Kwenye jambo lolote kubwa au la tofauti na ambalo halijawahi kufanyika na watu wengi mar azote unapotaka kufanya unakuwa na hofu sana. Sio kawaida ya watu kuongea mbele za watu na imekuwa inaonekana wale wanaongea mbele za watu ni wenye akili sana lakini sio kweli unaweza kuwa mjinga lakini ukijiamini vya kutosha unaweza kusimama mbele za watu ukaongea.

Jambo lolote likishawezekana kufanywa na kila mtu haliwezi kuwa gumu tena kwa yule ambaye anaanza kufanya kwa mara ya kwanza. Changamoto inakuja pale ambapo unapotaka kufanya jambo ambalo ni wachache wamefanya au halijawahi kufanyika kabisa.

Jamii nzima itakwambia haiwezekana, ndugu zako watasema utatuaibisha, utashindwa,  na mengine mengi. Zote hizo ni hofu zinatengenezwa kwa ajili yako. Jamii inakutaka wewe ufanye vile vitu ambavyo imezoea kuona vinafanyika. Na kama ukiona unachokifanya kila mtu anakikubali basi kitu hicho hakina matokeo makubwa sana. Kama kila mtu anaweza basi thamani yake inakuwa ndogo.

Sasa ili uweze kushinda hofu yeyote ambayo inakujia unapofanya jambo ambalo halijawahi kufanyika kabisa au ambalo jamii ya huko kwenu haijawahi kufanya unapaswa uwe umejipanga vyema. Hakikisha umejenga mtazamo wako vizuri ili uweze kukabiliana na maneno ya watu. Hakikisha wewe mwenyewe umeishinda ile hofu ya kujitengenezea mwenyewe. Kuna maneno Fulani yanakuja ndani yako, “hivi nitaweza kweli?” “Hivi nikishindwa itakuaje” badilisha maneno hayo uwe na maneno mengine ambayo yanakufanya upate nguvu Zaidi. Anza kujiona ukiwa umefanikisha kile unachotaka kufanya.

Chukua Hatua kidogo kidogo kila siku usisubiri siku moja uanze. Hofu inaleta kuahirisha na hapo ndio hofu inazidi kuwa kubwa Zaidi. Kama umesema utafanya leo fanya le oleo, ukisema nitaanza kesho na kiwango cha hofu kinaongezeka.

Chukua Hatua haraka iwezekanavyo hasa kwa yale mambo ambayo yanakufanya uwe na hofu. Kama tu jambo ambalo unalifanya haliwezi kuuondoa uhai wako, haliwezi kukufanya uonekane una tabia chafu, haliwezi kukufanya uonekane hufai kwenye jamii yako, basi chukua Hatua mapema sana. Usiogope kushindwa au kupata hasara. Kama baada ya kupata hasara utakuwa bado hai basi hilo ndio la muhimu Zaidi.

Hofu inaondolewa kwa kuchukua Hatua mapema na sio kuahirisha. Ukiendelea kuweka pembeni vile ambavyo unaviogopa au unavyoona ni vigumu ndio unaikuza hofu yako.

Chukua Hatua, hiyo ndio dawa pekee ya hofu.

Ubarikiwe sana,

Rafiki Yako, Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

2 Responses

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading