Kabla Hujawaza kupata laki tano ya kuanzia biashara anza kuonyesha uwezo wako wa kutumia elfu hamsini. Kama ukishindwa kujua utaitumiaje elfu hamsini hata laki tano utashindwa kuitumia vizuri.

Watu wengi tumekuwa tunalalamikia tatizo la mtaji  lakini tatizo sio mtaji tatizo lipo kwenye akili yako. Ili uweze kupata kile kikubwa unachokitaka jifunze kutumia kidogo kilichopo karibu yako.
Kwenye Biblia wale watumwa waliogawiwa talanta wawili waliweza kuzitumia vyema na wakazalisha Zaidi lakini yule aliepewa talanta moja aliifukia chini. Wewe unaelalamika huna mtaji au mtaji ulionao hautoshi huna tofauti sana na aliefukia talanta chini.
Kwasababu kama umeshindwa kutumia kile kidogo unataka kikubwa cha kupeleka wapi? Hicho kikubwa utakiweza? Una watu wangapi wanakufahamu wewe kwa majina yako? Hawa watu wanakula, wanavaa, wanatumia vitu mbalimbali kila siku na vitu hivyo wananunua. Ulishawahi kuwaza kuwauzia kitu chochote kati ya vile wanavyotumia?
Tafuta watu 30 unaowajua mtaani kwako wanaokunywa chai na vitafunwa asubuhi. Waambie unawapelekea vitafunwa wanavyotaka wasinunue mahali pengine. Ukianza na elfu 20 kwa muda wa asubuhi tu unaweza kutengeneza faida nzuri tofauti na ukikaa nyumbani bure. Hao hao wateja utaendelea kugundua ni vitu gani wanahitaji ili uendelee kuwahudumia. Muda sio mrefu sana utakuwa umeanzisha biashara kubwa sana.
Rafiki yangu mmoja aliniambia yeye alikuwa anasoma chuo, sasa kwenye hosteli aliyokuwa anaishi kuna wenzake huwa wananunua chakula kila siku. Walikuwa kama kumi hivi, kwa chakula sahani moja ni tsh 2500. Huyu rafiki yangu akawaomba awe anawaletea chakula kila siku jioni wao wasiende kununua wenyewe. Kumbe huyu rafiki yangu akienda kwa mama muuzaji anamwambia nipe sahani kumi kwa tsh 2000. Akija kuwaletea wenzake anakuwa ametengeneza sh. Elfu tano ndani ya dakika chache tu.


Huyu rafiki yangu hakuwa na mtaji wowote, hakuwa na mgahawa, alikuwa na akili, akili ikampa wazo, akalifanyia wazo kazi kisha wazo likamletea pesa. Usisubiri kitu kingine chochote kikuletee mabadiliko ambacho hakitoki ndani yako, la sivyo kitakuwa ni maumivu makubwa.
Haijalishi umefeli shule au una kasoro ya aina gani. Jaribu kufikiri sawasawa utaona njia nyingi za kubadilisha Maisha yako. achana na wanaokusema maana huwezi kwenda kuwaomba hela ukiwa na njaa. Kuliko ukawaombe hela tafuta kitu ambacho utawauzia wakupe pesa. Kama watashindwa kununua hicho kitu hao hawana maana hata wakikusema.
ANZA NA KIDOGO ULICHONACHO.

#USIISHIE NJIANI
Usiache kusoma Kitabu cha SIRI 7 ZA KUWA HAI LEO wasiliana nami kwa 0654726668.
Jacob Mushi
Mwandishi, Mjasiriamali na Mhamasishaji.
Simu: 0654726668
jacobmushi.com.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading