HATUA YA 264: Unakuwa Kile Unachoamini.

jacobmushi
By jacobmushi
3 Min Read

Unakuwa Kile unachokiamini, kuamini kunakuja kwa kupitia njia mbalimbali kwanza ni kusikia, kuona, na wakati mwingine kusoma. Tukianza na kusikia kama akili yako na ufahamu wako utakuwa umeupa nafasi ya kusikia mambo mazuri yanayoendelea utajenga Imani ya mambo mazuri. Kama utaipa nafasi ya kusikia mambo mabaya yanayoendelea utajenga Imani ya kwamba kuna hali mbaya sana inaendelea.

Ukishajenga Imani yeyote kwenye ufahamu wako maisha yako yote yanakuwa yanaifuata ile Imani uliyojijengea. Kama Imani ile ilikuwa ni njema basi maisha yako yatakuwa bora sana na endapo Imani ile itakuwa ni mbovu basi utaona hali mbaya kwenye kila unachokigusa.

Unajipa ruhusa ya kusikia nini? Unajipa ruhusa ya kuona nini? Unajipa ruhusa ya kusoma nini? Chochote unachoingiza kwenye ufahamu wako kwanza kinakwenda kujenga Imani. Kama utakuwa unasikia jambo moja kwa muda mrefu litajijenga ndani yako na utakuwa unaamini ni hivyo.

Ukikaa na watu wanaolalamika na kusema hali ni ngumu sana kipindi hiki baada ya muda utaanza kuamini. Kama una biashara siku ikatokea kwamba hali haijaenda vizuri badala ya kutafuta suluhisho utajipa majibu ya kile unachokiamini kwamba hali ni ngumu. Hivyo badala ya kufikiri ufanye nini unajipa majibu rahisi kutokana na Imani yako kisha unaendelea na mambo mengine.

Unaposhindwa kutatua changamoto moja basi utafanya changamoto hiyo iendelee kuwa kubwa na kutengeneza matatizo mengine. Ukikosa pesa hata ukiulizwa au mtu anaekutegemea kama ni mke au watoto utawajibu kile unachoamini. Utajibu hali ni ngumu sana kipindi hiki yaani biashara haina wateja kabisa. Pesa imekuwa ngumu sana. Lakini chanzo cha haya yote ni ile Imani iliyokuja kwenye ufahamu wako kwa kusikia kutoka kwa marafiki zako.

Kama unataka kuendelea mbele usipende kabisa kujijengea Imani ambazo ni vikwazo kwako. Imani mbovu ambazo zinakufanya uamini mabaya, kutokuwezekana, au kushindwa. Hata kama ni tafiti zinasema ndio usijijengee Imani kutoka kwenye tafiti jenga Imani bora na maisha yako yatakuwa bora.

Matendo yetu yanaongozwa na kile ambacho tunaamini. Ni ngumu sana kupata matokeo nje ya kile unachokiamini. Ukiamini kutokuwezekana ukiona mtu kafanikiwa utasema ni bahati.

Badili Imani yako na maisha yako yatakwenda kuwa bora sana.

Jacob Mushi

USIISHIE NJIANI

“Piga Hatua”

TAGGED:
Share This Article
Follow:
Jacob Mushi is a Tanzanian Author, Minister, Entrepreneur, Founder and CEO of NETPOA.
Leave a comment

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading