HATUA YA 244: Tenda Wema Nenda Zako.

jacobmushi
By jacobmushi
3 Min Read

Ubinafsi ni kile kitendo cha kutaka kupata wewe peke yako na wengine wakose. Kitendo cha kutokujali wengine na kujifikiria wewe mwenyewe. Kujitoa kwa ajili ya wengine ni kitendo cha kuwa tayari kugawana kile unachokipata na wengine au wakati mwingine kuwa tayari kukosa ili wengine wapate.

Kama wewe ni mtazamaji wa picha za kivita unaweza kuwa umeshakutana na ile sehemu watu wawili wapo wanapambana na maadui. Ghalfa mmoja anataka kupigwa risasi halafu mwenzake anakuja kuzuia risasi zimpige yeye. Kwenye maisha haya tunayoishi ni watu wachache sana wanaweza kufanya kitendo hata kinachofanana tu na hicho.

Ni wachache sana wapo tayari kupoteza vitu vya thamani ili kuokoa maisha ya wenzao walioko kwenye shida.

Kuhusu Kutenda wema, tumejawa na watu ambao wakitenda jambo kwa ajili ya wengine wanataka kila mtu awaone na kila mtu ajue. Mtu akikusaidia akasikia umefanikiwa kila mahali atakapopita atasema yule jamaa nimemsaidia sana siku hizi hata hanisalimii.

Tenda wema nenda zako, usimsaidie mtu chochote kama unajua unatakuja kukikumbuka. Kutoa ni kusahau, unapompa mtu kitu hakikisha haukumbuki kumbuki kile kitu huo ndio utoaji wenye baraka.

Unapomtendea mtu wema usimfanyie ili aje akutendee jambo lingine lolote.

Ngoja nikwambie kitu kadiri unavyowatendea wema watu wengi ndio unarahisisha maisha ya watoto na wajukuu wako yawe mazuri hapa duniani. Hautendi wema kwa ajili yako mwenyewe.

Kuna siku utakuwa haupo na watoto wako labda utakuwa umeondoka duniani au watakuwa mbali na wewe. Huko walipo wanaweza kupatwa na janga lolote lakini kwasababu ya maisha mazuri uliyoishi hapa duniani ukajikuta umewasaidia bila hata ya wewe kuwepo.

Jinsi unavyoishi vizuri na wengine ndio namna unavyowatengenezea maisha mazuri na njia rahisi za kufanikiwa watoto na wajukuu zako hapa duniani. Kuna sehemu milango iliyofungwa itafunguliwa kwa ajili ya watoto  na wajukuu wako kwasababu ya maisha uliyoishi hapa duniani.

Tenda wema, ishi vizuri na kila mtu. Usitengeneze maadui bila ya sababu yeyote ya msingi. Jifunze kusamehe na kusahau, Usiweke vinyongo ndani ya moyo wako.

Hata kama huna pesa nyingi ishi maisha ambayo yatasababisha watoto wako wakijitambulisha mahali wanapokea baraka kwa matendo yako mema uliyowatendea watu.

TENDA WEMA NENDA ZAKO.

Nakutakia kila la Kheri.

Rafiki Yako Jacob Mushi.

www.jacobmushi.com/coach

Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading