Mimi binafsi ninapokwenda mgahawani kwa ajili ya kupata chakula au kinywaji nikifika nikashindwa kuhudumiwa vizuri hua ninaondoka. Kwasababu gani? Kwasababu kama huwezi kunishawishi ninunue kwanini nikupe hela yangu na hujafanya chochote cha ziada. Kwasababu mimi binafsi sijaichukua mahali kama unavyotaka kuichukua kwangu.

Sasa Maisha nayo ni kama mgahawa, ni mgahawa ambao una kila kitu ambacho unakitaka. Kwenye meza uliyopo kuna menu ya kila unachokitaka. Lakini kwenye mgahawa huu wa Maisha hakuna wa kukuletea, hakuna wa kukuandalia. Kwenye mgahawa huu wa Maisha ukisema ukae kwenye meza usubiri mhudumu akuletee unachokitaka hatakaa atokee.

Kwenye mgahawa huu unapaswa kuinuka hapo ulipo baada ya kuchagua unachokitaka uende ukajitengenezee mwenyewe. Wewe ndio mpishi na mhudumu wa kile ulichokuchagua kwenye Maisha yako.

Kitu cha ajabu wengi tumebaki kwenye meza tunasubiri baada ya kuchagua kile tunachokitaka. Naomba nikwambie kwenye mgahawa huu wa Maisha hakunaga wahudumu wala wapishi. Inakubidi uende jikoni mwenyewe ukapika.

Umefika kwenye mgahawa huu utawakuta wenzako wanakula unaweza kula kama wanachokula pia lakini lazima ukajiandalie mwenyewe. Chakula chochote kizuri unahokiona mezani wenzako wanakula kimewachukua muda kukiandaa jikoni.

Mgahawa wa Maisha, hauihitaji kelele nyingi ukiwa jikoni unajiandalia kile unachokitaka.

Soma: Fanya Maamuzi

Mgahawa wa Maisha unakuruhusu wewe kumuuliza yeyote uliependa chakula chake jinsi alivyokiandaa yeye anaweza kuamua kukupa maelekezo au asikupe. Usiogope wapo watu wema ambao watapenda na wewe uweze kula kama wanachokula watakuelekeza ili mradi tu utakwenda kuandaa mwenyewe.

Mgahawa huu wa Maisha una kila aina ya unachokitaka unachopaswa kujua ni kukiandaa mwenyewe tu. Hakuna wa kukuandalia ila wapo wa kukuelekeza. Wapo ambao unaweza kujifunza kwao.

Rafiki yangu ukishajua kutengeneza kile unachokitaka kwa bahati nzuri sana kwenye mgahawa huu inakuwa rahisi sana kwako kutengeneza na vingine na vingine kwa urahisi Zaidi. Usiogope, usijione upo mwenyewe. Tafuta ambaye unafikiri anaweza kukusaidia.

Ukiharibu chakula unachokiandaa huna wa kumlaumu, hakuna mhudumu wa kumpigia kelele umwambie akuletee. Utawajibika kwa kila unachokitaka.

Huo ndio mgahawa wa Maisha ndugu yangu. Nikukumbushe tu ukimaliza kuandaa chakula chako usiwe mchoyo kuwawezesha wengine wanaopata shida kuandaa vyakula vyao. Waandalie mwongozo ambao unafikiri wanaweza kuutumia kutengeneza na wao kile wanachokipenda.

Kinachonisikitisha sana ni kwamba kuna ambao wamebaki kwenye meza zao hawajui ni nini cha kufanya. Kuna ambao wamebaki kuiga wenzao. Kuna ambao wameingia jikoni wanakwama lakini wanaogopa kuuliza maswali. Kuna ambao muda mwingi wameutumia jikoni kuliko mezani.

KUMBUKA:

Kwenye mgahawa huu kuna vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza ni kuchagua ni aina gani ya chakula unataka na kujifunza namna ya kukiandaa. Kipindi cha pili ni kuingia jikoni na kuandaa ulichochagua.

Kipindi cha tatu ni kula kile ulichopika jikoni.

Hakuna anaejua ni saa ngapi ataambiwa muda wa kuwepo kwenye mgahawa umekwisha. Kuna ambao wameondolewa mgahawani wakiwa bado wanachagua. Kuna ambao wameondolewa wakiwa jikoni wanaandaa na kuna ambao wameondolewa wakiwa katikati wanakula.

Soma: Kitabu Mbinu 101 za Mafanikio

Unachopaswa kufanya ni kujua namna ya kuutumia muda wako vizuri. Kile kipindi ulichonacho kitumie vizuri. Wakati wa kujifunza jifunze vizuri, wakati wa kuandaa andaa kwa makini. Uje ufurahie matunda ya kazi yako.

Kuna ambao wameishia kula chakula walichopikiwa na kuna ambao wamewakuta waliowaleta hapa mgahawani bado hawajajua wapike nini. Kila mmoja anayo nafasi ya kuandaa kile anachokitaka haijalishi yupo upande upi.

Karibu kwenye Mgahawa wa Maisha.

Ni mimi Rafiki Yako,

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading