HATUA YA 223: Haitakuwa Rahisi Ila..

Haitakuwa Rahisi Lakini Inawezekana.
Ndoto yako kutimia haitakuwa rahisi lakini inawezekana kutimia.
Kinachotakiwa ni wewe kutambua kwamba inawezekana kutoka ndani yako.
Inatakiwa wewe uamua kwamba japokuwa itakuwa ngumu, japokuwa kuna maumivu ni lazima ufikie ndoto yako.
Mafanikio na ndoto yako sio kitu kidogo hivyo usifikiri unaweza kuyafikia kirahisi tu.
Haijalishi itakuwa ngumu kiasi gani wewe pekee ndiye unaamua kufanikiwa.
Kama ingekuwa rahisi basi kila mmoja angeweza, kila mmoja angeshafika nakotaka.
Kama ingekuwa rahisi kusingekuwa na haja ya kutiana moyo wala kufundishana mbinu mbalimbali.
Endelea kukazana utafika mwisho wa safari yako. mafanikio utayaona.
Usikubali yeyote akwambie haiwezekani.
Tumekuwa na wimbi kubwa la watu wanaotafuta njia rahisi za kufanikiwa, wanasahau kwamba kama zingekuwepo njia hizo wa kwanza kuzijua wangekuwa ni wenye mafanikio tayari.
Hakuna mafanikio nje ya kuweka juhudi kwenye kile ulichochagua mwenyewe kufanyia kazi. Hakuna njia rahisi ambayo ninaweza kukwambia uipite maana hata mimi ningeishaitumia.
Huwezi kujenga ghorofa kwa kuanza na mwisho wa ghorofa lazima uanze mwanzo. Lazima upitie hatua zote za muhimu ili uweze kuwa na ghorofa bora.
Chochote chenye njia za mkato hakiwezi kuwa bora.
Chochote kilichopatikana kwa njia za uchochoroni hupotea kwa haraka.  Inawezekana kama ukikubali kufuata kanuni zilizokuwepo tangu zamani.
Ukubwa wa ndoto yako ndio ukubwa wa juhudi unazotakiwa kutoa. Kile kikubwa unachotaka kitokee kwenye Maisha yako ujue kwamba na gharama nayo utalipa kubwa Zaidi.
Usitegemee kuvuna Zaidi ya unachokipanda sasa hivi. Gharama unazoweka sasa hivi ndio zinaonyesha kule unapotaka kufika.
Hakikisha kila siku kuna jambo unafanya linaloelekeza kule unapoelekea. Kama ni mwimbaji basi kila siku imba hata kama nyimbo hiyo hutaiweka hadharani, tafuta watu wachache uwaimbie, kama ni mwigizaji basi igiza kila siku  peke yako au hata mbele ya watu wachache. Kama ni mwandishi andika kila siku. Hii inaonyesha kwamba kuna mahali unaelekea na unataka kuwa nani.
Chochote kile unachokitaka hakikisha kila siku unakifanyia kazi ili kitokee kwenye Maisha yako.
Jacob Mushi
#USIISHIE_NJIANI
jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading