Kuna msemo wa wahenga unasema ukiona vyaelea ujue vimeundwa. Yaani chochote kile unachokiona kimependeza kwa nje unatakiwa ujiongeze kwamba kuna watu tena inawezekana wasiojulikana wamekifanyia kazi kwa wakati usiojulikana hadi kikaanza kuonekana kwa nje ni kizuri.

Sasa wewe kwa tamaa zako unataka ukipate kile ambacho wenzako wamekifanyia kazi kwa muda mrefu sana hadi ukaanza kuvutiwa nacho kwa kweli huwezi kukipata kwa bei rahisi lazima utawajibika kutoa gharama za kutosha.

Binadamu wengi tunapenda sana matokeo kuliko mchakato unaoleta matokeo. Wengi tunapenda kuona mwisho wa jambo Zaidi kuliko hapa katikati ya safari ambapo ndio panaleta mwisho.

Kabla hujatamani chochote kizuri kwa nje penda kujiuliza ni mchakato gani umefanyika hapo hadi uzuri wake ukaanza kuonekana. Wengi huishia kudumbukia kwenye kutapeliwa kwa kutamani muonekano wa nje peke yake. Wengi hudondokea pabaya kwa kutamani vile vitu ambavyo vinavutia na baadae hulipia gharama kubwa sana kuliko walivyotarajia.

Kama unakwepa kutoa jasho ili upate vizuri unavyotaka basi uwe tayari kutoa fedha za kutosha. Kama unajua huwezi kupata fedha za kulipia nenda tu kaanza mchakato.

Ukiona Mke, Mume mzuri ujue kuna watu wametokwa na jasho hapo hadi ukaanza kuona muonekano mzuri kwa nje.

Ukiona watoto wazuri ujue kuna watu wametokwa na jasho jingi kwenye malezi bora.

Ukiona gari nzuri ya kutembelea mtu anayo ujue alitokwa na jasho jingi kutafuta pesa.

Ukiona chochote kinachovutia macho yako na sio cha asili basi ujue kuna mwanadamu mwenzako aliumiza akili, nguvu zake hadi kikaanza kuonekana hivyo.

Ukiwa mtu unaependa matokeo basi penda na mchakato. Hakuna jambo litatokea lenyewe kwenye maisha yako kama hujalifanyia kazi.

Pia unatakiwa utambue ukikwepa kulipa gharama sasa hivi utakuja kulipa gharama baadae gharama inaweza kuzidi mara mbili ya hii unayotakiwa kulipa sasa hivi.

Mambo mazuri yote unayotaka kubali kulipia gharama. Kubali kujipa muda wa kusubiri matokeo. Haijalishi unataka kuwa mtoto wa kumzaa mwenyewe kwa haraka kiasi gani lazima usubiri miezi tisa. Kuwa mtu wa subira pale unapoamua kulipia gharama ya kile unachokitaka.

 

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog Bonyeza hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

 

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading