Mojawapo ya dalili za kuanguka kimafanikio ni pale pesa inapoanza kumtawala mtu. Tunaposema mtu ametawaliwa na pesa ni pale pesa inapofanya maamuzi badala ya mwenye pesa kufanya maamuzi. Ukiona umefikia kiwango ambacho ukipata pesa kila mtu anajua una pesa na zikiisha kila mtu anajua zimeisha ujue wewe pesa imekutawala.
Ukiona umefikia mahali pesa ndio inaamua kitu cha kununua badala ya wewe kuamua nini cha kufanya na pesa umetawaliwa.
Ukiona kale ka usemi Kanaitwa “pesa inaongea” kanakujia sana unapokuwa na pesa ujue pesa imekutawala.
Ukianza kuona wewe ukipata pesa tabia zako zinabadilika ghafla unaanza kwenda sehemu ambazo huendagi. Unabadilisha hadi marafiki ujue wewe ni mtumwa wa pesa. Kamwe usikubali ubadilishwe na pesa au uongozwe na pesa.
Pesa siku zote zinakaa kwa mtu anaeweza kuzitunza na kuzizalisha. Pesa zinawakimbia wale ambao wanajua tu kutumia pasipo kuzitengeneza.
Soma: Tatizo Sio Pesa tatizo ni Wewe
Njia pekee ya kuepuka kuwa mtumwa wa pesa au kutawaliwa nayo ni kuanza kujitengenezea mazoea ya kumiliki pesa nyingi. Unajitengenezea mazoea haya kwa kuanza kujiona ukiwa na pesa nyingi zile unazotamani kuwa nazo.
Kuza ufahamu wako juu ya pesa. Kama ufahamu wako juu ya pesa ni saizi ya ndoo ukipata pesa inayojaa pipa lazima zitamwagika. Na zinapomwagika ndio tunaona huku nje matendo yako yakibadilika baada ya kupata pesa nyingi.
Achana na maneno ya kusema “tumia pesa ikuzoee” anza kuongeza ufahamu wako na kuitafuta pesa kwa njia nyingi pesa itakuzoea tu. Pesa itakuzoea kwa kujua njia nyingi za kuitafuta na sio kutumia.