Huwezi kuishi kwa furaha na Amani duniani kama una mtazamo wa kuwakandamiza wengine ili wewe uonekane upo juu.
Kuna mtazamo ambao wengi wanao na wamekuwa wakiamini kwamba ili uwe juu lazima wengine wawe chini. Ili uwe Tajiri lazima wengine wawe maskini, ili uwe na nguvu lazima wengine wawe dhaifu, ili uwe na umaarufu lazima wengine wapoteze umaarufu wao kwanza.
Huu ndio mtazamo mbaya ambao unaleta chuki na watu kutaka kulipizana visasi. Alieko chini akiwa ana mtazamo huu atakuwa anamchukia alie juu siku zote na mipango yake itakuwa ni kumshusha chini ili yeye awe juu. Na yeye alie juu pia siku zote ataishi Maisha ya kuwasukuma wengine chini ili yeye abaki juu siku zote.
Jamii yenye watu wenye mtazamo wa aina hii siku zote inakuwa ni ya ugomvi na kuchukiana. Ukiona mwenzako amepata maendeleo badala ya kufurahi utakuwa unaona wivu na kufikiri kwamba huyu atakuja kututesa na pesa zake.
Kitu Cha Kufanya:
Tunapaswa kujua kwamba kila mmoja ana nafasi ya kufika sehemu yeyote anayoitaka bila ya kumshusha mwenzake. Duniani kuna matajiri wale mabilionea tu Zaidi ya 500 na hawa kila mwaka wanaongezeka. Hii ina maana kwamba kuna uwezekano wa wewe kufika juu bila ya kumuondoa alieko juu kwanza.
Badili mtazamo wako juu ya Maisha na mafanikio, lazima ujue kwamba mwenzako kufanikiwa haikuzuii wewe kufanikiwa. Hata kama mnafanya kitu kimoja kinachofanana. Kila mmoja ana nafasi ya kufanikiwa kwenye jambo aliloamua kufanyia kazi.
Ili uweze kuishi kwa Amani na furaha badili mtazamo wako wapende waliofanikiwa Zaidi yako na wapende walioko chini yako ikiwezekana wasaidie na wao waweze kupiga Hatua. Tunaweza kutengeneza dunia ambayo ina Amani na furaha kama tutaamua kubadilika sisi wenyewe.
Haujazaliwa duniani ili uje kutengeneza vita na wengine upo kwa ajili ya kulitimiza kusudi lako. Anza kuamini kwamba bado unaweza kufanikiwa haijalishi wameshafanikiwa wangapi kwenye unachotaka kufanya.
Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi
#UsiishieNjiani
“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”
Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu
Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog
Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp… https://jacobmushi.com/whatsapp/