Shule ya Sekondari niliyosoma kulikuwa na waalimu ambao nawakumbuka mpaka sasa. Mwalimu mmoja alisifika sana kwa kufundisha vizuri sana, Mwalimu mwingine alisifika sana kwa kuchapa viboko. Wote ni waalimu lakini mmoja ana sifa ya kazi yake na mwingine ana sifa ya kuchapa. Hapa kuna kitu cha kujifunza Rafiki wewe unataka sifa gani kwenye kile unachokifanya?

Unataka watu watu wakutambue wewe kwa sifa gani? Kile unachokipa nafasi Zaidi ndio kitaonekana na kusikika kwa watu Zaidi. Umekipa kitu gani nafasi kwenye Maisha yako?

Ulipokuwa mdogo ulijengewa mtazamo wa ukikosea unapigwa. Na hii imejichora kwenye ufahamu wako wa ndani kiasi kwamba unakuwa unaogopa kabisa kufanya vitu vikubwa kwenye Maisha yako. Umekuwa ni mtu wa kuogopa kufanya mambo ambayo wengi watayapinga. Kwa kuogopa kukosea umejiweka katikati ya kundi la watu na unajikuta unafanya yale mambo ambayo kila mtu anafanya.

Njia pekee ya kuondoa huo ufahamu wa ukikosea unapigwa ni kwa kuanza kuchukua Hatua sasa ili uweze kuishinda hiyo sauti ambayo inakupa hofu ndani yako. Unapaswa kuiambia akili yako kwamba siku hizi yule Mwalimu aliekuwa anakuchapa ukifeli mtihani hakufundishi tena. Unapaswa kuiambia akili yako yule mzazi ambaye alikuwa anakuchapa viboko kwasababu umejaribu kitu Fulani halafu ukakosea kwa sasa hawezi kukuchapa tena.

Anza kuchukua Hatua Rafiki hakuna mwingine wa kukupiga tena Zaidi yako mwenyewe. Embu kumbuka ulipokuwa mdogo ulivyokuwa na ujasiri wa kufanya mambo makubwa na wakati mwingine yalikuwa yanahatarisha Maisha yako. Kwanini leo umekuwa muoga unaogopa kuanza biashara? Unaogopa kuanza kufanya kile ambacho unakipenda? Umeamua kuwa kama kondoo ambaye anafuata kila ambacho anaambiwa.

Rafiki embu inuka hapo ulipo sio mahali pako, sio mahali panapokufaa ndio maana hauna Furaha. Sio mahali ambapo unatakiwa kuwepo kwasababu hadi sasa unatamani kuwepo sehemu nyingine. Rafiki usijidanganye wewe mwenyewe ndio unaujua ukweli. Wewe mwenyewe unajua kile unachokitaka.

Nakutakia Kila la Kheri Katika Kuchukua Hatua na Kujaribu Vitu Vikubwa.

Rafiki Yako,

Mwandishi na Kocha wa Mafanikio

Jacob Mushi

www.jacobmushi.com/huduma

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading