Jambo lolote unalotamani kulifanya linaanza na uthubutu wa kuchukua hatua ya kwanza, kama hutajaribu kuanza kupiga hatua hautaweza kwenda mahali popote.

Mtoto mdogo anaweza kusimama kwa kuanza kusimama kidogo kidogo huku akiogopa na mara nyingine huanguka.

Nakumbuka nilikuwa na mdogo wangu mmoja wakati akiwa mdogo aliogopa sana kutambaa, ikabidi tuwe tunamwekea kioo mbele yake. Anapojiona kwenye kioo anaanza kutambaa kukifata kioo, kadiri anavyokaribia kioo tunakisogeza mbele. Zoezi hili tulilifanya hadi akaweza kutambaa.

Wakati mwingine mtoto anaposimama hua anaogopa kuanguka, inabidi unamsimamisha kisha unamwachia bila kujua kisha unamwambia ona umeweza kusimama mwenyewe! Hii inaanza kumjengea ujasiri taratibu.

Mafundisho kwenye mtandao huu yakawe ni chachu kwako kwenye kufanya uthubutu wa kile unachokitaka. Haijalishi utafeli au utaanguka. Hilo ni kawaida sana, mtoto mdogo anapoanguka sio mwisho wa kujaribu kusimama au kutembea.

Shida kubwa ipo kwenye kuanza, huwezi kutamani kukimbia wakati hujawahi hata kujaribu kutembea. Tatizo kubwa lipo pale tunapowatazama wanaokimbia na tunataka tukianza kesho tujua kukimbia. Huwezi kujua kila kitu kwa siku moja.

Wenzako wanaoweza kukimbia hawajaanza leo, wenzako walioweza kuruka hawajaanza leo. Sio lazima utamani kuonekana mbele za watu mapema hii unapojaribu kusimama au kutembea. Sio watu wote watafurahia ukianguka wengi watakukosoa. Jifunze kutembea mbele ya watu wachache wanaopenda maendeleo yako.

Kama wewe ni mwimbaji anza kujifunza kuimba mbele ya watu wachache, jaribu kupanda juu ya majukwaa ya watu wachache kwanza. Kama wewe ni mtangazaji anza kuzungumza na watu wachache kwanza.

Ili ufike hatua mia moja lazima ukubali kupiga hatua moja kwanza na kuendelea.

Anza sasa, thubutu, chukua hatua, acha woga, unaweza kufika mbali sana kama utaanza leo.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading