Nilipokuwa mdogo nakumbuka ilikuwa unapoharibu jambo mama akirudi unakimbilia kusema mabaya ya wenzako waliofanya. Unasema hivi ili kujipunguzia adhabu ya kosa lako. Lakini ukweli ni kwamba bado viboko vinahusika hata kama utajitetea vipi na kuwasema wengine.
Kwenye Maisha ya sasa bado inawezekana una tabia kama za mtoto huyu ambaye akisaharibu anakimbilia kuanza kujitetea kwa kusema wengine walivyohusika kusababisha yeye akakosea. Unakutana na mtu ana sababu kibao kwanini hajaweza kufanya biashara, watu walivyomkwamisha, watu walivyomtapeli na mengine mengi.
Lakini hapo unasahau kwamba kuna mahali na wewe ulihusika kusababisha yote hayo. Tena umehusika kwa kiasi kikubwa sana kusababisha yatokee. Ila kwasababu hupendi kuonekana una makossa basi unakuja na sababu tele.
Haijalishi utajitetea kwa nguvu kiasi gani haibadilishi chochote kwenye Maisha yako. Kama ni umaskini bado utabaki nao. Kama ni hasara ulipata basi itabakia hivyo kwamba ulipata hasara. Kama ni uzembe wako ulisababisha basi haibadilishi chochote kabisa.
Cha kufanya:
Achana na sababu, achana na kujitetea. Vitu hivyo sio suluhisho la tatizo ulilonalo.
Acha kuwatupia wengine lawama wajibika kwa sehemu yako pale ulipohusika hakikisha unajirekebisha.
Uzembe wako umekusababishia ukatapeliwa, acha kuwalaumu matapeli, wewe pekee ndie uliyewakaribisha Maishani mwako.
Anza sasa kuchukua hatua kubadilisha hali uliyonayo sasa. Usingojee muujiza Fulani utokee. Kuna watu wanaishi kwa kungoja huku wanajiambia lolote linaweza kutokea.
Ndugu yangu hakuna lolote linalotokea bila ya kusababishwa au kuandaliwa.
Achana na hizo hadithi ingia kazini rekebisha pale ambapo umekosea. Tengeneza usonge mbele wakati unakwisha. Kuna nyakati zinakuja unatakiwa uwe umetuliza akili sasa wewe badi utakuwa unahangaika.
KUMBUKA:
Kujitetea kwanini hujaanza biashara mpaka sasa hakuondoi tatizo la fedha ulilonalo.
Kujitetea kwanini hutaki kusoma vitabu hakuondoi ujinga uliopo kuchwani kwako.
Kujitetea kwanini mpaka sasa wewe ni maskini hakukuondolei umaskini wako.
Chagua moja kuendelea kujitetea au kuchukua hatua. Ukiendelea kujitetea utabaki ulivyo ukichukua hatua tutaona mabadiliko maishani mwako.
Jacob Mushi
#USIISHIE_NJIANI