Napenda kuchukua nafasi hii ya leo kumshukuru sana Mungu kwa zawadi ya uhai na nafasi ya kuendelea kuwepo hapa duniani. Nashukuru kwa kipawa hiki cha uandishi ambacho kimekuwa faida kwa wengi ambao wamekuwa wanasoma kila siku hapa.
Nimeona nikuandikie mambo 26 niliyojifunza ndani ya miaka hii niliyopo hapa duniani.
- Kuzaliwa ni kama bahati kwasababu hakuna aliejua kama angezaliwa, hakuna alieomba kuzaliwa. Kila mmoja alijikuta tayari akiwa duniani na kuendelea kuishi. Ni vyema kuthamini sana uwepo wako hapa duniani maana ni wa kipekee sana.
- Huwezi kuchagua wazazi wala mazingira ya kuzaliwa. Huu ndio ukweli, hakuna binadamu anaeweza kuchagua azaliwe kwenye mazingira ya aina gani. Ukiona imetokea kwako umezaliwa sehemu yenye neema basi mshukuru Mungu kwa hilo. Usiwadharau waliopo kwenye hali mbaya hawakuchagua ni Mungu ana mpango nao. Usitumie hiyo kama sababu ya wewe kutofanikiwa. Bila kujali ugumu wa mazingira uliyozaliwa bado unaweza kufanikiwa.
- Hakuna aliezaliwa anajua chochote. Tulizaliwa watupu tusiojua kitu lakini ndani yetu kulikuwa na vitu ambavyo vimefichwa. Ni jukumu la kila mmoja kuanza kugundua vitu hivyo. Ni kama vile dhahabu, almasi, mafuta, gesi. Hivi vyote Mungu aliviumba lakini hakusema kama vipo duniani. Alituachia tugundue wenyewe.
- Mazingira yanatengeneza watu lakini sisi tunatakiwa tuyatengeneze mazingira yaendane na vile vitu ambavyo Mungu ameweka ndani yetu. Ukikubali kwamba mazingira yamekuzuia wewe kufikia mafanikio yako utakuwa unamkosea Mungu. Mazingira yapo wewe ndio unapaswa kujitengeneza katika namna ya kuweza kufanikiwa kulingana na maizngira uliyopo.
- Kila mmoja amepita Maisha ya aina yake. Ni mara chache sana utakuta watu wanafanana aina ya safari walizoishi. Lakini ukija kutazama safari yako unakuta inaunganisha dots za wewe kufanikiwa. Kama ulizaliwa kwenye familia maskini basi ujue una nafasi ya kuondoa umaskini. Ulishindwa kusoma mpaka elimu ya juu basi tambua kuna kitu Mungu anataka kwako kitumike kama ushuhuda.
- Ni jukumu lako kutengeneza mazingira na aina ya wazazi ambao unataka watoto wako waje wazaliwe nao. Pamoja na kwamba hakuna anaeweza kuchagua mahali pa kuzaliwa na wazazi wa kumzaa. Basi sisi tuliokwisha kuzaliwa ni jukumu letu kuwaza ni aina gani ya mazingira tunataka kuwaleta watoto wetu? Ni aina gani ya wazazi tunataka kuja kuwa kwa watoto wetu?
- Usipojitambua utaendelea kutengeneza aina ile ile ya Maisha ya wazazi wako, au mbaya Zaidi. Kama ulizaliwa kwenye mazingira ya kimaskini na ukashindwa kutambua kwamba ulizaliwa hapo kwa kusudi gani unaweza kujikuta unaendelea kutengeneza aina ile ile ya Maisha ya wazazi wako. Ni vizuri tukatambua tumezaliwa tuje kuleta mabadiliko. Tumezaliwa kufanya mambo ya tofauti Zaidi ya vile tulivyokuta.
- Ubinafsi ndio unaturudisha nyuma. Kuna aina nyingi za ubinafsi kwenye dunia hii lakini ubinafsi wa kutaka kuendelea kubakia wewe sehemu ile uliyopo ni mbaya sana. Kutaka kuendelea kwenye nafasi uliyopo bila kujali wengine ndio hatari Zaidi. Watu hawahitaji sana uwasaidie kwa pesa wakati mwingine ni namna unavyoonyesha kuwajali wengine inatosha kuwafanya watu wajisikie Amani na kusonga mbele Zaidi.
- Duniani hakuna raha kama hakuna wengine. Yaani wewe na kipaji chako sio wa pekee sana kama wengine hawatajua vipaji vyao na kuvitumia. Tuseme dunia ingekuwa ni waandishi tu kungekosekana vitu vingi sana. Mimi binafsi nisingefurahia sana maana napenda sana kusikiliza nyimbo. Hivyo basi kila mmoja na kile ambacho Mungu ameweka ndani yake ni kwa ajili ya kuipendezesha dunia na kuifanya iwe mahali bora kwa kuishi.
- Usijione wewe ni bora kuliko wengine. Ukitaka kuishi kwa Amani na furaha kamwe usiwe mtu wa kujiona wewe ni bora au wewe unafanya vizuri sana. Acha watu waseme, acha watu wakusifie lakini wewe jishushe sana chini.
- Thamani ya Maisha inapimwa kwa idadi ya watu ambao umewagusa kwa kile ambacho umepewa ndani yako.
- Kama zilivyo gesi, almasi dhahabu na mafuta, ndio na baraka za Mungu zilizopo ndani yako. Ni jukumu lako kujua ni namna gani unaweza kuzitoa ndani yako.
- Ukitaka kufika mbali kubali kujitesa, kuumia, kukosa usinginzi, kusemwa vibaya, kutokutambuliwa. Kuna mengi yanatokea kwenye Maisha sio kutuumiza bali kuonyesha kwamba bado tunatakiwa kufanya kazi kwa bidi Zaidi.
- Mafanikio ya wengine hayapaswi kuwa huzuni kwako bali kukukumbusha wewe kwamba unatakiwa kuongeza bidi sana.
- Mtazamo wako umeathiri sana Maisha ya wengi. Badili namna unavyotazama mambo na mazingira utaona fursa nyingi ndani yake.
- Makossa ndio yanaonekana kwa urahisi Zaidi. Ukiona umefika sehemu ambayo ukikosea watu wanakusema sana basi jua unatazamwa na wengi. Haijalishi kwamba hawakukupongeza ulipofanya mazuri cha muhimu ni wewe kutengeneza tu pale ulipokosea.
- Mambo magumu, watu wabaya, nyakati za hatari zinapaswa kutufundisha sana ili tuweze kuishi kwa adabu na nidhamu kwenye Maisha ya mafanikio.
- Wapo watu ambao hawatakaa wabadilike. Huu ndio ukweli tangu kale kuwekuwa na watu wanatamani kuibadili dunia lakini ukweli ni kwamba watu hawatakaa wabadilke wote na wawe kitu kimoja bado wabaya wataendelea kuwepo, wajinga, wapumbavu, waoga, na wenye bidii, wenye mafanikio, wenye mtazamo chanya. Unatakiwa kufanya kwa nafasi yako.
- Ukilea tabia mbovu zitakuabisha siku moja. Tabia yeyote ambayo unailea taratibu ipo siku itakuwa kubwa na italeta madhara kwako.
- Tatizo likiwa kubwa uistegemee kulitatua kwa siku moja. Kuna watu wanakuja na changamoto ambazo zimejengwa miaka na miaka halafu anataka ushauri ambao akiuchukua na kwenda kuufanyia kazi siku moja abadilishe kila kitu. Ukweli ni kwamba kama ilivyo tatizo halijatokea tu ndani ya siku moja basi itakuchukua siku nyingi pia na juhudi Zaidi kutatua.
- Nimekutana na mtu akaniambia wewe unaandika umeshafanya kitu gani hasa hadi uandike? Nikawaza na kutafakari mara mbili. Kidogo ile kauli ingeniharibu lakini nikaweza kuishinda. Ukweli huhitaji kufanya vitu vikubwa ndipo uweze kuandika kwasababu kuandika sio lazima uandike ulichofanya wewe unaweza kuandika walivyofanya wengine ambao sio waandishi na watu wakaweza kujifunza kupitia kwenye maandishi hayo. Usikubali maneno ya watu wasiojua kwanini unafanya unachokifanya yakakuzuia wewe.
- Kile unachotoa ndio kilaleta vitu kwako. Kama hakuna unachotoa basi hakuna utakachopokea.
- Ongeza thamani ya unachotoa ili thamani ya unachotoa iongezeke. Ukitaka kuongezeka ongeza thamani ya kile unachokitoa lazima matokeo yake yatakuwa makubwa.
- Maisha ni shule kubwa sana kama kila mmoja ataamua kuishi kama mwanafunzi. Kuna mengi sana ambayo unaweza kujifunza na ukafanya vitu vikubwa kwa kuitazama tu dunia ilivyo.
- Ishi Maisha ambayo yatakufanya uje kuwa mfano wa kuigwa.
- Usikubali kubaki wa kawaida, kila unapojiona umezoea sehemu basi tafuta sehemu nyingine ya juu Zaidi ambayo itakufanya usiwe kama umezoea hapo ndipo utakuwa unaongezeka.
- Nakupenda sana Rafiki yangu, wewe ndio unanipa hamasa ya kuendelea kuandika. Nikiona umesoma Makala Napata nguvu Zaidi.
Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi
#UsiishieNjiani
“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”