HATUA YA 356: Kujua Mtoto Atazaliwa Haitoshi.

Mama anapobeba ujauzito kwa kawaida inajulikana kwamba ni baada ya miezi 9 ndipo mtoto huzaliwa. Kadiri muda unavyokwenda kuisogelea ule mwezi wa 9 ndipo shauku huwa kubwa juu ya kupokea mtoto. Kitakachowafanya wawe na nguvu kubwa Zaidi ya kufurahia mtoto ajaye ni pale daktarin anaposema mtoto atazaliwa tarehe 25 au 26.

Vile vile kwenye Ndoto na malengo ambayo unayo kinachofanya upate nguvu kubwa na shauku Zaidi katika kutimiza ni pale unapokuwa umeweka malengo na Ndoto zenye muda maalumu wa kutimia. Acha kabisa yale mambo ya kusema ipo siku na mimi nitaendesha gari. Usiendelee kujidanganya ipo siku utakaa kwenye nyumba nzuri. Jiwekee mipango ya kutimiza kile unachokitaka.

Kujua mtoto atazaliwa haitoshi kwasababu kinachotupa nguvu na uhakika wa kuzaliwa kwa mtoto ni pale tunapojua kwamba atazaliwa baada ya miezi 9. Ndoto na malengo yasiyo na muda maalumu wa kutimia ni sawa na kutamani kitu ambacho kilishakupita.

Kama mpaka sasa hujajua malengo yako yatatimia lini unapoteza muda Rafiki yangu. Kama nikikuuliza mwaka 2025 utakuwa unafanya nini au utakuwa mtu wa aina gani ndugu yangu unapaswa ujipange la sivyo utapata tabu sana kutimiza hizo Ndoto unazoziota.

Unapaswa kuzitengeneza Ndoto zako ziwe zako kweli yaani uanze kuziishi. Maneno yako yaongee Ndoto zako, matendo yako yatende Ndoto zako. Kila unachokifanya kitoe ishara ya kule unakotaka kufika. Kuna vitu ukivifanya huhitaji kusema wewe ni nani bali watu wanajua huyu atakuja kuwa mtu Fulani. Mama mjamzito hujulikana kwa vitendo Zaidi na wala sio tumbo. Dalili za ujauzito ni za muhimu Zaidi kwasababu tumbo kuwa kubwa linaweza kuwa ugonjwa au kitambi tu.

Hakikisha umeanza kuziandika Ndoto zako. Kama huna kitabu cha Ndoto zako kanunua baada ya kusoma Makala hii. Usiendelee kufanya maigizo na Maisha yako Rafiki yangu. Kile unachokifanya mara nyingi ndio kinaleta matokeo Zaidi kwenye Maisha yako. Au niseme hivi hakikisha kile unachokifanya mara kwa mara ndio kinaleta matokeo makubwa Zaidi kwenye Ndoto zako.

 

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

This entry was posted in HATUA ZA MAFANIKIO on by .

About jacobmushi

Jacob Mushi ni Mwandishi wa makala, nukuu na vitabu vya Maisha na Mafanikio, Kocha wa Maisha na Mjasiriamali. Kiu yake kubwa ni kuona wewe unakuwa mtu bora, unatimiza ndoto zako na unaishi Maisha ya mafanikio. Kazi yake kubwa ni kuhakikisha wewe hauishii Njiani kwenye lile kusudi ambalo Mungu ameweka ndani yako.

2 thoughts on “HATUA YA 356: Kujua Mtoto Atazaliwa Haitoshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *