Kwenye dunia hii hakuna kitu ambacho utakifanya uwe umeanza peke yako. Chochote unachotaka kukifanya kuna mtu alishakifanya au bado anaendelea kukifanya. Ni muhimu sana kufahamu ni nani anafanya kile unachotaka kufanya au unachokifanya. Nia ya kufahamu sio ili umjue mshindani wako hapana ni ujue nani wa kujifunza kwake.
Ukifahamu mtu huyu au watu hawa wanaofanya kile unachokifanya wewe ndipo unaweza kufanya mambo makubwa Zaidi na ya tofauti pia.
Lazima ujiulize maswali kadhaa ya msingi kabisa ili uweze kufanya mambo ya tofauti.
Ni nani anafanya hii Biashara ninayofanya?
Amefikia mafanikio Makubwa kiasi gani?
Ni vitu gani naweza kujifunza kwake?
Mimi Binafsi nataka nifike wapi?
Ni vitu gani hafanyi naweza kuvifanya kwa ubora Zaidi?
Nafikaje Huko ninakotaka kufika?
Ukiweza kujiuliza maswali haya na ukayapatia majibu utagundua upo sehemu gani. Na utapata nafasi ya kubadilisha na kuboresha mambo mengi sana kwenye hicho unachokifanya.
Hakikisha kuna mtu anafanya hicho unachokifanya na amefikia mafanikio makubwa huyo awe ni mtu unaejifunza kwake kila wakati.
Mtu huyu awe ni ambae unamfuatilia mara kwa mara kuliko mtu mwingine yeyote. Shida kubwa tuliyonayo tuna kizazi sugu sana kisichoelewa kinapoelekea hivyo unakutana na mtu hana hata mpango wa kuwa mwimbishaji sehemu yeyote lakini mtu anaefuatilia habari zake na kumjua sana ni mwanamuziki Fulani. Mwingine hana mpango wa kuwa mchezaji au hata mchambuzi wa michezo au tunaweza kusema hana mpango wa kufanya chochote kinachohusiana na michezo lakini anafuatilia mpira kuliko kitu kingine chochote.
Soma: Jenga Msingi
Lazima ujue unachokifanya kwa nguvu kina faida gani na Maisha yako. Nguvu zako nyingi unazitumia kwenye kitu gani? Unamfuatilia nani Zaidi? Anahusika vipi kwenye Maisha yako? Ana mchango gani kwenye Maisha yako ya baadae?
Weka vipaumbele kwenye kila unachokifanya.
Karibu sana.
Jacob Mushi