Habari rafiki, natumaini unaendelea vyema na safari hii ya mafanikio. Karibu sana kwenye hatua ya leo tujifunze pamoja. Leo tunaangalia  tabia tatu ambazo wenye mafanikio makubwa huwa nazo. Kama wewe ni mmoja wa watu ambao wanatamani kufikia mafanikio makubwa basi ni muhimu ukajifunza.

 

Wanadhibiti Hisia Zao.
Watu wenye mafanikio makubwa siku zote wana uwezo wa kudhibiti hisia zao, haijalishi wamepatwa na mabaya kiasi gani lakini wana uwezo mkubwa wa kutoonyesha hadharani hisia zao. Watu wengi wanashindwa kuelewa hili ndio maana hupata mawazo hasi juu ya watu waliofanikiwa sana. Ukweli ni kwamba sio kila hisia zinapaswa kusemwa hadharani. Haijalishi jambo limekugusa au kukuumiza kiasi gani lazima ujifunze kukaa kimya. Sio kila jambo linapaswa kuzungumzwa hata kama ni la ukweli. Mambo mengi unayaacha moyoni mwako kwani kusema yote ni kuumiza wengine.
Mfano mdogo ni kama leo umetoka kwenye biashara zako na zipo kwenye hali mbaya sana, wakati mwingine hutakiwi kusema tu unakaa kimya kwanza. Unaposema sema matatizo yako kuna watu watapoteza matumaini. Hata kama unaona unaelekea kushindwa kwasababu ya watu wengi walioko nyuma yako wanakutazama wewe hutakiwi kuonyesha udhaifu wala kuumizwa.
Wanafanya Zaidi.
Watu waliofanikiwa sana hufanya Zaidi. Kama waliweka lengo Fulani huenda Zaidi ya pale waliposema watafika. Wanapoahidi jambo kwa wateja wao huenda mbali Zaidi ya waliyoahidi.
Soma: Hakuna Kinachopatikana Kirahisi
Jenga tabia hii ya kwenda mbali Zaidi ya kawaida. Kama wengine wanaishia 50% ya malengo yao wewe nenda 120%. Kama uliahidi mteja utakamilisha kazi yake baada ya siku mbili fanya vizuri Zaidi kama inawezekana mfikishie baada ya siku moja.
Kama uliahidi bidhaa yako ni bora kiasi Fulani vuka ubora nenda Zaidi.
Wanasoma Kila Siku.
Kama ulikuwa hujatambua watu waliofanikiwa kusoma kila siku ni tabia yao kubwa na ya muhimu sana. Kinachonishangaza sana ni wewe unasema unataka mafanikio lakini hutaki kujifunza. Hutaki kusoma vitabu hutaki kusikiliza vitabu vya sauti. Muda wako mwingi umewekeza kwenye kutazama filamu na taarifa za habari ambazo hazikujengi.
Labda nikuulize mtanzania mwenzangu, kuna matukio ya ajabu ajabu yalianza kipindi tunaanza mwaka hadi sasa, yamekuwa yanajadiliwa kwenye  mitandao ya kijamii sana. Mara nyingi mimi nilikuwa nafuatilia sana kuona watu wanasema nini na wanawaza nini. Kitu cha ajabu unakutana na mtanzania mtu mzima anasema yeye yupo tayari alale njaa lakini asikose kifurushi cha intaneti ili aweze kufuatilia habari hizo na mijadala hiyo. Yaani mtu anasahau kabisa kwamba kuna vitu anatakiwa afanye na vya muhimu sana kuliko hata mijadala inayoendelea. Mtu huyo haweza kusema hakubali kifurushi kiishe ili aweze kusoma vitabu au atembelee mitandao ya kuongeza maarifa kwenye akili yake.
Mafanikio hayaji kirahisi ndugu yangu. Lazima ukubali kuwekeza kwenye akili yako. Hiyo akili uliyonayo sasa hivi haiwezi kukufikisha kule unakotaka kwenda. Lazima ukubali kuongeza maarifa kama unataka kusogea mbele.
Mafanikio sio lele mama lazima ukubali kulipa gharama. Sahau vitu ambavyo havina umuhimu kwenye safari yako. vipe vipaumbele vitu ambavyo vinakupeleka unakoelekea.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading