HATUA YA 217: Hiki Ndio Kinakuzuia Kufanikiwa.

jacobmushi
3 Min Read
Umeamua Kuyatafuta mafanikio lazima ukubali kujikana uache kuishi yule mtu wa zamani ambaye alikuwa hakuletei maendeleo. Huwezi kusonga mbele kama bado umeshikilia tabia zile zile za zamani, lazima ukubali kuaziacha ili upokee mabadiliko mapya.
Huwezi kuotesha mbegu kwenye shamba ambalo halijafanyiwa usafi. Kubali kufanyia usafi kwenye Maisha yako ili upokee vitu vipya. Mbegu zinazooteshwa kwenye shamba ambalo halikufanyiwa usafi hufa. Kama hujafanya usafi kwenye Maisha yako utaendelea kuona kila unachokifanya kinaharibika au kuishia njiani.
Kubali leo kutengeneza Maisha yako ili ufike kule unapotaka kufika. Matengenezo yeyote ya Maisha yanaanza kwenye ufahamu wako.
Badilisha ulichokuwa unaingiza kwenye akili.
Ili uanze sasa kupata mabadiliko lazima uanze na chanzo cha hali uliyokuwa nayo. Anza kubadilisha kila ulichokuwa unaingiza kwenye akili yako kisichofaa.
Zipo taarifa nyingi unazipokea kila wakati ambazo zinaharibu uwezo wako wa kufanya kazi. Ili uweze kuzibadili lazima ukubali kufanya kitu cha ziada.
Anza kusoma vitabu kulingana na kile kitu unachokitaka wewe. Wakati wa kufanyia usafi shamba sio kitu rahisi hasa shamba ambalo halijawahi kulimwa kabisa, kunakuwa na miiba, wadudu, mawe. Hivyo utakutana na vikwazo vingi katika kubadilisha kilichokuwa kinaingia akilini mwako.
Badala ya kutumia muda wako na simu yako kusoma vichekesho soma Makala nzuri za kukufundisha. Tafuta makundi mazuri ambayo utajifunza mambo chanya.
Badilisha marafiki uliokuwa nao.
Haiwezekana unataka kuolewa halafu bado kampani yako kubwa ni mabinti wenzako ambao hawajafikiria kuolewa. Haiwezekana unataka kuoa halafu vijana wenzako ulionao kila siku wanasema bado wanakula ujana.
Marafiki unaokaa nao wana mchango mkubwa sana wa jinsi ulivyo sasa hivi. Kama unataka kubadilisha kile kinachoendelea kwenye Maisha yako sasa hivi badilisha pia marafiki. Tafuta marafiki ambao angalau wanafanana na wewe. Kama unawaza biashara wawe ni ambao wana biashara zao. Kama unawaza kuingia kwenye ndoa wawe ni ambao wana mpango wa kuoa/kuolewa karibu au wewe tayari kwenye ndoa.
Hawa ndio unaweza kushauriana jambo mkaelewana. Hawa ndio lugha zenu zinaweza kufanana. Haiwezekana wewe unazungumzia biashara rafiki ulienae anazungumzia kutumia pesa kwenye starehe. Haiwezekani wewe unazungumzia kuwekeza yeye anazungumzia kununua vitu vya gharama kwa pesa anazopata.
Anza Kuchukua Hatua.
Chochote kile unachokitaka kutimiza kwenye Maisha yako anza sasa kukifanyia kazi. Acha na sababu zozote ulizonazo na uanze na kile kidogo ulichonacho.
Shamba likifanyiwa usafi na likaachwa bila kupandwa chochote magugu huanza kuota upya. Anza kufanyia kazi ndoto yako. Anza pale pale ulipo sasa usingojee hadi hali iwe nzuri.
Usitazame yale ambayo huna tazama una nini kisha angalia ni kwa namna gani unaweza kukitumia ulichonacho kuanza. Hakuna mwanadamu asiye na kitu kinachotufanya tusiweze kuchukua hatua ni kuvitazama tusivyo navyo badala ya vile ambavyo tayari Mungu ametupa.
Jacob Mushi
Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading