Hii ni siku ya 45 tangu nimeanza kuandika kila siku mfululizo. Ninatarajia kuandika kila siku hadi mwaka huu upite. Naomba tusiishie njiani endelea kujifunza na ufanyie kazi haya unayojifunza.

Kwenye jamii zetu tumeaminishwa kwamba utapeli ni pale mtu anapokuuzia sabuni badala ya simu, au anapokuuzia kiwanja ambacho kilishanunuliwa. Vilevile pale unapouzwa mali ya wizi.

Lakini kuna huu utapeli umeenea sana kila siku na watu hawajautambua. Kuna siku nimeenda sokoni kununua vitu mara zote hua sina tabia ya kuchagua nikamwagiza muuzaji aniwekee viungo vizuri. Baada ya kumaliza kununua vitu nafika nyumbani na kuanza kupekua vitu nakuta alinichanganyia vitu vilivyooza kabisa. HUU NI UTAPELI. Pesa nimelipa ya halali kabisa lakini kaniwekea vitu vilivyooza.

Unapoamua kufanya biashara ambayo inawagusa watu lazima ukubali kuwa mwadilifu. Kama unatoa huduma hakikisha unafanya kulingana na gharama unayotoza. Kamwe usishuke chini ya viwango.

Kama mtu amelipia huduma ya shilingi elfu kumi thamani ya huduma hiyo iwe elfu kumi. Inasikitisha sana pale thamani ya huduma inapokuwa chini na pesa umewatoza watu kubwa. Huu nao ni utapeli.

Watu wametafuta pesa zao kwa shida unatakiwa uijali pesa yao na kuwapa kile wanachotaka kulingana na pesa waliyolipia.

Wewe umeajiriwa halafu unategea kazini kazi unafanya kwa bidi pale anapotokea bosi. Huu pia ni utapeli. Mwisho wa mwezi mshahara upo palepale lakini wewe ulitegea.

Mwenzako anajitoa kwa kila namna ili wewe uwe na furaha lakini unampotezea tu baada ya kupata kile unachokitaka. Ungefurahia na wewe ufanyiwe hivyo?
Chochote unachokifanya kwa wengine kumbuka kujiuliza ingekuwa ni wewe ungeridhika kufanyiwa hivyo? Ingekuwa ni wewe usingeona pesa zako zimepotea?

Kuna msemo unasema yale usiyopenda kufanyiwa usiwafanyie wengine. Ukweli unaweza usifanyiwe wewe lakini akafanyiwa mama yako, dada yako, kaka yako, mtoto wako, baba yako au mwingine yeyote unayemjali sana. Na kusema kweli lazima utaumia. Kama utaumia basi tambua kwamba hata wale wengine uliokuwa unawaumiza walikuwa wanaumia.
Karibu sana.
Jacob Mushi
Entrepreneur & Author
Phone: +255654726668

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading