Kwenye safari ya mafanikio kuna mambo mengi yanaweza kuwa sababu ya kuturudisha nyuma kila tunapopiga hatua Fulani. Mojawapo ya mambo hayo ni madeni. Madeni haya kwa namna moja ama nyingine yanakuwa sababu ya watu wengi kushindwa kuendelea katika sehemu zao wanazofanyia kazi.

Ni hatari sana kama utakuwa na madeni mengi kwenye Maisha yako utajikuta unashindwa kusonga mbele kabisa kwenye kila hatua unayopiga. Kila ukipata kipato kikubwa kinaishia kwenye madeni. Unakuwa sawa na mtu anaetembea hatua moja mbele na kurudi nyuma hatua tatu. Kamwe huwezi kusonga mbele.
Andaa Mpango wa kulipa Madeni Yote Unayodaiwa.
Hakikisha umeandika madeni yote unayodaiwa kwenye kitabu chako. Ukishayaandika jua idadi yote kwa ujumla ni kiasi gani. Andaa utaratibu wa kuyalipa kidogo kidogo kadiri siku zinazokwenda. Chagua yale madeni ambayo unayotakiwa kuyalipa kwa haraka yaweke kama vipaumbele kisha jua ni hatua gani utachukua uanze kuyalipa. Ukweli ni kwamba huwezi kulipa yote kwa wakati mmoja. Hakikisha wanaokudai wanajua hali inayoendelea kwako ili wasije kuwa sababu yaw ewe kuzima simu au kuwakimbia. Waeleze kabisa hali uliyonayo hivyo watakuelewa. Wape mpango wako wa kuwalipa madeni yao. Fanyia kazi huo mpango hadi uyamalize.
Punguza Anasa
Kitu kikubwa kinachowafanya wengi kuingia kwenye madeni ni anasa. Anasa ni vitu vyote vile ambavyo havina umuhimu sana kwenye Maisha yetu. Yaani ni vitu vyote ambavyo hata tusipokuwa navyo bado Maisha yetu yatasonga mbele. Tuseme wewe ulikopa pesa ukaenda kununua simu ya Tsh milioni moja wakati uwezo wako bila kukopa ungeweza kumiliki simu ya laki mbili. Simu ya laki mbili ina karibia kila kitu ambacho kipo kwenye simu ya ghali uliyonayo. Ulikuwa na tabia ya kuishi Maisha juu ya kipato chako lazima uingie kwenye madeni. Punguza vitu vyote ambavyo hata ukivikosa leo bado utaendelea kuishi. Hakikisha tu unapata mahali salama kwa kulala/kuishi, hakikisha unapata chakula bora na pia hakikisha unavaa vizuri. Kama hivi unaweza kuvipata bila shida punguza mengine yote kama kwenda Baa, night club, na mengine mengi yanayovutia sana.
Ongeza Njia za Kukuingizia Vipato.
Hatua ya tatu hakikisha unaongeza njia za vipato. Kama wewe ni mwajiriwa basi jiongeze fungua biashara nyingine pembeni. Kama wewe ni mwanafunzi buni wazo la biashara hapo chuoni. Kama umejiajiri jiongeze hapo kwenye biashara yako ni vitu gani unaweza kuongeza au kufikia wateja Zaidi.

Ukiongeza mkondo mwingine wa kipato unakuwa unarahisisha kupunguza au kumaliza kabisa madeni yako. Kuna mithali inasema yeye akopaye ni mtumwa kwa yule amkopeshae. Kama wewe una madeni mengi wewe una watu wengi wanaokutumikisha.
Nimalizie kwa kusema hivi usikubali kukopa pesa ukaenda kutatua matatizo, wala kwenda kufanyia biashara ambayo hujawahi kuifanya. Usikubali kukopa pesa ukaenda kutumia kwenye matumizi yako ya nyumbani. Usikubali kukopa pesa ukaenda kununua gari. Kama utafanya hivyo basi unaukaribisha umasikini.
Kujifunza Zaidi tafadhali jiunge na semina ambayo tutaendesha kwa njia ya Whatsapp kwa ada kidogo sana ya Tsh elfu tano. Wasiliana nasi kwa 0654726668
Karibu sana.
Jacob Mushi
Entrepreneur & Author
Phone: +255654726668

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading