Tunayaelewa mambo kulingana na uwezo wetu wa kufikiri na namna mitazamo yetu ilivyo. Kama ni hivyo basi utakuwa ni upotevu wa muda usio na msingi kabisa kama utakaa kwenye kundi la watu ukibishania, mpira, siasa, dini, au kitu kingine chochote.

Kila mtu anaweza kutetea kile alichokiamini, sio rahisi ubadilishe Imani ya mtu kwa maneno matupu Zaidi sana labda umwonyeshe ishara. Itakuwa ni upotevu wa muda kama utakuwa unakaa na mtu mnabishania jambo ambalo yeye Imani yake iko tofauti na wewe.

Rafiki yangu kama mabishano unayojichanganya nayo hayakuingizii chochote achana nayo. Labda iwe ni mdahalo maalumu uliondaliwa wenye lengo la kupanua mitazamo ya watu, lakini ile ya vijiweni ya kupigiana kelele mara nyingi huwa ni kupoteza muda. Mara nyingi unaweza kujikuta jambo lile lile linabishaniwa na kamwe halifikii muafaka kwasababu kila mmoja ana Imani yake.

Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. –Methali 13: 20

Mnyama aina ya nguruwe anaamini matope ndio sehemu yake ya kuchezea, lakini wewe binadamu unaona matope ni uchafu. Sasa kama utakuwa unabishana nae juu ukweli matope ni uchafu utakuwa unapoteza muda, na kamwe hawezi kukubaliana na wewe juu ya unalomwambia.

Ni bora kujiingiza katika mjadala unaokufanya uongezeke maarifa kwenye kichwa chako badala ya kupoteza muda na watu mkijadili jambo lile lile kila wakati. Unakuta watu wamekaa kijiweni kubishania mchezo wa mpira ambao kiuhalisia hakuna kinachoongezeka kwao. Lakini hutawakuta hata siku moja wkaijadili mambo yenye faida kwa taifa au hata kwa Maisha yao wenyewe.

Upotevi mkubwa wa muda ambao kwa sasa umeshika kasi ni kwenye mitandao ya kijamii. Watu wengi ni rahisi sana kuchangia mada hasi iliyowekwa kwenye mtandao kuliko mada chanya yenye msaada kwao. Watu wengi ni rahisi sana kupoteza muda kukosoa nguo aliyovaa msanii kuliko hata kujiuliza ni namna gani wanaweza kufika pale alipo.

Ndugu yangu acha kuuza muda wako kwenye vitu visivyo na matokeo bora kwenye Maisha yako. Una mengi sana ya kufanya, kuna mengi mazuri ya kufuatilia na kuchangia. Usikubali kujiweka katika kundi la wpaumbavu wengi wanaopoteza muda wao wakijadili upumbavu na mizaha.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog

Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp… https://jacobmushi.com/whatsapp/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading