“Strong minds discuss ideas, average minds discuss events, weak minds discuss people.” 
― 
Socrates

Mwanafalsafa wa zamani sana aitwaye Socrates aliwahi kusema akili kubwa zinajadili mawazo, akili za kawaida zinajadili matukio na akili ndogo zinajadili watu. Ni miaka mingi sana imepita lakini haya maneno bado yanaishi. Kwenye jamii zetu bado tunaona watu wakifanya mambo yale yale ambayo yaliandikwa toka zamani.

Pamoja na mabadiliko makubwa ya teknolojia lakini hakuna mabadiliko kwenye akili zetu na uwezo wetu wa kufikiri. Bado watu wana tabia zilezile ambazo walikuwa nazo kabla ya mabadiliko haya. Kwa maneno haya ya Socrates ni kwamba tangu zamani zao kulikuwa na watu ambao kazi yao ilikuwa ni kujadili watu na matukio.

Yaani hawa watu maisha yao hayaendi bila ya kujadili wengine. Maisha yao hayaendi bila matukio kutokea na wao wakaanza kuyaongelea. Na hadi sasa kwenye kizazi chetu bado tunaona mambo yakiendelea yale yale.

Teknolojia imerahisisha upatikanaji wa habari na taarifa lakini sasa bado taarifa ambazo zinakuwa zinatafutwa Zaidi ni zile zile za matukio na maisha ya watu. Mambo yanayoendelea kwenye mitandao ya kijamii bado ni yaleyale ya kujadili watu na matukio.

Ni vyema ukajiuliza wewe upo kundi lipi?

Upo kwenye kundi gani kati ya makundi haya matatu?

Unajua ni kwanini watu wenye mafanikio ni wachache? Ni kwasababu watu wengi wanatumia muda wao kujadili watu waliofanikiwa na matukio yao. Huku waliofanikiwa wakitumia muda wao kujadili mawazo ya kuwafanya waendelee kuwa na mafanikio.

Sasa na wewe bila ya kujielewa umeshakuwa mtumwa maisha yako hayaendi bila ya kuwa na matukio. Unasubiri tukio litokee upate cha kujadili. Na kwasababu watu wameshajua shida yako ni nini basi kila siku watakutengenezea tukio la kujadili. Mwisho wa siku unakuta miaka inakwenda na hakuna chochote ulichokifanya kwenye hii dunia.

Rafiki yangu usiwe mpumbavu kiasi hicho ukawa unaendeshwa na matukio. Maisha yako yatengenezee matukio yako binafsi. Ukiendelea kujadilia maisha ya watu na matukio huwezi kufika popote. Unajua wanaojadili mawazo ndio wanaoleta matukio? Na wewe umebaki kujadili matukio na maisha yao.

Watu wanakaa chini wanasema tufanye kitu gani ili tuvute umakini wa watu? Wanatengeneza tukio. Na wewe bila ya kuelewa unajikuta umeshabebwa unaanza kuajdili.

Chagua kuwa mtu ambaye anatengeneza maisha yake. Chagua kuwa mtu ambaye na wewe utakuja kuzungumzwa siku moja kwenye mitandao. Na hilo haliwezi kutokea ndani ya siku moja. Lazima ulipe gharama miaka na miaka.

Usipoteze muda wako ndugu. Usiuze muda wako kwenye matukio yasiyo na tija kwenye maisha yako. Lazima uwaze mara mbili mbili kabla hujajiingiza kwenye mkumbo wowote.

Ni mimi Rafiki Yako,

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.

 

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog Bonyeza hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp https://jacobmushi.com/whatsapp/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading