Ukweli ni kwamba ukitafuta kueleweka utakuwa unawachanganya watu badala ya watu kukuelewa. Kitu ambacho unaweza kukifanya pekee ni kuendelea kufanya kile unachoamini, endelea kuwa wewe hata kama watu wanakupinga.
Kutaka kueleweka na kila mtu ni kazi ngumu sana ambayo wengi walishashindwa. Ukianza kuishi kile unachokiamini kuna watu wengi wataendelea kukufuata kwasababu wataanza kuamini kile unachokifanya.
Unapofanya bila kuangalia watu wanasemaje au wanatoa maoni gani unakuwa unapata mwelekeo sahihi ule ambao uko ndani yako. Ukifanya unachokifanya kwa kusikiliza maoni ya kila mtu mwisho wa siku utapoteza mwelekeo.
Endelea kusonga mbele hata kama hakuna anaekuelewa ipo siku kile unachokifanya kitaleta maana na ni pale watu watakapoanza kuona matunda yake. Tajiri Namba moja wa dunia kwa mwaka 2018 kwa mujibu wa jarida la Forbes wakati anaanzisha Mtandao wa Amazon watu wengi ikiwemo marafiki zake walimdharau sana.
Wengine walimwambia unaanzisha Mtandao wa kuuza Vitabu mbona watu wamezoea kwenda kununua kwenye maduka ya kawaida? Hakuna atakaenunua Vitabu vyako. Ukizingatia tena Jeff Bezos alikuwa ameacha kazi yake nzuri sana tena alikuwa CEO na analipwa mshahara Mkubwa sana wengi walimcheka.
Sasa kama Jeff angepoteza muda wake kutaka kila mtu amuelewe anataka kufanya nini labda tusingekuwa na Amazon leo. Kuna watu hawatakaa wakuelewe mpaka waanze kuona matunda ya kile unachokifanya kwa hiyo wewe endelea mbele tu bila kujalisha ni nani anakupinga au kukukatisha tamaa.
Rafiki Yako,
Mwandishi na Kocha wa Mafanikio
Jacob Mushi