HATUA YA 102: Sababu 8 Za watu wengi kushindwa kwenye Biashara.

By | March 26, 2017
Zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kuwa chanzo cha biashara nyingi kushindwa lakini hizi ni baadhi nimeziainisha kulingana na nilivyoona watu wanavyofanya biashara zao. Angalia ni wapi unakosea kisha fanya marekebisho usonge mbele.


Kukosa Mpango
Watu wengi wana biashara lakini hawana mipango ya kuuza, kukua, wala kupanuka Zaidi. Unakuta mtu kile anachokipata na wale wateja alionao ni haohao tu kila siku. Kama huna mpango huwezi kupanua wigo wa wateja wako. Lazima uweke mipango chini ya kufikia wateja wengi Zaidi. Lazima uwe na mpango wa kupanuka Zaidi yah apo ulipo sasa hivi.  
                     
Kuridhika
Watu wengi wameridhika na kile wanachopata na pia wameridhika na pale walipofika. Kulingana na faida mtu anayopata kwenye biashara yake inatosheleza yale mahitaji ya muhimu kwenye Maisha anasahau kwamba anatakiwa kusonga mbele Zaidi. Maisha yanabadilika kila siku hivyo ukiridhika na unachokipata kuna siku utakuja kuona hakitoshi.

Ubinafsi       
Biashara nyingi hazikui kwasababu ya ubinafsi wa watu wengi. Wanashindwa kukaa chini na watu wengine waliofanikiwa na kuwashirikisha ni wapi wanataka kufika. Kama wewe utakuwa unaona hakuna wa kukushauri utaishia shimoni siku moja. Hii ni kwasababu kuna watu wengi wameshapita huko ulipo. Washirikishe wenzako unaowaamini zile changamoto unazopitia. Wafundishe wengine walioko chini yako wanaotaka msaada.     
          
Kukosa maarifa   
Ukosefu wa maarifa umekuwa ni sababu nyingine inayosababisha wengi wakwame. Kama huna maarifa ya kutosha kuna mambo mengi yatakuwa changamoto kwako. Ndio maana tunapiga kelee watu wajifunze kila siku kwa kusoma vitabu vya aina mbalimbali.  Hudhuria semina na makongamano mbalimbali ujifunze. Tembelea biashara za wenzako waliofanikiwa ujifunze kwao.  
                
Taarifa potofu   
Watu wengi hupata taarifa mbalimbali za kibiashara lakini nyingi huwa ni potofu na hazina ukweli. Kama ilivyokuwa inaenezwa kulima kitu Fulani kinalipa sana. Halafu wengi wanakimbilia kulima na kupata hasara. Kila biashara ina changamoto zake ni muhimu kupata taarifa sahihi ili ujue unavyopambana nazo.   
                  
Kukosa Hamasa   
Ukikosa hamasa kwenye kile unachokifanya lazima utashindwa kuendelea mbele Zaidi. Hamasa ndio inatumika katika kutuvusha kwenye changamoto tunazopitia. Hamasa ndio zinatuwezeshe tupande milima na mabonde. Wakati mwingine bila ya hamasa ni rahisi kukata tamaa. Hamasa inaletwa na wewe kupenda kile unachokifanya. Ukikosa hamasa hata kuwahudumia wateja wako huwezi kuwahudumia vizuri. 
           
Kukosa maono
Biashara nyingi zinakwama kwasababu hazina sehemu zinapoelekea. Kama utakosa maono kwenye biashara maana yake ni kwamba umechagua kubakia kwenye hali hiyo hiyo uliyopo sasa hivi. Maono ndio yanatuongoza kufikia sehemu mbalimbali kubwa. Nimekutana na watu wengi wanaomba ushairi juu ya kukuza biashara zao ukiwauliza wana maono gani, wameyaandika chini? Hawana na wala hawajayaandika.  Wengi hupenda kusema mimi natamani kuja kuwa mfanyabiashara mkubwa.  Kwa kusema tu bila ya kuainisha huwezi kujua ni wapi unaelekea vyema. Hakikisha huyo mfanyabishara mkubwa unaetaka kuja kuwa unamfahamu vizuri anamiliki nini? Mtaji wake mkubwa kiasi gani? Ana wafanyakazi wangapi? Na mengine yote chimba kabisa ingia ndani ujue kuna nini.  
            
Kukosa Nidhamu.
Watu wengi hawana nidhamu ya matumizi ya pesa kwenye biashara zao. Hawajui faida ni ipi na mtaji ni upi. Matatizo yakitokea hawajui ni njia gani ya kutatua. Nidhamu nyingine watu wanayokosa ni kufanya kwa bidi bila kujali upo kwenye hali gani. Haijalishi sasa unapata matokeo gani kule unakotaka kufika nidhamu ndio itakufikisha.
Chukua hatua ufanyie kazi.


Your Partner in Success
Jacob Mushi
Success Motivator, Author & Entrepreneur
Phone: +255 654 726 668
jacobmushi.com

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *