Kama tunasema kila binadamu ana upekee wake basi ni kama zilivyo mbegu za mimea mbalimbali. Kila mbegu ina muda wake wa tofauti katika kuonekana imeanza kuchipuka kutoka ardhini. Ukipanda mahindi au maharage unaweza kutegemea kuuona mmea umeanza kuchipuka siku ya tatu hadi saba. Lakini tukija kwenye mimea mingine kuna ambayo hupita muda mrefu sana hadi uonekane. Unaweza kusahau kabisa kama ulipanda mbegu.

Tunapokuja kwenye suala la watu kutaka kuona mabadiliko kwenye Maisha yako wewe tambua kwamba hayo hayawahusu sana. Wewe umepanda mbegu endelea na yale yanayokupasa kufanya kama ni kunyeshea endelea kunyeshea. Acha kutaka kuwaridhisha watu, kwasababu hawakusaidii chochote Zaidi ya kukuzungumzia tu.

Sio kila mti utaonekana faida yake kwa wakati mmoja. Kuna miti mingine ilioteshwa kwa ajili yam bao na mingine ilioteshwa kwa ajili ya matunda. Usijisikie vibaya ukiona mwenzako ameanza kutoa matunda. Jua kusudi lako wewe ni lipi. Inawezekana wewe ni kwa ajili ya mbao na hivyo basi bado miaka mingi sana ukomae na ufae kwa mbao. Wakati huo huo ukumbuke kuna mahindi yalishavunwa baada ya miezi mitatu ya kuoteshwa, sasa kama wewe unaiga watu au unajilinganisha na wengine Maisha yako yote utabaki unaumia.

Unatakiwa pia utambue kwamba sio kila mti ambao upo kwa ajili ya mbao basi hutumika tu kama mbao. Mbao pia zina thamani tofauti tofauti, kuna zinazotumika kwa ajili ya kuezeka paa, nyingine hutumika kama fenicha za ndani. Ukijitambua wewe unatakiwa kuwa wapi huwezi kuonea wivu nafasi za wengine. Wewe ulitengenezwa ili uje kukaa kwenye paa usipojua hilo utaishia kuumia kwasababu unaona wenzako wanakaa sebuleni kama meza au viti.

Ukiweza kulijua kusudi lako vizuri kamwe hutapoteza muda wako kuwaiga wengine, wala kujaribu kuiga wenzako. Sio kila mtu ataweza kuwa maarufu inawezekana kusudi lako halikupi nafasi ya kuwa maarufu sasa wewe usilazimishe umaarufu utajikuta unapotea.

Jua kusudi lako ili usilazimishe mambo ambayo sio yako. Jua kusudi lako ili usilazimishe majira ambayo sio yako. Jua kusudi lako ili usiige wengine.

Ni mimi Rafiki Yako, Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

“Piga Hatua, Timiza Ndoto Yako.”

Jipatie Vitabu vya Biashara na Mafanikio… https://jacobmushi.com/patavitabu

Tengeneza Kipato kwa kupitia Blog ….. https://jacobmushi.com/jipatieblog

Karibu Kwenye Kundi Maalumu la WhatsApp… https://jacobmushi.com/whatsapp/

 

 

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading