Mafanikio yako yamebebwa na watu wengine. Ili uweze kufika mbali lazima uwajue watu ambao ni sahihi kwenye mafanikio yako. Pesa unazozihitaji zipo kwa watu sasa ni jukumu lako kujua ni watu hasa wanazo pesa zako. Na sio kuishia kujua tu ni lazima kwanza uwe umejua wewe una kitu gani ndani yako ambacho kitakuongoza kuwajua watu wenye pesa zako.

Watu hao wamegawanyika katika Makundi matatu:

Marafiki.

Hawa marafiki ni watu ambao wanapenda kazi zako na wapo tayari kulipia gharama ili wapate kazi yako. Kama huna hawa watu haijalishi unatoa kitu bora cha aina gani utaendelea kuwa na Maisha magumu. Na hawa sio wale marafiki kwenye mitandao yako ya kijamii hapana. Nawazungumzia wale watu ambao wako tayari kuwaambia wengine juu ya vitu unavyofanya, bidhaa zako, Huduma unazotoa na kadhalika.

Ukiweza kupambana ukawapata hawa marafiki kuanzia 1000 wewe unakuwa umefikia kiwango cha juu cha mafanikio. Mfano wewe ni Mwandishi wa Vitabu na umefanikiwa kuwa na hawa marafiki zako 1000 elfu moja kisha mwezi huu ukawa unatoa kitabu kipya ambacho utakiuza tsh 10,000/= elfu kumi. Kwa kawaida hawa ni watu tumesema ukitoa bidhaa zakoi wako tayari kuzinunua kwa namna yeyote ile hivyo basi utaweza kuuza kitabu chako nakala elfu moja kwa muda mfupi tu. Ambapo itakuwa ni kama tsh 10,000,000/= yaani milioni kumi.

Basi tuachane na Habari za Vitabu kama utakuwa na bidhaa ambayo wewe unauza na kwa mwezi mzima mtu mmoja anaweza kukupa faida kidogo sana ya tsh 10,000 tu. Halafu wewe umeshakuwa na marafiki zako elfu moja basi bado utaweza kutengeneza tena milioni kumi kila mwezi.

Hawa marafiki hawatengenezwi kwa siku moja lazima ukubali kufanya kazi muda mrefu tena kwenye kitu kimoja au vitu vichache mpaka watu wavielewe na kuvikubali. Inaweza kuchukua hata miaka 5 au Zaidi ukiwa unafanya kazi tu.

Marafiki wa Karibu.

Hawa ni wale watu ambao wapo tayari kukutetea mbele za watu hata kama umefanya kosa kweli. Hawa ni wale marafiki ambao wapo tayari kukwambia ukweli pale unapoharibu au unapofanya vibaya.

Hawa mara Nyingi hawatakiwi wawe wengi sana kwenye Maisha yako. Na wanaweza kuwa ndugu zako wa damu, marafiki tu mliojuana kitambo, mke wako au mume wako, mchumba au yeyote yule.

Naomba nikwambie hawa ndio watu wa muhimu sana katika mafanikio yako kwasababu hawa ndio wanaweza kukutengeneza au na kuwa na wewe kuliko hata wale marafiki elfu moja. Hawa ni watu ambao watakuwa na wewe siku zote uwe umepoteza pesa, umaarufu unaumwa umeachwa, umepata dhuruba mbalimbali watakuwa karibu yako siku zote.

Mentors/Kocha

Hawa ni aina ya marafiki au watu ambao wameona kile kitu kikubwa ndani yako na wakakubali kukulelea hadi ufikie mafanikio makubwa. Kwa nchi zetu za Africa Hatuna sana watu hawa lakini kadiri siku zinavyokwenda wanaendelea kuwepo taratibu.

Kwa sasa unaweza kuwa na mentor yeyote yule unaemchagua wewe kwasababu mitandao ya kijamii imetufungulia njia za kukutana na watu mbalimbali ambao hata hatujawahi kuonana. Unaweza kujifunza kwa kupitia historia ya mtu ambaye wewe umechagua awe mentor wako na ukajifunza kwenye Maisha yako na ukafanikiwa sana.

Ili uweze kuwa na mafanikio lazima ukubali kuwa mnyenyekevu, lazima ukubali kujifunza, lazima ukubali kuwa mvumilivu, lazima ukubali kuonywa, kugombezwa, na pia kupitia mitihani mbalimbai unayopewa.

Unaweza kukutana na mtu akakupa mtihani ile siku ya kwanza tu ukafeli, mfano umekuja kwangu kuniomba ushauri Fulani nikakupa mtihani au kazi ya kufanya na nikakwambia ukifanya uniletee majibu ya ulichopata labda umefanikiwa au umefeli uniletee majibu. Sasa wewe kwasababu sijui ya nini ukaishia huko huko, mimi binafsi nitakuona haukuwa makini sana. Hata shuleni ili uweze kufanikiwa lazima ukubali kufuata yale ambayo Mwalimu anakupa.

Mara nyingine tunaweka gharama kwasababu ya watu ambao ni wazembe. Unakutana na mtu anakuja anaomba ushauri kisha unampa ushauri anaondoka zake baada ya muda ukimfuatilia unakuta alishaacha kile alichokwambia anataka kufanya. Sasa nikiweka gharama kidogo unakuwa unaona uchungu wa pesa yako na pia mimi mimi niliekuwekea gharama nakufuatilia kwa karibu sana.

Ukifuatilia kwa makini wanafunzi wengi waliokuwa wanafaulu darasani walikuwa wanapenda kuwa karibu na waalimu wa yale masomo ambayo walikuwa wanafaulu vizuri. Hii nayo ni kitu cha kujifunza kama unataka kufaulu kaa karibu na Mwalimu wako, mweleze ni wapi unakuwa huelewi na atakusaidia na utaweza kufaulu kwenye kile unachokifanya.

Je ungependa niwepo kwenye Kundi gani kwenye maisha yako? Najua umejfunza kitu, Unakwenda kuchukua Hatua Gani?

Rafiki Yako,

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading