Tunavyojifunza kila siku ni kwamba watu hawafanani hata siku moja. Tuna vitu vingi sana ambavyo vinatufanya tuwe tofauti tofauti. Tukianza na mazingira tuliyopo, Maisha tuliyoishi, watu ambao tumekuwa nao, shule tulizosoma na vingine vingi. Hapo bado kuna tabia ya mtu binafsi.
Ukiweza kutambua hivyo huwezi kugombana na mteja wako hata siku moja kutokana na tabia yake. Ukielewa kwamba kuna watu ambao wanaishi Maisha ya tofauti na unayoishi wewe utaweza kuwahudumia kila mmoja na wote wakaridhika.
Mteja anaekuja akijua ni kitu gani anataka.
Huyu ni mteja ambaye anakuja kwenye biashara yako akiwa ameshaamua tangu nyumbani kwake anakuja kununua kitu gani kwako. Wateja hawa mara nyingi wanakuwa ni wazuri sana kwasababu hawauliziulizi maswali mno wanasema wanachotaka unawahudumia na kuondoka.
Tatizo linakuja pale ambapo wewe unatamani umuuzie bidhaa nyingine Zaidi. Mteja kama huyu unapaswa kujenga nae ukaribu Zaidi ili unapomweleza kuhusu bidhaa nyingine nzuri ulizonazo aweze kukuelewa na kufanya maamuzi mengine.
Changamoto ya wateja wa aina hii wanakuwa ni wagumu sana kuwashawishi wanunue bidhaa ya aina nyingine hivyo unatakiwa utumie mbinu za aina mbalimbali ili umteke awe anakuja kwako tu na aongeze anavyonunua.
Ni muhimu ukamfahamu kama anaishi na nani ili uweze kujua unapomshawishi unagusa wakina nani anaowajali. Mfano ukajua ana watoto wadogo unaweza kumwonyesha bidhaa ambazo watoto wake wangependa. Wakati mwingine unaweza kumpa kama nyongeza akawape watoto wake. Mteja kama huyu hawezi kukuacha kamwe kwasababu umeonyesha kuwajali hadi watoto wake.
Soma: Kubali Kupata Hasara
Mteja Asiejua ni Kitu gani Anataka.
Mara nyingi wateja kama hawa wanaonekana ni wateja wasumbufu sana kwenye biashara. Wateja wa aina hii wanapenda kuulizia vitu vingi sana lakini anaweza kununua kitu kimoja. Wafanyabiashara wengi wamekuwa hawawapendi wateja wa aina hii. Kitu unachokosea ni kwamba huyu ndie atakuja kuwa mteja wako mzuri sana hapo baadae kama utamwezesha ajue ni kitu gani kinamfaa.
Kuna duka niliwahi kwenda kipindi cha nyuma muuzaji anakupandisha na kukushusha akiona kwa mwonekano wako hauna pesa basi hataonyesha kukujali kabisa. Kawaida hakuna mtu anaependa kufanyiwa hivyo awe na pesa au asiwe nazo. Ukimfanyia hivi mteja wako unakuwa umefukuza wateja wengi sana ambao wangekuwa nyuma yake.
Mteja asiejua kitu gani anataka ni jukumu lako wewe kumwelekeza na kumwonyesha kile kinachomfaa. Tambua kwamba sio kila anaekuja atakuwa na ufahamu wa bidhaa zako. Ni jukumu lako wewe kumwonyesha anafaidikaje na bidhaa anayotaka kununua.
Ukikaa unataka wale wanaokuja na kutoa pesa na kuondoka utaharibu biashara yako. mteja mzuri anatengenezwa.
Mteja mwenye Wasiwasi.
Huyu ni aina ya mteja ambaye ana wasiwasi na bidhaa zako au huduma zako. Usijaribu hata siku moja kuwa mkali kwa mteja wa aina hii utampoteza. Kuwa mpole jibu maswali yake yote kwa furaha kabisa.
Wasiwasi wake unaletwa na kuogopa kupoteza pesa yake kwa kununua kitu kisichomfaa. Ni kazi yako kumwonyesha faida anazokwenda kupata baada ya kununua bidhaa yako. Mfanye aone hapotezi pesa yake kwa kununua bidhaa yako.
Kama upo kwenye biashara na unaona ni kazi sana kujibu maswali ya wateja wako ni bora ukaondoka hapo. Sio kila anaekuja kwenye biashara yako anafahamu kila kitu ni jukumu lako kuwaelewesha vyema na wasiwasi ukamwondoka.
“Usije ukasema nachukia wateja wa aina hii wanauliza maswali weee halafu wanaondoka bila kununua chochote” unakosea sana. Hiyo ndio kazi yako asiponunua leo atakuja kesho. Asiponunua yeye atakwenda kuwaambia wengine. Mweleze kwa furaha na tabasamu pana.

 

Rafiki Yako,

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading