494; Endapo Maisha Yote Uliyoishi Mpaka Sasa Yangekuwa ni Ndoto.

By | July 8, 2019

Habari Rafiki, leo naomba ujiulize swali hili la msingi sana. Iwapo umeamka asubuhi halafu ukajitazama ukakuta umerudi nyuma miaka 10 au ishirini iliyopita. Yaani kumbe yote yaliyotokea kwenye Maisha yako miaka kumi iliyopita ilikuwa ni ndoto tu ulikuwa unaota usiku wa jana.

Swali la msingi la kujiuliza je hiyo ndoto itakuwa inatamanisha kuwa kweli? Je ungependa hiyo ndoto uliyoiota iwe kweli miaka kumi ijayo? Hayo Maisha uliyoyaona kwenye ndoto ndio unayoyataka? Majibu ya wengi naamini yatakuwa ni HAPANA.

Hapana kwasababu Maisha ya wengi yamekuwa ni magumu na ya kubahatisha. Huenda hujapata ile elimu uliyokuwa unataka, huenda kwenye Maisha uliyoishi mpaka sasa imekuwa ni maumivu kila wakati. Huenda umepitia magumu yasiyoelezeka kiasi kwamba ukiwambiwa uyarudie hayo Maisha hutakubali hata kidogo.

Naomba nikwambie kitu kimoja, UNAWEZA KUYAFANYA YAWE KAMA NDOTO NA UKAANZA UPYA LEO. Maisha yako yote uliyoishi tangu jana kurudi nyuma unaweza kuamua tu yawe kama ni ndoto na ukaanza upya leo kutengeneza ile ndoto unayoitaka kwenye Maisha yako. Ni kweli itakuwa ngumu kidogo kwasababu mengi yameacha alama kabisa kwenye Maisha yako. Yameacha alama ambazo hazitaweza kuwa ndoto tena. Lakini ukiamua kutokushikilia yale yaliyopita ndio utaweza kushikilia yale yanayokuja na kuyatimiza.

Achilia yaliyopita yapite uendelee kufanyia kazi ile ndoto yako. Ukweli ni kwamba kama bado upo hai mpaka sasa na umeweza kusoma Makala hii una nafasi ya kutengeneza upya yale Maisha ya ndoto yako. Ni kweli kuna vitu havitafaa kurekebisha tena  lakini hivyo havikuhusu viache tengeneza vile vinavyofaa kutengeneza. Fanyia kazi vile ambavyo vipo kwenye uwezo ambao Mungu amekupa.

Nakutakia kila la Kheri katika Kutengeneza Maisha ya Ndoto Yako.

Rafiki Yako

Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

Leave a Reply