Category Archives: USHAURI

512; Mimi Ni Mtenda Dhambi Kuliko Wewe.

Siku Moja nilikuwa nawaza hivi, “Siku Nikifa Nikakuta hakuna Mungu Nitacheka Sana”, Sauti nyingine ndani yako Ikasema, “Hapo Utakapokuwa Unachekea ni Nani Huyo Atakuwa Amekutengenezea” Ndugu Yangu Mungu Yupo, Ukatae Ukubali…………………

Kuna ule mtazamo wa kuwaona watu ambao wamefanya mambo makubwa, na wale wenye ushawishi mkubwa sana kuwa hao ni watu wasio na makossa kabisa. Na hiyo hupelekea pale wanapokosea kitu cha kawaida kabisa mfano ndoa kuvunjika, tunawaona kama vile ni wamefanya makossa makubwa sana.

Wakati huo huo kuna watu wengi sana kila mara ndoa zao zimekuwa na matatizo makubwa na wanaishia kuachana bila hata kujulikana.

Rafiki napenda ufahamu kwamba kila mmoja ana jambo ambalo huwa ni udhaifu wake. Kila mmoja kuna kitu ambacho kimekuwa kinamshinda mara kwa mara hata wewe ukijitafakari utaona kunai le dhambi ambayo kila mara hukuangusha. Hata kama hakuna anaeijua basi wewe mwenyewe na Mungu wako ndio mnaijua vizuri.

Kama kwako kuna kitu kama hicho basi ina maana kwamba kila mtu kuna jambo ambalo limekuwa likimsumbua pia. Kila mmoja kuna ka udhaifu Fulani huwa kinamwangusha. Ndio maana katika wanafunzi 12 wa Yesu bado kulikuwa na mmoja Yuda Iskariote aliemsaliti Yesu kwa tamaa ya fedha. Bado pia kuna Petro ambaye alimkana Yesu mara tatu, kuna mwingine huyu anaitwa Thomaso alishindwa kabisa kuamini kama Yesu amefufuka mpaka amshike kwa mikono yake.

Sasa kama Yesu mwenyewe alijua amechagua watu 12 wazuri na bado wakaonekana wenye madhaifu mimi ni nani niseme sina dhambi hata kidogo? Ndio maana nataka kukwambia mimi ni mtenda dhambi kuliko wewe, Neema ya Mungu tu ndio hunisaidia, napenda ulijue hili ili usije kunihukumu siku moja ukisikia makosa niliyoyatenda. Vilevile hata wewe kuna kitu najua ni udhaifu wako, unakusumbua mara kwa mara, umekuwa unajaribu kuacha lakini unakwama.

Nataka uwe na mtazamo chanya kwenye mambo ya wengine uweze kuchukuliana na kila mtu kwasababu kila mmoja ana jambo ambalo linamsumbua sana ndani yake hata kama hatakwambia. Na haya mambo ndio mara zote huwaga ni siri za ndani ya watu.

Unaweza kuwa unasema sasa Jacob unataka kusema kila mmoja awe huru kufanya dhambi ile ambayo inamshinda? Hapana hapo utakuwa umenielewa vibaya, maana yangu hapa ni kuwa wewe utambue mtu akiwa hai na akakosea kwa chochote kile bado ana nafasi ya kutubu mbele za Mungu wake.

Inawezekana Mtu ametenda uovu ukasambaa sana akatubu kwa Mungu akapata msamaha na wewe ukaendelea kumhukumu, kumsema vibaya, kumuandika vibaya, ikatokea umekufa ukaenda kuhukumiwa kwa kutenda dhambi ya kuhukumu wengine. Maana yangu hapa kama wewe huna nafasi ya kwenda kumshauri au kumsaidia mtu aliekosea usipoteze muda wako kumsema na kumzungumzia kwasababu huenda unasema yule ni mtenda dhambi sana, kumbe alishatubu siku nyingi na kusamehewa.

Hakuna haja ya kuzungumza mabaya ya mtu kama huwezi kuzungumza mazuri yake. Hakuna haja ya kumchukia mtu alietenda maovu bali twapaswa kumuombea Mungu amsaidie. Na wewe binafsi ukishaujua udhaifu wako basi ni jukumu lako, kuhakikisha unakaa mbali na vile vitu ambavyo vinakupelekea kuitenda dhambi. Ukishatambua kile ambacho kinakuangusha kirahisi ni jukumu lako kutafuta msaada kwa watu wenye uwezo kwenye tatizo lako wakusaidie uweze kujidhibiti.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

511; Unakimbilia Wapi? Tazama Pembeni Yako.

 Haya Ndio Maisha yetu kwenye vitu vingi tunavyopitia kila siku, Soma kisa hiki ujifunze: “Habari kaka Jacob, ninaomba ushauri wako kuhusu hili. Ni mwaka wa tatu sasa tangu nikutane na binti mmoja na nikampenda sana. Nina tabia moja huwa sikati tamaa haswa pale ninapokuwa nimekipenda kitu Fulani maishani mwangu. Nimekuwa naamini kwamba ipo siku tu kitakuwa cha kwangu.

Binti huyu kila nilipokuwa namfuatilia ili niweze kuwa nae amekuwa akinisumbua sana, kila wakati ananipiga chenga za namna mbalimbali. Nimejitahidi kumpatia kila anachokitaka, lakini alikuwa anasema anatamani tuwe marafiki tu kwani tukiingia kwenye mahusiano tutakuwa tunagombana na mwisho wake tutaachana.

Kwasababu nilimpenda kwa dhati ikanibidi nimsikilize tu. Sasa huu ni mwaka wa tatu tumekuwa karibu kama marafiki na nilijiapiza sitaingia kwenye mahusiano mengine kwakuwa niliona kama ananipima uaminifu wangu.

Wiki mbili zilizopita kanijia huku akilia machozi na kuniomba msamaha anasema ananipenda sana na yupo tayari kuwa na mimi kuanzia sasa. Anadai amegundua alikuwa anapoteza muda na watu ambao hwakuwa wanampenda bali kumtumia tu.

Hilo halikuwa shida, kubwa Zaidi ananiambia kwamba mwanaume aliekuwa nae kwenye mahusiano kwa Zaidi ya miaka 3 akijua anampenda, amempa ujauzito na kumkimbia. Huku akidai hawezi kuwa nae kwenye Maisha yake.

Naomba ushauri wako, nifanyeje, ukweli huyu binti nampenda sana, changamoto ni huu ujauzito alioniletea, sielewei kama ananipenda kweli au ni kwasababu ya matatizo aliyopitia tu. “

Kijana huyu amekumbwa na mkasa huu mzito sana kwenye Maisha yake. Ni kweli inaumiza sana, nataka na wewe ujifunze kitu kwenye huu mkasa, je ni vitu gani umekuwa ukivikimbilia ukijua ni vyako mpaka pale ulipopoteza?

Huyu binti amekua akishikamana na watu ambao hawakumpenda na akasahau kabisa kuona mtu aliekuwa karibu yake wakati wote. Inawezekana hata wewe kuna vitu umekuwa unavishikilia ukidhani ni vyako na ukasahau vile ambavyo ni vyako siku zote vipo karibu na wewe siku zote.

Embu jaribu kutazama ni nani huwa yupo karibu yako kila mara? Ukiwa na shida, ukiwa na raha yupo. Wakati wowote ukimhitaji anakuwa yupo tayari kwa ajili yako. Naomba nikwambie watu hawa ni wa thamani sana kwenye Maisha yetu. Usikubali kuwa mtu ambaye unaiona thamani yao wakati wa matatizo tu.

Kuna watu wanaweza kukwambia wanakupenda kwa maneno matamu lakini kuna watu wanakupenda kwa kufanya vitendo kwenye Maisha yako. Kuna watu ambao hujawahi kusikia wakisema NAKUPENDA lakini wamekuwa wakifanya mambo makubwa kwenye Maisha yako kuliko neno hilo na NAKUPENDA.

Jifunze kutofautisha watu wanaouhitaji mwili wako na wanaouhitaji moyo wako, jifunze kutofautisha watu wanaozihitaji pesa zako na wanaokuhitaji wewe kwenye Maisha yao. Wapo wengi wanaonekana kama wanatuhitaji sisi kumbe wanahitaji vile vitu tulivyonavyo. Ukishindwa kujua haya utaishia kutumbukia kwenye shimo kila mara.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

510; Ninajihisi Kama Mtu Aliekwama Kwenye Tope.

“Kaka Jacob naomba ushauri wako, sijui hata nifanyeje, huu ni mwaka wa 5 sasa nimekuwa najaribu kuingia kwenye mahusiano tofauti tofauti lakini naambulia kuachwa na kuumizwa. Mara ya mwisho nilikutana na mkaka mmoja ambaye tulianza nae mahusiano kwa haraka na motomoto sana lakini mwisho wake nikaja kuona anaanza kupunguza mapenzi taratibu, kaanza kupunguza mawasiliano na mpaka akafikia kupotea kabisa.

Yaani niseme kwamba yaani imekuwa tabia ni hiyo tu. Wanakuja kwa kasi na baada ya muda wanaondoka kama vile hatukuwahi kujuana kabisa. Sasa mpaka nakutumia ujumbe huu nimejaribu kutafakari sana sijapata majibu. Nimejaribu kuangalia labda ni mimi mwenyewe nina matatizo, labda kuna mahali nakosea, bado sijapata majibu.

Najihisi kama mtu aliekwama kwenye tope zito na kila ninaempa mkono anivute anaishia kuniacha kwenye tope hilo. Embu nishauri kaka nifanye nini? Muda unakwenda na sijawahi kudumu kwenye mahusiano Zaidi ya miezi mitatu, wengi wanaishia mwezi mmoja mpaka wa tatu.

Nifanyeje?”

Nataka nizungumze na mtu ambaye anajihisi amekwama kwenye tope la namna mbalimbali. Inawezekana na wewe unapitia hali ambayo unajihisi umekwama kwenye tope zito na unahitaji mtu wa kuja kukutoa humo.

Mara nyingi hali mbalimbali tunazopitia kwenye Maisha yetu huwa hazihitaji watu wengine kuja kututatulia bali sisi wenyewe unakuta tunahitaji kupata utulivu mkubwa wa akili ili tuweze kuona ni wapi tunakosea tuchukue hatua. Wakati mwingine ukiwa kwenye tope na mtu akaja kwenye Maisha yako akagundua kweli upo kwenye tope ni rahisi kukukimbia kwasababu anajua akijaribu tu kukusaidia na yeye atajikuta kanasa hapo uliponasa wewe.

Wakati mwingine sio kila anaekukimbia inamaanisha wewe ndio una matatizo hapana wengi hukimbia kwasababu ya woga walionao, wanahisi watanasa kwenye mtego uliokunasa.

Vitu vya Kuzingatia:

Punguza Kasi,

Ukiwa mtu mwenye kasi kubwa sana hasa mahusiano yanapokuwa mapya ni rahisi kuchokana mapema kabla hujafika popote. Lazima ujifunze kwenda taratibu na kama mtu sio sahihi utaona tu atakukimbia kwasababu yule asie na lengo la kudumu na wewe akiona wamcheleweshea anachokitaka ataamua kuondoka. Usiruhusu mtu ayajue madhaifu yako mapema wakati hamjajenga msingi mzuri ambao unaruhusu kuwekana wazi kwa baadhi ya mambo ambayo ni siri.

Soma: Acha Kutafuta Samaki Msituni

Tumia akili yako Zaidi Kuliko Hisia,

Fanya maamuzi kwa kutumia Akili, Usiruhusu Hisia Zikuongoze.

Ukitulia Ndio Utaweza Kujua Kile Unachokitaka.

Wakati mwingine Subira Hutujulisha kama ni kweli tunavihitaji vitu Fulani au vinaweza tu kupita. Ukipanda mbegu mbichi ya mahindi ni rahisi sana kuoza kuliko kuota, kwenye Maisha yetu kuna vitu vinatakiwa vipewe Subira ili viweze kukomaa ili vifae kutumia kwenye hatua nyingine. Mara kwenye mapenzi tunawahi sana kufanya vitu ambavyo vilitakiwa vipewe muda ili vikomae kwanza. Kwasababu kama havijakomaa urahisi wa kuharibika unakuwa mkubwa.

UVUMILIVU;

Uvumilivu wahitajika sana sio kuvumilia mateso hapana nazungumzia kuvumilia hasa ule wakati unakihitaji kitu na hakipo au hakipatikani kwa wakati huo. Kuweza kudhibiti hisia zako na kusema sitaingia kwenye mahusiano kwa wakati huu ambapo nipo kwenye hisia kali za kuhitaji mtu ni jambo la muhimu sana kwasababu hisia kali zaweza kukusababishia uanzishe mahusiano na mtu asiye sahihi au ambaye hatadumu tena baada ya hisia zako kuisha.

MAOMBI;

Kumuomba Mungu ni muhimu sana kwasababu yeye atakupatia muongozo na pia atakukwepesha na wale ambao hawakutakiwa kuja kwenye Maisha yako. Mungu atakuepusha na vile vitu ambavyo havikutakiwa kutokea kwenye Maisha yako.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

506; Nilimwona Akiingia Gesti Jana Jioni

Ni mara ngapi umewahi kuambiwa kuhusu wengine, mfano; “Nilimwona Fulani akiingia Gesti Jana”, “Fulani ana Mwanamke Mpya” na mengine mengi. Ukweli ni kwamba huenda umeyasikia sana kutoka kwa watu au hata wewe ulishawahi kumwambia mtu.

Sasa nikwambie kitu kimoja, hayo ni maoni tu ya watu ambayo hayana ukweli halisia. Ngoja nikupe kisa hiki, Miaka michache iliyopita nilikuwa na Rafiki yangu mmoja wa kike ambaye alikuwa anasoma chuo cha SAUT MWANZA. Sasa binti huyu alikuwa anapendwa sana na baba yake na hivyo mara kwa mara baba akipita Mwanza kwa ajili ya kazi zake lazima wakutane wale na waongee. Mara zote baba akija hushukia Lodge iliyopo karibu na chuo kwa binti ili iwe rahisi kukutana na kula pamoja.

Sasa huyu Binti ilitokea mahusiano yake yalivunjika kwasababu tu kuna mtu alimuona akishuka kwenye bodaboda halafu akaingia lodge alipo baba yake. kwa sentensi moja tu, “Nilimwona Akiingia Gesti Jana Jioni” kila kitu kikaharibika.

Sasa kikawaida ukiwa chuo unaweza kujulikana na watu wengi lakini wewe ukawa na marafiki wachache, na hawa wachache ndio watajua mambo yako. Hawa ndio utawaambia ukiwa umetoka kwenda kukutana na baba yako, au hata kwenye mambo mengine. Sasa endapo tu wale ambao wanakufahamu lakini hawakujui vizuri wanaweza kukuona ukiwa unaingia lodge, kwa haraka haraka kitakachokuja kwenye akili zao ni kwamba umeenda kukutana na mwanaume wako au umeenda kufanya umalaya.

Sasa hawa wakija kukutana na marafiki zao wanaweza kueneza maneno hayo kwamba wewe unamsaliti mpenzi wako mara kwa mara kwasababu wanakuonaga ukiingia lodge. Lakini huo sio ukweli wewe huwa unaingia lodge kuonana na baba yako mzazi. Na sio kwamba hata mnaonania chumbani ni kwenye restaurant tu ya palepale lodge. Lakini wale wasiokujua vizuri walikuona kwa getini na tayari wakaanza kutoa hukumu zao.

Kwa kupitia maneno tu ya mtu aliekuona ukiwa getini unaingia lodge yanaweza kuvuja mahusiano yako. Mfano siku hiyo uliondoka bila kumuaga mpenzi wako kwasababu labda ilitokea tu dharura baba amekuja ghafla na anaondoka jioni hiyo hiyo. Mpenzi wako akaja kusikia umeonekana unaingia lodge mida ya jioni, hata ukijaribu kumueleza hatokaa akuelewe na mnaweza kuvunja mahusiano.

Nataka niongee na Watu Wawili Hapa:

Wewe unaependa kuzungumza Maisha ya watu kwa vitu ambavyo huna uthibitisho navyo, nataka nikwambie tafuta mambo ya muhimu ya kufanya kwenye Maisha yako. Achana na Maisha ya watu, kwa maneno yako tu machache unaweza kuvunja mahusiano ya watu. Kwa maneno yako yasiyo na uthibitisho wa kutosha unaweza kuwavurugia Maisha wenzako.

Achana na Maisha ya wengine fanyia kazi Maisha yako, wewe mwenyewe una matatizo kibao yanakusonga achana na ya wengine kwasababu haulipwi chochote hapo.

Wewe ambayo unapokea maneno ya kusikia, nataka nikwambie maneno yoyote unayosikia kuhusu mtu kutoka kwa mtu mwingine mara nyingi hayana uhalisia. Mara nyingi mtu anaongezeaga kile anachoamini yeye kuwa ni kweli. Mtu akikuambia alimuona Fulani akiingia lodge Usiishie kujawa na hasira bila kujua vitu vyote vya muhimu. Tumia akili zako vizuri, usikimbilie kumhukumu mtu kwa maneno ya kusikia.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

504; Nyama Kilo 1 ni Tsh elfu moja.

Embu jiulize leo bei ya nyama kilo moja ni Tsh elfu tano hadi elfu saba kulingana na maeneo, sasa ukipita mahali ukakuta kuna nyama ya ng’ombe safi kabisa imenona wanauza kilo moja shilingi elfu moja utavutiwa kwenda kununua? Jibu rahisi sana na ambalo kila mmoja atafanya ni HAPANA. Na itakuwa hapana kwasababu haiwezekani nyama iuzwe bei rahisi hivyo bila ya sababu.

Nyama ina thamani sana sio kitu ambacho kila mtu anaweza kukipata kama huna hela ya kutosha. Sasa kwasababu ya thamani yake ukiikuta mahali inauzwa bei rahisi sana lazima ujiulize maswali mengi ambayo hayana majibu, na pia utajaribu kutengeneza majibu yako mwenyewe kichwani, LABDA HUYO NG’OMBE WAMEMUIBA MAHALI, AU LABDA NI MG’ONJWA, AU LABDA KUNA MAMBO YA USHIRIKINA HAPO au ATAKUWA AMELALA. Kila mmoja atajiuliza swali lake na hata kama utanunua kwasababu ya usongo wa kutokula nyama kwa muda mrefu utaenda na wasiwasi sana na pia kuwauliza wengine.

Sasa embu jiulize tena kama nyama tu ambayo ilikuwa inauzwa elfu sita ikauzwa elfu moja ghafla itakupa wasiwasi wakununua inakuaje unataka kupata mafanikio kirahisi? Iweje utegemea mafanikio makubwa yaje kama maji yanayotiririka kutoka mlimani?

Kwanini sasa ukikutana na changamoto unaogopa na kusema hutaki tena? Ina maana umeshindwa kutambua kwamba mafanikio makubwa ni kitu cha thamani sana na gharama zake ni changamoto ambazo unapitia?

Naomba utambue Rafiki kwamba kama wataka mafanikio makubwa lazima ukubaliane na gharama zake. Kama wataka kuitwa mtu mkuu lazima ukubali kudharaulika, hiyo ndio gharama ambayo wapaswa kulipia. Ukiona hakuna gharama yeyote hicho kitu kinaweza kuja kukusumbua. Ukiona nyama inauzwa bei rahisi sana mtaani inaweza kuja kukuletea ugonjwa endapo utakimbilia kwasababu ya bei rahisi.

Jipe nafasi ya kutambua gharama unayopaswa kulipa na ulipie kikamilifu. Usiogope, usione mbona mambo ni mengi sana, usione mbona kuna ugumu sana, hizo ndio gharama, wewe zilipe tu baada ya muda utaanza kufurahia utamu wa kile ulichokuwa unakilipia.

Nakutakia kila la Kheri.

Ubarikiwe sana.

Rafiki Yako

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/coach

493; USIWATHIBITISHIE. (DON’T PROVE THEM WRONG)

Kwa muda mrefu nimekuwa nikiona watu wanafanya vitu mbalimbali kama ujasirimali, biashara fulani, kazi Fulani, ili tu kuwathibitishia watu fulani waliokuwa wanawaona wao hawafai. Mfano mtu aliambiwa wewe hujawahi kuweza kitu hutaweza biashara. Anaingia kwenye biashara kwa hasira ili tu amthibitishie yule mtu kwamba anaweza.

Unaweza kuambiwa wewe huwezi kupata kazi Fulani kwasababu huna elimu ya kutosha halafu ukaanza kupambana kufanya vitu mbalimbali ili tu uweze kuipata ile kazi watu wajue kwamba hata wewe unaweza.

Hii ni mbaya sana kwasababu unaweza kujikuta unatumiwa bila kujijua. Mfano mtu atakuja akwambie huwezi kufanya kitu Fulani ukafanikiwa kwasababu anataka ukifanye halafu wewe ukafanya ukaweza na yeye akajikuta ametimiza lengo lake. Wewe utaona umeweza kumwonesha kwamba unaweza lakini yeye anakucheka kwasababu ameshakutumia.

Hasara nyingine ni kwamba unaweza kujikuta unafanya hata vitu visivyo sahihi ili tu upate ile kazi au ufanikiwe kwenye ile biashara ambayo uliambiwa huwezi na ikawa ni madhara makubwa kwako. Unaweza kujikuta umetoa rushwa kwasababu unataka kwa haraka yale mafanikio ili kuwakomesha wale watu waliosema hutaweza. Unaweza kutoa rushwa ya ngono ili upate kazi ambayo uliambiwa na marafiki zako kuwa wewe huwezi ipata.

Kitu kingine ambacho ulikuwa hukijui ni kuwa unakuwa umedhibitiwa na yule mtu aliekwambia huwezi. Unajikuta unafanya kwa kupitia ushawishi wake alioweka ndani yako kwa kusema huwezi. Hivyo basi yule mtu anakuwa amekudhibiti. Kwa kifupi unakuwa ni mtumwa wake, inawezekana hata yeye asijue kwamba alikufanya mtumwa. Kibaya Zaidi ni pale anapokuwa amejua halafu akaamua tena kukutumia.

UFANYEJE?

Ukweli ni kwamba kufanya hivyo ni kutoka nje ya lengo la Maisha yako. Hujaja hapa duniani kuwaonesha wengine kuwa unaweza. Umekuja hapa duniani kuishi ishi Maisha yako vile unavyotaka, usipoteze muda hata kidogo kufanya chochote ili tu kumthibitishia mtu unaweza.

Akitokea mtu akakwambia huwezi kitu Fulani, au unachokifanya hakitakaa kikuletee mafanikio mpuuze, mwambie hajui kwanini unakifanya. Kaa mbali kabisa na mtu anaekwambia ni kitu gani huwezi, kaa karibu Zaidi na wale wanaokuonesha ni vitu gani unaweza.

Wapuuze wote na wala usifanye chochote kuwaoneshea kwamba umeweza kwani utajikuta unakimbia mbio ambazo hazina mwisho na wala faida zozote. Malengo uliyojiwekea mwenyewe ndio ya muhimu kuliko mengine. Hata mtu akija kukwambia hutayatimiza mwambie haikuhusu nisipotimiza ni juu yangu mwenyewe.

Hakuna atakaekuchapa usiponunua gari, hakuna atakae kufukuza usipotimiza malengo yako, kwa kifupi wewe mwenyewe ndio utawajibika na kuumia kwa kutokutimiza kile ulichokuwa unakitaka hivyo basi hakikisha unafanya kile ambacho moyo wako unataka.

ACHA, FANYA KILE UNACHOKIPENDA BILA YA MSUKUMO WA KUTAKA KUWATHIBITISHIA WENGINE KUWA UNACHOKIFANYA NI SAHIHI, AU WALIVYOSEMA UTAFELI WALIKOSEA.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

489; Hizi Ndio Fikra Zinazokufanya Usiendelee Kwenye Maisha.

Ndani ya jiji lenye watu wengi kuliko miji mingine ndani ya Tanzania jiji la Dar es Salaam, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya Usafiri. Hivyo basi serikali pamoja na watu binafsi wamekuwa wakiwaza kila siku ni njia gani inaweza kuwa suluhisho la tatizo hili.

Katika kufikiri huko kukatokea watu wawili ambao walikerwa sana tatizo hili la usafiri wa kugombania hasa kwenye daladala. Watu hawa walikuwa hawafahamiani lakini kwa wakati mmoja walipitia matatizo yanayofanana. Kwa wakati mmoja wakawaza kujiondoa kwenye tatizo hili la usafiri.

Kila mmoja alifikiri kwa namna yake, mmoja aliamua kuchukua mkopo akanunua gari ndogo ambayo itamsaidia kufika kwenye shughuli zake kwa urahisi na haraka zaidi, na yule mwingine akaamua kununua daladala yake mwenyewe ili aweze kupunguza adha ya usafiri kwake na kwa watu wengine Zaidi.

Watu wote hawa wana mawazo mazuri ya sana ya mabadiliko na kupanda viwango. Utofauti walionao ni katika fikra tu. Mmoja alijifikiria yeye mwenyewe na akaamua kujitatulia tatizo peke yake, na mwingine aliwaza mbali kabisa akaona hili sio tatizo tu bali ni fursa. Kama watu ni wengi kuliko daladala maana yake nikiongeza daladala zangu hapa nitawasaidia watu na pia nitatengeneza pesa.

Watu wengi tuna fikra kama za huyu jamaa alienunua gari yake binafsi ya kutembelea ili awahi haraka kwenye shughuli zake. Ni wazo zuri sana, ni maendeleo mazuri sana lakini haya ni ya kibinafsi na pia hayatakusaidia sana kama huyu aliewaza kwenda kununua daladala zake.

Kuna matatizo mengi yapo kwenye jamii na watu wanawaza kuyatatua lakini changamoto ipo kwenye aina za suluhisho tunazotaka kuleta kwenye matatizo yetu. Mara nyingi mawazo yanayotujia huwa ni ya kibinafsi Zaidi na ndio maana tunakuwa wengi tuna Maisha ya wastani na hatuendelei na kufikia utajiri mkubwa.

Ukiwa na fikra za kujifikiria wewe mwenyewe tu katika kutatua matatizo sio rahisi kuona picha kubwa kwenye matatizo unayopitia. Lazima ubadilishe mtazamo wako uanze kuwaza namna gani utawasaidia na wengine wanaopitia kwenye tatizo kama lako na sio utafute njia rahisi ya wewe binafsi kuepuka tatizo.

Mfano mwingine tuna wanafunzi wengi waliomaliza vyuo wako mitaani hawana ajira na katikati ya wanafunzi hao kuna watu wenye fikra za kibinafsi na wenye fikra pana Zaidi katika kutatua matatizo ya wengine. Wenye fikra za kibinafsi wanaweza kukimbilia kujiajiri tu mahali ambapo watapata pesa za kuendeshea Maisha yao. Wenye fikra pana za kutatua tatizo sio kwa binafsi tu bali hata kwa wengine wenye tatizo linalofanana watawaza kuleta makampuni ambayo yatapunguza tatizo la ajira. Watawaza kuja na aina mbalimbali za suluhisho ambazo zinatawasaidiwa wengi na wao watafaidika pia.

Rafiki yangu nataka uache fikra za kibinafsi katika matatizo unayopitia.

Anza kuwafikiria wengine kama wewe mnaopitia tatizo linalofanana na uone ni namna gani unaweza kuwasaidia ili na wewe ujisaidie. Ukiishia kufikiria wewe tu kwenye kila tatizo unalopitia mwisho wa siku utaishia kuwa na Maisha ya wastani, hutaweza kufanya jambo lolote kubwa hapa duniani. Watu wote waliofanikiwa na kufikia kuitwa mabilionea waliwaza katika namna ya kutatua matatizo ya watu kuliko kufikiria Zaidi wao binafsi.

Badili fikra zako kuanzia sasa. Tatizo lolote unalopitia sasa hivi kuna wengi wanapitia embu anza kuwatazama katika namna ya tofauti ona zile ni hela, yaani kwamba kila mmoja anaepitia tatizo kama lako ukiweza kulitatua basi atakulipa pesa nzuri. Zidisha hiyo pesa kwa idadi ya watu unaowaona wanapitia tatizo kama lako halafu utaona ni kiasi gani utakuwa unatengeneza.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

#usiishienjiani

www.jacobmushi.com/coach

488; Usiongeze Matumizi, Ongeza Hiki.

Badala ya kubadilisha aina ya maisha unayoishi baada ya kuongezeka kwa kipato Wekeza zaidi kwanza.

Badala ya kukununua vitu ambavyo vitakuongezea matumizi ya pesa zaidi nunua vitu ambavyo vitakurahisishia kupata pesa zaidi.

Badala ya kuongeza wanawake wengi Wekeza Kwenye baadae ya watoto wako.

Badala ya kutaka kila mtu ajue umepata pesa weka nguvu kubwa zaidi katika kuwainua wale ambao unaowapenda na kuwajali.

Haitakusadia chochote kupandisha aina ya maisha yako kwa haraka baada ya kiwango chako cha pesa kuongezeka bali kutakuangusha.

Unajua kabisa kuna aina ya Tv ukinunua lazima itakubidi Ubadili hata masofa uliyonayo ili viendane. Na kun sofa ukinunua itakubidi hata ile kapeti uliyoizoea ya kawaida uibadii. Vivyo hivyo hata kabati lile litatakiwa libadilishwe kwasababu haliendani na sofa n TV.

Mwisho wa siku unajikuta maisha yako yameishia kubadilisha vitu na hakuna cha maana ulichofanya siku chache za mbele utaanza kuona tena zile pesa hazitoshi. Kumbe ungewekeza, kumbe ungewaza kuizalisha zaidi ingekuwa na manufaa zaidi kwako.

Ni rahisi mtu kutamani simu ya gharama wakati huo huo hana biashara yoyote anayofanya.
Mtu Mmoja akasema kama huku duniani ungekuwa peke yako, vitu vingi sana hata vingepatikana bure usingevichukua. Kuna nguo wala zisingekutamanisha kuvaa.

Vitu vingi ulivyonavyo ulinunua kwasababu unataka watu wakuone. Ukweli ni kwamba hao unaotaka kuwaridhisha hawakusaidii chochote. Hao unaotaka waone umependeza hata hawakufikirii.

Sio kwamba usinunue chochote cha gharama la hasha, unaweza kuwa na malengo hayo lakini hakikisha unazo fedha za kutosha. Usiniambie fedha hazitoshagi, huo ni msemo wa maskini pekee. Matajiri wanajua fedha zinatosha matumizi yeyote wanayoyataka kwasababu kuna nyakati walisahau vitu vizuri kwa ajili ya baadae.

Mtu yeyote anaekushauri kuwa utafute halafu utumie yote kwasababu hujui utakufa lini huyo amekosa matumaini na wala usimsikilize. Mimi nakwambie tafuta na tumia kwa makini huku ukiwekeza zaidi na kuzalisha zaidi kwa ajili ya baadae. Pia sio lazima kila unachokitafuta sasa hivi ukifaidi wewe unaweza kupanda mti ukiwa na umri wa utu uzima lakini kwa malengo ya wajukuu zako waje kufurahia matunda na kivuli. Hivyo hata kama ikatokea umeondoka kuna watu hawataishi kwa kuteseka kwasababu ya juhudi ulizoweka wewe.

Maisha Yako ni Maamuzi Yako.

Rafiki Yako, Kocha Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

487; KUNA WATU UMEWAZIDI VITU VINGI, LAKINI WANAFANIKIWA, ZIJUE SABABU ZINAZOKUKWAMISHA.

Umeshawahi kusikia mtu anasema, “Mbona kama wamempendelea yule! sionagi cha maana anachokifanya wala simuelewagi!!”

Mwingine anadiriki kusema, “Atakuwa ametoa rushwa kuipata ile nafasi”, “Atakuwa anajuana na mtu kule ndio maana amependelewa”

Je na wewe unafikra za aina hii? Ukiona wenzako wanafanya vizuri unafikiri wamependelewa au wana bahati Fulani? Haujawahi kuamini kwamba watu hawa wamefanikiwa kwa juhudi walizoweka wewe unaamini tu kuna upendeleo Fulani wamefanyiwa?

Ukweli ni kwamba hutakaa uweze kufikia ndoto zako kama wewe huamini katika uwezo wa wengine. Kama ukiona wanaopiga hatua Fulani unaanza kudhani wametumia njia za mkato basi hata wewe itakuwa ngumu kufanikiwa. Hii ni kwasababu na wewe utaenda kutafuta njia za mkato halafu utafeli.

Wale watu ambao unaona wanafanikiwa kuliko wewe na ukitazama walichokifanya wala hakionekani kama ni kikubwa sana kuliko uwezo wako ni watu ambao wanajiamini. Ni watu ambao hawakujali sana kuwa wakamilifu waliamua kuchukua hatua vilevile walivyo na kilekile walichokuwa wanakijua. Wewe kwasababu unataka ujue kila kitu, unataka uwe na mtaji wa kutosha wenzako walianza hivyo hivo, wenzako walisumbua watu mbalimbali mpaka wakapewa nafasi na wakaonekana.

Kinachokukwamisha ni hiki hapa:

FIKRA POTOFU

Kikubwa kinachokufanya wewe uendelee kubaki hivyo hivyo ulivyo ni fikra zako potofu juu ya mafanikio ya wengine. Huamini kama mtu Fulani aliefanikiwa alitumia njia sahihi. Ufahamu wako umejazwa na fikra potofu ambazo zinakufanya wewe usichukue hatua na kubaki hapo hapo siku zote.

Fikra zako zinakwambia hata upambane vipi huwezi kufanikiwa kwasababu wakina Fulani walitoaga rushwa ndio maana wakafanikiwa. Kina Fulani walienda kwa mganga ndio maana wakatoka. Kina Fulani ni freemason ndio maana wamepata umaarufu mkubwa. Hizi fikra ukiwa nazo huwezi kufanya chochote utaishia kukaa na ujuzi ulionao, akili ulizonazo, bila kufika mahali popote.

Anza kwanza kubadili fikra zako ziwe chanya, ukiona dada mzuri amepandishwa cheo hata kama hana uwezo mzuri kuliko wewe acha kufikiri kwamba ametoa rushwa. Kwasababu hata wewe kuna kitu unaweza kukifanya vizuri na ukapandishwa cheo. Hata kama ni kweli alitoa rushwa wewe haikuhusu sana endelea kufanya vitu sahihi kwa ubora wa hali ya juu.

Tengeneza fikra chanya kwenye mafanikio unayoyataka amini kwamba waliofanikiwa walifanya kazi kwa bidii hawakukata tamaa. Hawakuwa wavivu kama wewe, hawakuwa watoa sababu kama wewe walikuwa wachukua hatua, walisumbua watu wa namna mbalimbali hadi wakapata fursa za kufanikiwa.

KUTOKUJIAMINI

Huwezi kufika sehemu yeyote ile kama hujiamini. Kama unajiona wewe huwezi. Kikubwa kinachowafanya uone wale wamefanikiwa lakini hawana hata uwezo mkubwa ni kwamba walijiamini sana. Hawakuangalia hawawezi nini bali waliangalia kile wanachokiweza na wakakitumia kwa nguvu zote.

Wewe ukisema usubiri ujue kila kitu ndio uanze utachelewa sana. Anza na kilekile unachokijua na kukiweza vizuri cha muhimu ni kujiamini. Mbele ya safari ndio utaendelea kuboresha.

Unaweza kuwa mmoja wa watu ambao unajua vitu vingi sana lakini huna hata kimoja ulichokifanyia kazi kwasababu tu hujiamini. Unataka ukianza tu uwe umefanya vizuri kuliko wote. Rafiki yangu hapo utachelewa sana. Huwezi kuanza kwa kufanya vizuri kila kitu lazima ukosee, lazima uanguke kisha usimame tena kama mtoto mdogo anavyojifunza kutembea.

KUSUBIRI UWE UMEKAMILIKA.

Ndio usisubiri hadi uwe na mtaji wote, usisubiri mpaka uweze kila kitu. Ukisema mpaka niweze kabisa kuna wengine wanaanza wakiwa hawajui na wanajifunza kwenye makossa yao. Kuna msemo unasema furs ani kama maembe wewe ukisubiri yaive wengine wanakula na chumvi. Maana yake wewe unaposubiri ukamilike wapo watu waanza wakiwa hawana chochote. Wako watu wanaanza na elfu kumi wakati wewe unasubiria ijae laki moja.

Wenzako wanaazima wanaanza wewe unataka kila kitu uwe umekinunua. Usipoteze muda wako kusubiri uwe umekamilisha kila kitu. Hata facebook ilipoanza haikuwa kama ilivyo sasa kuna vitu vingi sana wameendelea kuboresha na hata unavyosoma hapa wanafikiria kuboresha vitu vingine. Anza hivyo hivyo ukikosea utajifunza Njiani.

Usisubiri uje kupoteza milioni kumi anza na laki ikipotea utaumia kidogo lakini utakuwa umejifunza. Ukianza na milioni kumi ikapotea utaanguka presha ndugu yangu.

KUCHAGUA KUWA MKOSOAJI WA VITU VYA WENGINE BADALA YA MLETA SULUHISHO.

Ndio inawezekana wewe umechagua kuwa mtu ambaye unakosoa kila kitu na huku hujafanya chochote cha maana kwako mwenyewe. Wewe umekaa unasema Fulani ametoa hongo ndio maana anaitwa sana kwenye Tv kuliko mimi kumbe kuna mahali tu hujajua wakati wewe umekaa unawaza hivyo yenye anajenga mahusiano mazuri na urafiki na watu mbalimbali ambao wanampa nafasi.

Wakati wewe unapoteza muda na watu ambao wanalalamika na kukosoa tu wenzako wamekaa na watu walifanikiwa Zaidi na wanawashika mkono. Mwisho wa siku unaishia kusema wametoa rushwa, wameenda kwa mganga, wamependelewa, wana mjomba wao Tajiri na kadhalika. Utaendelea kubaki hapo kama hutoamua kutoka kwenye mkosoaji na kuwa mleta suluhisho

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

484; Ukiachwa Ni Nani Anakuwa Amepoteza?

Nilimpenda sana, nilimwonesha mapenzi yote, nilimpa kila alichokuwa anataka lakini nimeambulia kuachwa. Hayo ni mojawapo ya maneno ambayo watu wengi wamekuwa wakiyatoa baada ya kuchwa na wale waliokuwa wanawapenda sana.

Nimetafakari nikajakugundua kama ni kweli ulikuwa unamfanyia mambo yote mazuri na kumpa kila alichokuwa anataka halafu akaja akakubwaga ukweli ni kwamba sio wewe uliepoteza bali yeye ndie aliepoteza mtu aliekuwa anampenda sana. Ukiweza kuubadilisha huo mtazamo unaokufanya uendelee kuumia utapona maumivu uliyonayo.

Kikubwa hapa sio wewe kumpenda sana, wala kumpa kila alichokuwa anataka kikubwa hapa ni wewe ulipokuwa unajitahidi kuwa mtu sahihi kwake halafu akakuacha. Kwako hakitapungua kitu bali kwake ndio kutapungua kwasababu alikuwa anapokea upendo hataendelea kupokea tena kutoka kwako.

Nataka ubadili mtazamo wako ili usiendelee kuumia wala kuwaza kupoteza. Unapoumwagilia maji mti na kuutunza kwa gharama kubwa halafu ukaja kunyauka na kupotea hupaswi kuuchukia ule mti, utaumia kwa muda kidogo kwasababu ya ule upendo ulikuwa nao juu ya mti halafu utajaribu tena kupanda mti wa aina nyingine.

Usiweke mtazamo wa kupoteza kitu cha maana sana kwako wakati mtu huyo hakujali yale ambayo ulikuw unamfanyia. Ni kweli kuumia kupo na lazima uumie kama ulikuwa unapenda kweli ila hupaswi kuendelea kuumia milele, hupaswi kuendelea na mamumivu Maisha yako yote.

Usikubali kudumu na maumivu ndani ya moyo wako juu ya mtu yeyote aliendoka maishani mwako. Hakuna kinachodumu milele, sisi wenyewe hatudumu ipo siku tunakufa, watu pia hawadumu ndani ya Maisha yetu. Ukiona mtu ameondoka ujue basi ndio wakati wake wa kuondoka umefika.

Nakutakia Kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

#usiishienjiani.

www.jacobmushi.com/coach