Katika kila kitu ambacho mtu anafanya mara nyingi wengi hupenda kutafuta njia rahisi. Hata kama ni safari wengi hupenda kutafuta shortcuts ambazo zitawafikisha kwa haraka. Unachotakiwa kutambua ni kwamba hizo njia fupi zipo lakini unaweza kujikuta unalipa gharama kubwa kuliko hata ule muda uliofikiri unauokoa.

Njia za kufanikiwa kwa haraka mara nyingi watu wamekuwa wanazitafuta na kujikuta wanaingia katika mikono ya matapeli. Ni kweli utasikia hadithi nyingi za kukuvutia juu ya watu walioweza kufanikiwa kwa muda mfupi lakini mar azote hawakwambii ni gharama gani alilipa akayapata hayo mafanikio. Ukishaingia ndani ya mtego ndipo utajionea mwenyewe kumbe kazi ni kubwa kuliko ulivyokuwa unaambiwa kwa nje.

Unaweza kusikia hadithi nyingi na nyingine za kuvutia, ukaonyeshwa walioweza kununua magari, wengine wajenga nyumba nzuri na mengine mengi. Yote hayo yanaweza kuwa kweli kabisa lakini sasa hutaambiwa ni gharama gani alilipa mtu huyo akaweza kuvipata vitu hivyo. Mwisho wa siku wewe unaambia ingia kwanza uone. Ukishaingia unakuta mambo ni tofauti tena ni magumu kuliko hata kule ulipokuwa unakimbia.

Ninapenda kukwambia kwamba hakuna mbadala wa kufanya kazi kwa bidi. Chochote unachokiona kimefikia mahali pa kutamanika kwa nje ujue kuna kazi kubwa imefanyika wakati wewe huoni. Haijalishi imechukua muda gani lakini elewa kwamba kuna kazi kubwa imefanyika. Hakuna kizuri kinachotokea bila ya jasho kumtoka mtu.

Unachopaswa kufanya ni kuchagua kitu ambacho utakifanyia kazi, fahamu misingi yake, simamia misingi hiyo na ufanye kazi kwa bidi. Fanya kazi kama vile hakuna anaekuona. Miaka michache baadae watu wengi watakuwa wanatamani kuwa kama wewe. Miaka michache baadae kuna watu utakuwa unawahadithia ulipotoka na watatamani kufika ulipo.

Tatizo la wengi hupenda kuona kwa macho ya kawaida kwanza ndipo uanze kuchukua hatua. Ukweli ni kwamba macho ya kawaida utaonyeshwa vile vitu vya nje tu. Hutaonyeshwa zile gharama unazopaswa kulipa ili ung’are. Tumia macho ya ndani kuona vitu macho ya ndani ndio yanaona sawasawa.

HAPO ULIPO SASA HIVI: Kama kuna kitu unakifanya sasa hivi endelea nacho kama umeamua kweli kukifanya kutoka moyoni. Fanya kazi kwa bidi bila ya kumuonea aibu mtu yeyote. Kuna siku hao unaowaonea aibu watakuwa hawapo hiyo sehemu uliyofika. Kuna siku hao unaowaogopa watakuwa wanasikia habari zako tu hawajui kinachoendelea. Usiyumbishwe na hadithi au fursa nyingi zinakuja kila siku. Hakikisha umelipa gharama za kutosha ili upate yale mafanikio unayoyataka.

SEMA HAPANA NYINGI ZAIDI: Hapana zikiwa nyingi unakuwa huru Zaidi, ndio zikiwa nyingi unakuwa mtumwa. Kiwango cha fursa ulizozikataa haimaanishi wewe utakuwa maskini inamaanisha kuna kitu umeamua kukifanyia kazi usiku na mchana hadi kilete matokeo. Unajua mwanamke anapoambiwa nakupenda na wanaume wengi halafu akawakubalia anakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kuchagua au kuamua awe na yupi hasa. Lakini unapokuwa na machaguo machache ndio unapata uwezo wakujua ni yupi hasa anakufaa.  Hivyo kwenye fursa pia ni muhimu ukajua wewe unahusika na mambo gani Zaidi kuliko kupokea kila linalokuja mbele yako.

Ni mimi Rafiki Yako,

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading