Mojawapo ya vitu vinavyowafanya watu wapoteze mwelekeo na kusahau ndoto zao ni kujaza mambo mengi kwenye akili zetu yasiyo na umuhimu. Kama akili yako inakuwa imetawaliwa na mawazo mengi ambayo hayaendani na maono yako ujue ndio matokeo utakuwa unapata kila siku.
Mawazo yako ukishindwa kuyadhibiti utajikuta unaishi Maisha yasiyo na mwelekeo na kupoteza maana. Kile kilichojaa kwenye mawazo yako ndio akili yako hufanyia kazi na kuleta matokeo.
Hakikisha maono yako na ndoto zako zinatawala akili yako kuliko vitu vingine vyovyote. Kuliko marafiki au hata ndugu zako wa karibu sana. Bila kufanya hivyo utajikuta kila wakati unarudi nyuma na unashindwa kuwa mtu mwenye matokeo kwenye kila unachokifanya.
Mawazo yako yakitawaliwa na ugumu wa Maisha au hali ngumu unayopitia sasa utashindwa kusonga mbele na utakosa mwelekeo wakati mwingine.
Mawazo yako Yakitawaliwa na matukio yanayoendelea hapa nchini utajikuta mwaka umeisha na hakuna ulichokifanya kwenye Maisha yako mwenyewe.
Njia za Kudhibiti Mawazo yako Yasitawaliwe na Mambo Mengine yasiyo ya Muhimu.
Acha kufuatilia Habari kwenye Tv au Magazeti (Habari zilizo Hasi) Unaweza kujitetea kwamba kuna mambo ya muhimu lakini jiulize hayo ya muhimu yana mchango gani kwenye Maisha yako kwa ujumla? Mengi utakuta yanakujazia hofu tu hakuna kingine.
Kaa mbali na Mitandao ya Kijamii.
Hizi simu zetu tunaziita simu janja zinatumika sana vibaya kwa kipindi hiki. Mtu anafanya kazi kidogo tayari ameshaingia kwenye mitandao kuangalia kinachoendelea. Mwisho wa siku unakuta kwako hakuna ulichokifanya. Jitoe kwenye group ambazo hakuna unachojifunza.
Unapoamka Asubuhi Kuwa na Dakika 30 wewe Peke Yako.
Tafuta dakika 30 asubuhi kwa ajili yako uwe unazitumia kutafakari Maisha yako yanapoelekea. Yatazame matendo yako kama yanaendana na matokeo unayoyataka. Jifanyie tathimini wewe mwenyewe kulingana na maono uliyonayo.
Soma Maono yako Kila siku.
Kila unapoamka asubuhi kabla hujatoka au hujafanya chochote pitia maono yako yasome tena na tena. Hakikisha yametawala mawazo yako. Hakikisha yamekuwa kitu unachokiongelea Zaidi kuliko kitu kingine chochote. Ukiona wewe unaongelea matukio yanayoendelea nchini kuliko maono yako jua umeshapoteza dira. Jioni kabla hujalala soma maono yako tena. Fanya zoezi hili kuanzia sasa.
Kama utashindwa kudhibiti mawazo yako utajikuta unakosa vipaumbele vya Maisha yako. Kipaumbele kukubwa cha Maisha yako ni maono yako sio kingine.
Karibu sana.
Jacob Mushi

Andika Maoni Yako Hapa

Discover more from Jacob Mushi

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading