Siku moja nikiwa maeneo ya stand nikakutana na watu wawili wakigombania Tsh elfu mbili mmoja katika hasira sana akamwambia mwenzake wewe mbona unakuwa kama umekuja stand jana?
Kwa hasira sana mwenzake akajibu kwamba nipo hapa tangu mwaka 96 nikashangaa sana kuona watu sh elfu mbili inawafanya wajivunie kuwepo kwenye kitu kile kile bila ya mabadiliko yeyote kwa Zaidi ya miaka 20.
Hapa napenda ujifunze kitu kwamba shida ulizonazo, umaskini ulio nao sio kitu cha kujivunia. Sio kitu cha maana sana kusema upo kazini kwa miaka 40 sasa na maisha yako hayajabadilika chochote.
Haina maana yeyote kuendelea kuweka nguvu zako na akili zako kwenye kitu ambacho hakileti mabadiliko kwenye maisha yako.
Ni kupoteza muda kama utaendelea kufanya kitu kile kile kwa akili zile zile, mtazamo ule ule halafu utegemee mabadiliko.
Mbaya sana ni kwamba akili yako ikizoee hali Fulani itakuambia kwamba hayo ndio maisha na mwisho wake utajikuta umekwama sehemu moja bila kusonga mbele.
Kama ambavyo wewe ulipozaliwa hukubakia mtoto unakua na kuongezeka ndivyo hivyo pia unapaswa kukua na kuongezeka kwenye sehemu nyingine za maisha yako.
Unapaswa kutoka sehemu uliyopo au uliyokaa kwa muda mrefu.
Mawazo makubwa uliyonayo yataweza kuleta matokeo endapo utaelewa kanuni ya kukua na kuongezeka kwenye maisha yako.
Kukua na kuongezeka hakuji kama hufanyi uwekezaji kwenye akili yako. Kama utaendelea kujua yale yale unayoyajua, utabakia kama mti uliokosa maji ndani ya jangwa.
Kinachokufanya ubakie hapo ulipo siku zote ni akili zako kuwa vilevile zilivyo zimekosa mabadiliko ya aina yeyote.
Wekeza kwenye akili yako kila siku, nawe utakuwa kwenye kila sehemu inayotumia akili.
Jacob Mushi