HATUA YA 226: Jisikilize Zaidi.

Kama kuna mahali panachosha Zaidi kwa kipindi hiki ni kwenye dunia. Kuna kelele nyingi sana ambazo zinaweza kukufanya ukakosa utulivu kwenye kile ulichoamua kukifanya. Kuna watu wengi wanasema sana. Kuna maoni ya kila mtu juu ya kile unachokifanya.
Kuna ambao watakwambia kwanini usifanye hivi, kwanini usifanye vile. Lakini mwisho wa siku sio nani amekwambia ufanye nini ila ni moyo wako unasema unataka nini. Unajua wakati umefikia maumivu ya moyo unaumia mwenyewe sio wale waliokwambia. Wakati unajuta kwa maamuzi mabovu uliyochukua ni wewe mwenyewe utajuta wale uliokuwa unawasikiliza watakuwa hawapo wakati mwingine.
Kuna sehemu inafika inabidi uamue kile ambacho moyo wako unasema na sio kile ambacho watu wanataka ufanye. Unaweza kuzungukwa na watu ambao wanakwambia wewe una kazi nzuri hivyo, mshahara mkubwa sasa unahangaika nini na mabiashara? Unahangaika nini na kujichosha huko? Lakini wewe mwenyewe ndio unajua unahcokitaka. Ukiamua kuwasikiliza ambao wanakwambia unahangaika nini siku sasa utakapopoteza kazi yako hawatakuwa na wewe. Na wakati mwingine hawatakuasaidia hata chembe.
Unakuta wewe mwenyewe ndio unajua shida unazopata kwenye mahusiano yako. unajua mateso unayopata kwenye ndoa yako. lakini watu wa nje wanaweza kukusifia na kukwambia vumilia tu, au achana nae huyo kama umeshindwa. Lakini mwisho wa siku wewe unapaswa kuusikiliza moyo wako unasema nini na sio sauti za nje. Sauti yako ya ndani ndio inatakiwa iwe kubwa. Kama sauti ya ndani inasema sasa basi navunja haya mahusiano, vunja bila kuangalia watu wa nje wanasemaje. Kama sauti ya ndani inasema vumilia endelea kuvumilia. Kwani mwisho wa siku makossa ukiyafanya utajuta mwenywe. Na ukifanya maamuzi sahihi vilevile utafurahia mwenyewe.
Umepokea ushauri mahali popote kabla hujaifanyia kazi hakikisha umeisikiliza sauti yako ya ndani. Wazazi wanaweza kukulazimisha uwasikilize lakini bado wanatakiwa wakusikilize wewe. Unatakiwa uchague kile unachokitaka kutoka ndani yako na sio wanachotaka wewe uwe. Wazazi wanaweza kutaka uwe askari lakini wewe moyo wako unataka kuwa mwalimu usikubali kusikiliza sauti za nje. Maisha ya majuto utakuja kuyaishi wewe mwenyewe. Wakati huo umebeba mizigo uliyobebeshwa ukijitazama unatamani ungekuwepo sehemu nyingine.
Chochote kile ambacho wengi wanasema juu ya Maisha yako hakina nguvu yeyote kama utaamua kuvipotezea na kusikiliza sauti ya ndani. Napenda kukwambia kwamba chagua kusikiliza moyo wako unasema nini Zaidi na sio watu, marafiki, na wanaokutazama wansemaje. Maoni yako yanaweza kuwa mazuri sana lakini yasikufae kwasababu wewe hujazaliwa kuwa hivyo wanavyotaka uwe.
Kuwa mtu wa mwisho wa kuamua kwenye Maisha yako. ukifanya makossa ni wewe utabeba lawama zote juu ya Maisha yako. sio mtu mwingine. Hata kama walikushauri hawapaswi kulaumiwa wewe ndiwe wa kulaumiwa kwa kuchukua hatua bila ya kufikiri. Kumbuka kuna siku zinakuja utakuwa peke yako bila wao.
 Sikwambii usisikilize ushauri wa watu hapana, nakwambia, ukishauriwa sikiliza na moyo wako unasema pia. Kama unapata Amani ya moyo juu ya kile unachoambiwa nenda kachukue hatua. Kama unasitasita na unakuwa na mashaka fikiria mara mbili juu ya ushauri huo.
Chochote unachoambiwa na mwingine usikubali kukipokea kama kilivyo na kwenda kukifanyia kazi kichambue fikiri sawasawa, halafu ndipo ufanye maamuzi.
Usikilize moyo wako kwanza unasema kabla hujafanya maamuzi yeyote.
KUMBUKA: Mwisho wa yote ukikosea ni juu yako mwenyewe, ukifanya vizuri ni juu yako wewe mwenyewe.
“Akili za kupewa changanya na za kwako” –Jakaya Kikwete

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

jacobmushi
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading