Unaweza kukaa kwenye jamii ambayo haikuelewi kutokana na matendo yako au yale ambayo unayanena juu yao. Unaweza kukaa na marafiki ndugu au hata wazazi wasioelewa kusudi la wewe kuwepo hapa duniani. Kila mmoja anaweza kukupa tafsiri yake kulingana na uwezo wake wa kuelewa.

Kitu cha muhimu sana sio vile watu wanavyosema juu yako bali ni vile wewe unavyosema juu yako. Wapo watu wanaweza kusema yule amefeli kidato cha nne haweza kufika popote. Wengine watasema kwao hakuna mtu hata mmoja mwenye mafanikio hata yeye hawezi.

Wengine watasema angalia kwao, wote wa kike walizalia nyumbani, hata yeye ataishia kupewa ujauzito na huyo anaesema ni mchumba wake na atakuwa kama wenzake tu. Wengine wanaweza kusema kwenu mna laana, mmetupia majini na mikosi ya kila namna. Hizo zote ni Imani na fikra zilizopo ndani yao.

Kama wewe utasema juu yako kile ambacho watu wanasema juu yako utakuwa umejipoteza. Unapaswa kusema kile ambacho unaamini kwamba Mungu amekuleta duniani kuja kufanya. Usikubali maneno ya watu yawe ni maneno yako.

Naomba nikwambie haijalishi baba yako ni nani, haijalishi chochote kibaya ambacho kimewahi kutokea kwenye Maisha yako. Haijalishi watu wanasema mambo mabaya kiasi gani juu yako. Mimi nakuita mshindi, wewe una nguvu kubwa ndani yako, unaweza kuitimiza Ndoto yako.

Unaweza kuzishinda changamoto, unaweza kufanya mambo makubwa kwenye Maisha yako. Kuna sehemu ya juu kabisa unaweza kufika kwenye kile Mungu alichokuitia. Ungekuwa upo kwa bahati mbaya hapa duniani huenda ungeshakufa siku nyingi. Labda mimba yako ingeshaharibika, labda ungeshapata ajali na kufariki, lakini kwasababu Mungu ana mpango na Maisha yako ndio maaana upo hai mpaka sasa.

Endelea mbele kwenye kile ambacho umeanza kufanya na Usiishie Njiani. Kama bado unaogopa kuanza basi nikutie moyo anza sasa, unaweza kufikia ushindi mkuu sana.

Marko 8: 27- Walipokuwa njiani, Yesu aliwauliza wanafunzi wake, “Watu wanasema mimi ni nani?” 28 Wakamjibu, “Wengine wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine Eliya na wengine mmojawapo wa manabii.” 29 Naye akawauliza, “Na ninyi je, mnasema mimi ni nani?” Petro akamjibu, “Wewe ndiwe Kristo.” 

Hujaja duniani kupoteza muda, sababu ya wewe kuwa hai mpaka sasa ni kwamba Mungu ana kusudi na wewe.

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Jiunge na Usiishie Njiani Academy Hapa https://jacobmushi.com/academy/

Huduma Zetu https://jacobmushi.com/huduma/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading