa ya Ndoto yake kubwa ya kuwa Mjasiriamali mwenye mafanikio. Aliona zile hadithi za matajiri walianzia chini sijui waliuza viazi, wengine wanasemaga waliuza genge akaanza kuziona ni za uongo.

Baraka alipofika hapo nikamwambia asiendelee kusema tena. Nikamwambia neno moja kwamba “WENGINE WANAPOKUKATIA TAMAA, KUMBUKA MUNGU BADO HAJAKATA TAMAA NA WEWE NA NDIO MAANA BADO UPO HAI UNAPUMUA NA NI MZIMA”. Wengine wanapokukatia tamaa wewe mwenyewe usikubali kuungana nao na kukata tamaa pia.

Wengine wanaposema wamekuchoka wewe usikubaliane nao kwasababu hawajui kile ambacho umekibeba ndani yako. Wengine wanaposema mawazo yako sio halisi na hayawezekani waambie waendelee kusubiri.

Hakuna aliefanikiwa bila ya kukataliwa, kuna wakati unakataliwa na watu ili uweze kupata watu wengine bora Zaidi. Kuna nyakati Mungu anafanya watu wale ambao wangeweza kukusaidia wasikusaidia ili uweze kuona ukuu wake.

Usikubali kukata tamaa pale wengine wanapokata tamaa juu yako. Kumbuka Mungu hajakata tamaa na wewe. Hilo ndio jambo pekee la kukutia nguvu. Hii ndio hamasa ya kwanza ya wewe kusonga mbele Zaidi.

Kama bado upo hai usikubali kukata tamaa, usikubali kuishia njiani, sababu ya wewe kuwa hai mpaka sasa ni kuwa Mungu ana mpango na wewe. Ushindi mkuu upo mbele yako endelea kujaribu, endelea kujifunza kwenye makossa yako, endelea kutafuta watu ambao watakusaidia Zaidi.

Usisahau Kujiunga na MasterMind Coaching hapa >>>>https://goo.gl/gWbh7K

Nakutakia kila la Kheri

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

www.jacobmushi.com/huduma