HATUA YA 258: Moyo Wako Uko Wapi?

By | October 16, 2017

Mojawapo ya sababu ambazo zinawafanya watu waharibu kazi za wengine ni kufanya kazi huku mioyo yao iko sehemu nyingine kabisa. Wewe umekuwa mwalimu kwasababu uliona ndio utapata kazi kirahisi lakini moyo wako uko kwenye kilimo siku zote utakuwa ni mwiba kwa wanafunzi.

Biashara nyingi zimekosa maendeleo n ahata mafanikio kwasababu ya hawa watu ambao wanafanya kazi wasizozipenda. Kamwe hawawezi kufikiri mbali kwenye kazi, hawawezi kuwa na jambo la maendeleo la kushauri kwenye biashara.

Hawa huwezi kuwasikia hata siku moja wakikuletea mambo ya kuboresha sehemu zao za kazi.

Ukiona kazi, unayoifanya au majukumu uliyonayo yanakuwa kero sana kwako ni vyema sana ukajitafakari kwasababu haiwezekani mtu akachukia majukumu yake hasa kwenye kazi anayoipenda.

Kama upo sehemu ya kuhudumia wateja halafu kero za wateja zikawa ni kero kwako hiyo inaonyesha kwamba moyo wako haupo kwenye kazi unayoifanya kwanza unaifanya kwasababu ya pesa tu.

Hili limekuwa ni tatizo kubwa sana kwani watu wengi wamekuwa wanafanya kazi wasizozipenda hivyo watu hawa wanageuka kuwa wabaya kazini kwasababu tu wanachokifanya hakitoki mioyoni mwao. Ukiona unachokifanya hakitoki moyoni mwako unafanya tu kwasababu kuna mshahara mwisho wa mwezi anza maandalizi ya kuacha hiyo kazi.

Ni vyema sana mtu akafanya kazi kule ambapo moyo wake upo kwasababu ndio tutaona ubunifu, matokeo makubwa na vilevile watu watafurahia sana kile ambacho unakitoa. Kama utafanya tu kwasababu kuna mshahara au ulikosa kitu cha kufanya utaendelea kuwa maumivu kwa wafanyakazi wenzako, bosi wako na Zaidi sana kwa wateja ambao unawahudumia.

Kule moyo wako ulipo ndipo unapotakiwa uwe unapatia kipato Zaidi kuliko kwingine hii ni kwasababu utaweza kujitoa kwa moyo wako wote hadi upate mafanikio. Ukifanya kazi sehemu unayoipenda huwezi kuona kama wateja wanakukera hata siku moja utafurahia kwasababu hiyo ndiyo kazi yako.

Ni sawa na umpe mtu asiyependa watoto akae na mtoto anaelia ovyo ataweza kuwa sababu ya yule mtoto kuendelea kulia Zaidi. Lakini mtoto huyu ukimpeleka kwa mtu anaependa watoto atajua ni kitu gani cha kumpa mtoto ili anyamaze. Hawezi kuona kero mtoto anapolia badala yake atatafuta njia ya kumfanya mtoto akae kimya.

Sehemu ambayo moyo wako upo ni kule ambapo Mungu amekupa wewe kama kusudi lako hapa duniani. Sehemu ambayo moyo wako upo ni kwenye kipaji chako. Sehemu ambapo moyo wako upo ni kule ambapo unasikia kusukumwa Zaidi kufanya kwa msukumo utokao ndani na sio vitu vya nje.

 

FANYA KAZI, WEKA NGUVU ZAKO ZAIDI KULE AMBAPO MOYO WAKO UPO. PESA ZAKO NYINGI ZAIDI ZITOKE KULE AMBAPO MOYO WAKO UNAPENDA.

 

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio Hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog Bonyeza hapa.. BONYEZA MAANDISHI HAYA

 

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *