Nimezoea kuona watu wengi ambao wako chini kwenye vitu Fulani kuwaona wenzao waliowapita kama wana dharau sana.

Mfano mtu mwenye bodaboda atasema watu wenye magari wana dharau na hawawajali bodaboda.

Vilevile maskini ataona matajiri wengi wana dharau, wanajisikia, wanajiona, hawawapendi maskini. Ni wachoyo na mengine mengi.

Kama na wewe umeshakuwa na hisia kama hiyo kuona kwamba aliekupita vitu Fulani anajisikia au anadharau Fulani inawezekana ni kweli mtu huyo anadharau lakini pia inawezekana hana dharau ni hisia zako tu.

Ukweli ni kwamba mara nyingi watu hawa tunaowafikiria hivi hawako hivi, mara nyingine wanatupenda na kutujali kuliko tunavyofikiri. Japo sio wote wapo pia wenye dharau na kujisikia sana lakini ukiwaona hawa ujue hizo mali hawajatafuta wenyewe.

Mtu yeyote aliepambana na kuuumia akapata kile alichokipata hawezi kudharau walioko chini yake. Hawezi kuwadharau wanaopita kwenye njia ile aliyokuwa anapitia yeye.

Mara nyingi ni hisia hasi za kukataliwa ndio zinatuongoza na kujikuta tunawaza kwamba mtu huyu ana dharau sana. Lakini ukija kuchimba kwa undani Zaidi unakuja kugundua hakuna kitu kama hicho.

Hisia za kujiona chini na kujidharau mwenyewe ndio zinakufanya unafikiri kwamba alie juu yako ana dharau.

Hisia za kukataliwa ndizo zinakufanya uone wengine hawakujali na wanaringa au mengineyo yanayotokea kwenye hisia zako.

Usikubali maisha yako yakaendeshwa na hisia hizi kwani zinakuwa sababu ya wewe kushindwa kufika kule walipo.

Usikubali kujiona duni, usikubali kujiona hustahili, usikubali kujiona unakataliwa. Ona kila jambo linalotokea katika upande chanya na utaweza kuwa na maisha yenye mafanikio na furaha.

Mara nyingi watu waliofanikiwa Zaidi yako wanaweza kuwa hawana muda wa kutosha kufanya kile ambacho kila mtu anataka kwasababu pia wapo watu wengi kama wewe ambao wanategemea kutendewa mema na watu waliowapita kimafanikio. Hivyo kile kitendo cha mtu kuwa shughuli nyingi sana kinawafanya watu wafikiri wamedharaulika au wameonekana hawana maana.

Unachopaswa kujua ni kwamba kuna hatua unatakiwa uvuke ili uende kule walipo wale ambao unataka wakujali. Unachopaswa kujua hata wewe unastahili kufika kule walipo haupo kwa ajili ya kusaidiwa maisha yako yote.

Weka juhudi za kutosha utoke hapo ulipo. Ni mara chache sana watu walipo kwenye hatua zinazofanana kuona kama wanadharauliana. Hawa mar azote wanajuana, wanajua hali wanazopitia. Ila mtu akishapanda juu Zaidi ya mwenzake yule alieoko chini huanza maneno huyu jamaa tangu apate gari siku hizi hapokeo tena simu yako, hajibu tena sms zangu. Sawa hakuna shida na wewe toka hapo nenda kwenye kumiliki gari.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading