Watu wenye mafanikio makubwa duniani, ambao tunawaona ni matajiri waliweza kugundua siri hii kubwa na ya muhimu kwa kila mtu mwenye wazo au kipaji kizuri ndani yake. Kitakachokufanya ufanikiwe sio uzuri wa kipaji chako, sio sauti yako nzuri ya kuimba, sio watu wengi wanaokujua.
Lazima ugundue siri hii ya muhimu, ambayo ndio iliwatoa wengi sana nab ado inaendelea kufanya kazi kwa wengine. Kama hutaitambua uatendelea kubakia hivyo ulivyo tu siku zote. Tumekuwa na wasanii wengi wamepata umaarufu kisha Maisha yao yakaendelea kuwa ya kawaida na wengine wakapotea kabisa. Kwasababu walishindwa kuifahamu siri hii ya pekee.
Unaweza kuwa na wazo zuri sana na kubwa la biashara au la kuleta mabadiliko kwenye jamii ukashindwa sehemu moja tu ambayo ndio hii nakwenda kukwambia siku ya leo. Kama utakosa ujuzi huu na siri hii basi utashindwa kwenye kila kitu. Haijalishi utakuwa na bidhaa bora kiasi gani, utakuwa na vitu vya thamani kiasi gani, mafanikio yako yapo kwenye siri hii ya kipekee.
Muulize mtu yeyote unaemfamu ambaye amefika mbali utakuja kugundua kwamba aliifanyia kazi siri hii na hadi ikamletea matokeo.
Kitu cha kwanza cha kufanya kabla hujaitambua siri hii unapaswa kujinoa, na kuongeza thamani yako sana. Hakikisha umekuwa bora sana kwenye hiyo sehemu uliyopo kuliko mtu mwingine yeyote. Hakikisha umeweza kugundua vitu vingi ambayo vvitakufanya wewe uwe na thamani kubwa. Thamani yako ikiwa kubwa basi siri hii inakwenda kufanya kazi kwako kirahisi sana.
Usikimbilie kwenye siri hii kabla hujaongeza thamani yako kwa kiasi kikubwa. Najua unatamani sana niitaje hiyo siri lakini nataka ufahamu hivi vitu vya msingi kwanza ili uweze kugundua ufanyeje.
Siri hii ni KUUZA kama hutajua kuuza kile kilichopo ndani yako basi wewe hutakuwa na tofauti yeyote na watu wengine wa kawaida. Kipaji chako kinaweza kuwa kizuri sana lakini kama utashindwa kukiuza mbele za watu mafanikio utayasikia tu.
Watu wote wenye mafanikio makubwa kwenye vitu vyao walijua kuuza mawazo yao, vipaji vyao na vitu vilivyokuwa ndani yao ndio maana wakafikia mafanikio makubwa.
Kwanini nimesema pandisha thamani yako kwanza kabla hujakimbilia kuuza? Ukiwa na thamani ndogo bei yako itakuwa ndogo, hivyo basi ni muhimu sana thamani yako ikawa juu kwanza kabla hujaanza kuuza kile kilichopo ndani yako. thamani yako ndio bei yako. jitengeneze kwanza kiasi kwamba uwe unauzwa ghali. Hakuna mchezaji wa hovyo anaeuzwa pesa nyingi, lazima uwe na kitu cha pekee sana kuliko wengine ndipo bei yako itakuwa juu.
Mafanikio yako yapo kwenye thamani yako na uwezo wako wa kuuza ile thamani yako. kama ni mwimbaji hakikisha thamani yako inakuwa juu. Inakuaje juu sasa? Fanya mazoezi, jifunze mbinu mbalimbali, ongeza kitu kipya ndani yako kila siku. Mwisho wa siku ukianza kujipigia debe utakuwa haushikiki sokoni. Utakuwa na bei juu sana. Na ni lazima watu wakununue kwasababu unavitu vya thamani sana.
Watu wengi wameshindwa kuuza vipaji vyao ndio maana wamebaki wanalalamika, wengine hawajaweza kujitengeneza vya kutosha wanakimbilia sokoni. Ukikimbilia sokoni wakati bado thamani yako ni ndogo utakuwa bei rahisi. Hakikisha unajinoa sawasawa. Hakikisha unakuwa bora sana kuliko wengine.
Hakuna atakae kuzuia kama thamani yako itakuwa juu kuliko wengine na ukaweza kuuza vyema kila kilichopo ndani yako. mimi nitakuhakikishia mafanikio kama utakuwa na vitu hivyo viwili.
Jacob Mushi,