Yapo mambo mengi tunaweza kujifunza kupitia hayo kama tu tutaweza kuyatazama kwa jicho la kujifunza. Kama utashindwa kutazama kwa jicho la kujifunza utaendelea kuyaona mambo kama kawaida ulivyozoea kuona siku zote.

Kuku siku zote baada ya kuangua vifaranga vyake anaingia katika majukumu ya ulezi wa vifaranga vyake. Anapaswa kuwalinda na Wanyama wabaya na ndege kama mwewe na kipanga. Kuku pia huhakikisha kabla hajala yeye vifaranga wake wote wamepata chakula.

Wakati anawatafutia chakula hawa wanawe hajawahi kuwaambia kwamba nawatafutia chakula lakini mpo darasani. Ni jukumu la kila kifaranga kujifunza kutoka kwa mama yake namna ya kujitafutia chakula mwenyewe na namna ya kujificha adui anapojitokeza.

Vifaranga hawa baada ya muda Fulani mama yao huona wameshakuwa wakubwa sasa na wanaweza kujitafutia chakula wenyewe huanza kuachana nao, huwafukuza kabisa na ikiwezekana kuwapiga. Kifaranga nae anatakiwa akajitegemee atafute Maisha yake. Kama ni mtetea basi ajifunze na yeye kutaga mayai Ajifunze namna ya kujitafutia chakula chake mwenyewe kama kuku wengine wazima.

Sasa cha ajabu sana kwetu sisi binadamu tunashindwa kujifunza kwa kuku ambaye yeye ameishia kwenye kutaga, kutafuta chakula na kujikinga na adui (tena kuku huyu ni wa kienyeji sio hawa wa kisasa). Mwanadamu unaweza kumkuta ni mzazi anaishi na watoto wake wakubwa kabisa umri wa utu uzima wameshafika na kama ni wanaume basi ndevu zimeshaanza kuota lakini bado yupo nyumbani.

Binti ameshakuwa kama mama yake kabisa lakini bado yupo nyumbani anatazamana na mama yake kila saa. Ni hatari sana unaweza kufikiri unamsaidia mwanao, unamwonesha upendo, unampatia kila anachotaka, akiomba pesa unampa kwasababu zipo lakini unamlemaza bila ya kujua.

Kikawaida alipofikisha umri wa miaka 18 haijalishi ni jinsia gani anapaswa kujifunza namna ya kuanza kujitegemea hata kama bado anakaa hapo nyumbani kwako. Unapaswa kumfundisha namna ya kujitafutia pesa zake mwenyewe. Unaweza kufikiri unamsaidia kwa kumpa kila anachotaka kumbe ndio unamharibu. Kama ni binti basi akija kuwa na mwanaume wake akitaka kitu basi ni wakati huo huo anataka apewe kwasababu hajawahi kuambiwa kuna nyakati hakunaga pesa, au kama zipo basi ni za matumizi mengine.

Soma: Miliki Maisha Yako. 

Lazima ujifunze kutengeneza kizazi bora ambacho utakiacha hapa duniani. Haijalishi unaacha urithi mkubwa kiasi gani kama unaowaachia hujawaandaa utakuwa umeupoteza urithi ulioacha.

Tumekuwa na familia nyingi zikiporomoka kabisa baada ya baba kufariki kwasababu ya kuwa na watoto wasio jua namna ya kujitegemea. Tumekuwa na wamama ambao hawajui kutafuta pesa wamezoea kupewa kila kitu.

Maisha yatakuwa magumu sana hasa baada ya yule uliekuwa unamtegemea kuondoka. Ndio ni kweli mume wako anapaswa akuhudumie lakini unapaswa kutambua kuna nyakati anaweza kuondoka duniani je utatafuta mwanaume mwingine kwasababu huna wa kukuhudumia? Ni vyema ukatafuta kwasababu nyingine lakini sio hiyo ya kumtafuta mtu wa kukuhudumia.

Jifunze na wafundishe watoto wako kujitegemea, haijalishi ni jinsia gani usiwazoeshe sana kuwapa kila wanachotaka. Waonyeshe ni namna gani pesa inatafutwa. Mtoto wa kike anaejua ni namna gani pesa inatafutwa haiwezekana akaja kuteseka kwenye ndoa yake.

Haiwezekani akaingia tamaa ya vitu na kujikuta amedanganywa na wanaume. Kama ni zawadi mpe pale panapostahili lakini usimjengee mazoea ya kupata kila anachoomba. Akija amelia kidogo umeshampatia pesa. Unamlemaza hujamsaidia chochote.

Jifunze kwa kuku anaefukuza vifaranga wake ili wakatafute chakula wenyewe waache kufuatana na mama yao nyuma.

Ni mimi Rafiki Yako,

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading