Kwa nje anaweza kuonekana ni mtu mzuri kuanzia sura yake, kauli zake, na tembea yake lakini ndani yake kuna mengi yanakuwa yamejificha. Ni bora sana mtu akikutazama kwa nje aone uhalisia wako kuliko akaona vile ulivyoamua kumwonyesha.

Sehemu yenye mtego huwa inavutia sana kwa nje, ukishaingia ndani ndio utagundua kwamba ulikuwa mtego. Usikubali kuvutwa na mwonekano wa nje wa chochote.
Ni kweli kabisa lazima uanze kuvutiwa na nje ndipo ufanye maamuzi ya kuingia ndani. Lakini unachotakiwa kufahamu ni kwamba uzuri wa nje  wa chochote usifanye wewe utoe majibu ya  mwisho. Ingia ndani Zaidi kuujua ukweli.
Usipende kufanya maamuzi kwa picha ya nje endelea kufunua ndani Zaidi utakutana na ukweli wa kile kilichorembwa. Vingi vinarembwa kwa nje ila ndani vinabeba vitu tofauti.
Mtu akikuwekea mbuzi kwenye gunia akakwambia huyu ni mbuzi usitoe pesa kabla hujajiridhisha kama ni mbuzi kweli kwani hata binadamu anaweza kutoa mlio wa mbuzi.
Watu wengi hupenda kuonekana wana furaha lakini ukweli ndani yao wana huzuni kubwa. Ni bora uonekane una huzuni kwa nje lakini ndani una Amani ya moyo.
Ukiletewa fursa ambayo kwa nje wameeleza sana jinsi ambavyo unaweza kufanikiwa haraka usikubali kirahisi. Ingia ndani Zaidi usiridhike kwa kuonyeshwa picha. Usiridhike kwa kuonyeshwa mambo mazuri pekee tafuta kujua pande zote mbili. Wengine watakuona labda huna fikra chanya lakini unautafuta ukweli.
Ukweli upo upande wa pili ambao hauonekani. Ukweli wa jambo lolote unaloliona ni zuri sana upo upande wa pili wewe utaonyeshwa upande mmoja tafuta kujua na upande wa pili. Ukikuta upande wa pili ni mzuri utakuwa hujapoteza chochote. Ukikuta upande wa pili ni tofauti na walivyokuonyesha utakuwa umejiponya.
Kuna msemo unasema USIKUBALI KUSHIKIWA AKILI. Maana yake itumie akili yako kufikiri sio kila unaloambiwa unakubali kirahisi.
#USIISHIE_NJIANI


Jacob Mushi
Mwandishi na Mjasiriamali.
Phone: +255654726668

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading