Maisha yako hapa duniani ni kwa ajili ya wengine. Haiwezekani ukaishi maisha ya furaha na Amani kama hakuna unachokifanya kwa ajili ya kugusa maisha ya wengine. Tumeumbwa katika maisha ya kutegemeana. Kila mmoja anamhitaji mwenzake ili maisha yake yawe bora. Daktari hawi daktari ilia je ajitibu yeye ila ni kwa ajili ya maisha ya wengine.

Ili sasa uweze kuishi maisha bora sio kuwa na pesa nyingi peke yake bali pia na kuwa na mahusiano bora na wale wanaokuzunguka. Huwezi kuishi vyema duniani na kwa Amani kama huna mahusiano bora na wanadamu wenzako. Wengi wanaoishi kwa hofu wameharibu mahusiano yao na wengine.

Maisha yako yanawategemea wengine kwa kiasi kikubwa na wewe maisha yako yanategemewa na wengine vile vile. Haya hapa ni mambo manne yakufanya ili uweze kuwa na mahusiano bora na wengine.

1.Jua Nafasi yako.

Kwanza kabisa unapaswa kuitambua nafasi yako kwa jamii inayokuzunguka na kwa wale watu unaowajali na kuwapenda. Inawezekana wewe ni baba wa familia, mama, mume, mke, mtoto, kiongozi kwenye jamii, daktari, mwalimu na kadhalika. Ukishajua nafasi yako ni ipi utaweza kwenda hatua nyingine ya kuweza kufanya mahusiano yako yakawa bora.

Kila mmoja ana wajibu wake kwa wale wanaomzunguka. Kama wewe ni baba una wajibu wako kama baba kwa watoto. Kama wewe ni kiongozi una wajibu wako kama kiongozi kwa wale unaowaongoza. Ili uwe na mahusiano bora lazima uutimize wajibu wako kama ambavyo inakupasa.

2.Jitoe kwa ajili ya Wengine.

Kwa kupitia nafasi yako kwa wale wanaokuzunguka unatakiwa uwajali na uonyeshe kuitumia nafasi uliyonayo kwa ajili yao. Kama wewe ni daktari basi linapotokea swala la afya uweze kuwajibika na kujitoa kwa wale ambao unataka kuwa na mahusiano nao bora.

Kama wewe ni baba lazima uwe tayari kuwajibika na kujitoa kuonyesha ubaba wako kwa wale ambao unapswa kujenga mahusiano bora nao. Wanapowaza juu ya mtu wa kuwalea basi majibu yawe ni wewe. Wewe uwe kimbilio kwao wakati wanapohitaji msaada.

3.Usiweke Maslahi Yako Mbele.

Unapokuwa katika nyakati za kutaka kujenga mahusiano bora maslahi yako unayaweka pembeni. Unaweka mbele Zaidi maslahi ya wale ambao unataka kuwa nao karibu. Wakati mwingine kama uliitwa uje utoe huduma mahali kulingana na nafasi yako basi unaweza hata kukataa pesa watakazokuwa wanataka kukulipa kwasababu unataka kujenga mahusiano bora.

Unapojenga mahusiano na mtu wewe unatakiwa ujisahau, sahau kabisa kuhusu mahitaji yako kwa yule mtu unaetaka awe karibu yako. Weka mbele kumjali Zaidi kuliko kingine. Unapojisahau na kuweka shida zako mbele mtu yule atakaa mbali sana na wewe.

4.Usikumbukekumbuke Uliyowahi Kuwafanyia.

Kamwe usiwe mtu wa kukumbuka kumbuka yale uliyowahi kuwafanyia watu. Mfano ulijitoa bure mahali siku moja ukaenda ukaona wanakulalamikia ukaanza kusema nilishawahi kufanya hiki na hiki hata hamkumbuki?

Unapotaka kuwaleta watu karibu yako sahau kabisa juu ya mambo uliyowahi kuwafanyia. Weka Zaidi mbele maslahi yao na shida zao.

Hizi ni baadhi ya njia ambazo ukizifanyia kazi utaweza kutengeneza mahusiano bora kwa wale ambao wanakuzunguka.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading