Unaweza kukutana na mtu akakufanyia kila jambo zuri na mengine hujawahi kufanyiwa na mtu mwingine yeyote hapa duniani. Utajisikia rah asana na kumuona ni mtu wa kipekee sana kuwahi kutokea kwenye Maisha yako. Endapo wengine wataulizia kuhusu mtu huyo unaweza kumwaga sifa nyingi sana juu yake. Sasa hili ndio nataka ufahamu inawezekana mtu akakutendea kila jambo jema na akaonesha tabia njema kwako kwasababu tu anakuhitaji.

Tabia halisi ya mtu ipo pale anapowatendea watu ambao hawahitaji kwenye Maisha yake. Wale ambao anakutana nao t umara moja na hakuna uhakika wa kukutana nao tena. Zile tabia ambazo mtu anazionesha ndio tabia zake halisi. Mara nyingi tumekuwa tunajidanganya kwa kuwatazama watu yale wanayotutendea kisha tunasema hawa watu ni wema sana. Lakini ukweli ni kwamba mtu anaweza kuwa mwema sana kwako kwasababu kuna kitu anahitaji kwako na njia pekee ya kupata ni kukufanyia wema.

Vile ambavyo mama anamfokea binti wa kazi bila sababu yeyote au kosa linaloeleweka ndio tabia yake. Hata kama ataongea vizuri sana na watoto wake bado tabia yake halisi ni ile aliyoonesha kwa msichana wa kazi. Vile unavyowafanyia usiowahitaji ndio ulivyo kabisa. Ukitaka kuthibitisha hili angalia mahusiano yako na wale watu ambao haupo nao tena karibu kwenye Maisha yako.

Wale watu ambao ulikuwa nao karibu sana na sasa haupo nao kwasababu mbalimbali. Inawezekana mliachana, biashara au kile mlichokuwa mnafanya hamfanyi tena. Kile kinachoendelea baada ya kuachana ndio tabia yako ya ndani.

Kuna watu wakiwa wanahitaji kitu kwako wanaweza kuwa wema sana kiasi kwamba ukasema hawa watu walikuwa wapi siku zote kwenye Maisha yangu? Subiri baada ya muda wapate walichokifata au wagundue kwamba hakuna uwezekano wa kupata kile walichokuwa wanataka. Ghafla sana utaona mawasiliano yamekatika na hali imekuwa tofauti kabisa na mwanzo. Wewe bila kujua unaweza kusema huyu mtu kimembadilisha nini tena? Mbona hakuwa hivi? Ukweli ni kwamba tabia yake halisi ndio hiyo ile ya mwanzo alikuwa anaigiza tu.

Urafiki wa kweli na unaodumu ni ule ambao unaunganishwa bila ya kutazama ni nini unakwenda kupata kwa mtu huyo. Mahusiano ya kudumu yanajengwa kwa kutazama kitu gani unakwenda kutoa kwa mtu na sio kwenda kuchukua. Watu wengi wameshindwa kudumu kwenye mahusiano kwasababu wanaingia kwa mawazo ya kwenda kufaidika, na kila wanachofanya ni maigizo tu ili wapate kile walichokuwa wanatarajia.

Tabia yako halisi ni ile unayoonesha kwa watu ambao huna faida yeyote unayopata kwao. Vile unavyozungumza na mhudumu wa mgahawa mbele ya mpenzi wako, ndio tabia yako hiyo.

 

Rafiki Yako,

Jacob Mushi

#UsiishieNjiani

Dakika 20 za Mafanikio https://jacobmushi.com/dakika20/

Usiishie Njiani Academy https://jacobmushi.com/whatsapp/

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading