Inawezekana umeshangazwa na kichwa ambacho kinaenda leo. Ni kweli leo nataka tuangalie juu ya vitu ambavyo mara ya kwanza huanza kwa hamasa kubwa lakini ukishaanza kuingia katikati ndio unaanza kuupata ukweli halisi.
Mara zote kitu chochote kipya huwa kinahamasisha sana. Wapenzi wanapoanza mahusiano siku za mwanzo wanafurahiana sana. Kila mmoja anaweza kumpa mwenzake ahadi ambazo ukiziangalia kwenye uhalisia wewe ulieko pembeni yao unaona kabisa hazitekelezeki. Watu hawa hawa wanaambiana siwezi kukuacha kamwe, siwezi kuishi bila wewe, bora nikose vyote lakini nibaki na wewe. Na mengine mengi unayoyajua.
Kitu cha kushangaza sana ni muda unavyozidi kwenda mbele. Mambo yanaanza kubadilika ile hamasa inaanza kupungua. Kila mmoja anaanza kumuona mwenzake ni wa kawaida. Zile ahadi zinaanza kusahaulika. Hapa mtu ndio anaanza kuona kumbe naweza kuishi bila yeye. Anaanza kupunguza hata zile sms za kila saa. Sasa ukifika wakati mkwaruzano wowote umetokea ndio utaanza kuona kumbe zile ahadi zilikuwa ni za hamasa tu.
Kwanini nimekwambia hivi rafiki yangu nataka uone kwenye vitu. Unaponunua simu mpya au nguo mpya au hata gari jipya unakuwa na hamasa sana wakati wa mwanzo unapoanza kulitumia. Lakini kadiri unavyolizoea ndio unaanza kufahamu vyema madhaifu yake. Hapo ndio wakati hasa unatakiwa ujue kwanini uliamu kumiliki kitu hicho. Kama ulivutiwa tu kwa nje basi utatamani ukiuze ili ununue kingine kipya.
Usishangae sana kitu chochote mwanzoni kinakuwa na hamasa kubwa sana lakini katikati wengi wanaishia njiani.
Soma: Tabia ya Uvumilivu Ili Ufanikiwe
Hata biashara mpya mtu anapoanza anaanza kwa hamasa kubwa sana anajiona anakwenda kuwa bilionea kesho, lakini sasa akishaanza kuziona changamoto anakimbia na kuacha biashara kabisa.
Jambo moja nataka ufahamu ni kwamba wakati sahihi wa kujua kama mpenzi wako, biashara yako au chochote ulichosema unakipenda sana utadumu nacho hadi mwisho ni wakati unapitia magumu na changamoto. Hapa ndio unapimwa uvumilivu wako.
Epuka sana kuahidi vitu vingi sana wakati bado hujapitia changamoto yeyote. Kwenye mahusiano unaweza ukampenda mtu ukafikiri kama ndio mwisho wa Maisha kabisa. Ukakimbilia kumtambulisha kila mahali halafu kesho kutwa unakuja kugundua sio au wewe mwenyewe unachoka kutokana na changamoto unazokutana nazo. Embu jipe muda kwanza subiri uone kama utaweza kuvumilia changamoto.
Hakuna mahali uliona Maisha yanakuwa na raha siku zote kamuulize hata baba yako au mama yako kama wanapitia raha siku zote. Hivyo uvumilivu wakati wa changamoto ndio kipimo halisi cha ahadi ulizotoa wakati wa raha.
Rafiki yangu penzi change linapendeza sana kila mtu anatamani abakie hapohapo milele kwasababu ndio kuna kufurahiana. Lakini haiwezekani lazima msonge mbele mpitie kwenye miiba.
Nina neno Moja kwako CHOCHOTE ULICHOAMUA KUKIPIGANIA USIKUBALI KUISHIA NJIANI.
Ila usisahau kama umepanda gari ulikuwa unakwenda Arusha ukakuta gari inaenda Mbeya utashuka tu ila kama linakwenda Arusha usishuke kwasababu limepata pancha njiani.
ENDELEA MBELE UFIKIE HITIMISHO.
Ni mimi Rafiki Yako,
Jacob Mushi